December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nane kizimbani kwa kuisababishia Serikali hasara ya bilioni 8

Washitakiwa nane wa makosa ya uhujumu uchumi wakiwemo 7 waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na mmoja Wakili wa kujitegemea wakiingia mahakama ya hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kusomewa mashitaka yanayowakabili.

Daud Magesa na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

WALIOKUWA watumishi saba wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) akiwemo wakili wa kujitegemea wamefikishwa kizimbani na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza wakidaiwa kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 8.3.

Washitakiwa hao katika kesi hiyo ya Uhujumu uchumi namba 10 ya mwaka 2020 kwa pamoja wanakabiliwa na makosa 94 ya kuongoza genge la uhalifu, wizi, utakatishaji fedha, kughushi na kutoa nyaraka za uongo.

Mshitakiwa wa kwanza hadi wa saba katika shitaka la 93 wanadaiwa kuisababishia TPA hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 7.5 ambapo katika shitaka la 94 washitakiwa wote nane wakidaiwa kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 848.6.

Wakisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Bonveture Lema na waendesha Mashitaka wa Serikali Waandamizi Castus Ndamgoba na Yamiko Mlekano wakisaidiwa na Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Dismas Muganyizi.

Mashitaka hayo 94 yamesomwa kuanzia saa 11 jioni mpaka saa 1.05 usiku kwa kupokezana ambapo wakili Ndamugoba amesoma shtaka la 1 mpaka 30, Wakili Mlekano shtaka la 31 mpaka 60 na Muganyizi shtaka la 61 mpaka 80na kisha Ndamugoba akamalizia shtaka la 81 mpaka 94.

Ndamgoba, Yamiko na Muganyizi wakisoma mashtaka hayo kwa nyakati tofauti wamedai, shitaka la kwanza hadi la 71 linawahusu washitakiwa wa kwanza hadi wa saba kuwa walifanya uhalifu huo kwa nyakati tofauti kati ya Januari 1, 2015 hadi Februari 5,2020 wakiwa ni watumishi wa umma.

Aidha, mashitaka ya utakatishaji fedha namba 72 hadi 93 yaliwahusu washitakiwa kuanzia wa kwanza hadi wa saba ambapo shitaka la 94 linawahusu washitakiwa wote wanane.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutoka na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi na kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 26, mwaka huu kutoka na upelelezi kutokamilika na kupelekwa mahabusu.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa wa kwanza ni Deogratius Lema, Aike Mapuli, Marystella Minja, Thomas Akile, Wendellin Tibuhwa, James Mbedule na wakili wa kujitegemea Leocard Kipengele.