Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KIKOSI cha timu ya Namungo FC leo kitakuwa na kibarua kigumu mbele ya Raja Casablanca katika mchezo wake wa marudiano wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Namungo itaingia katika mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu ya kukubali kichapo cha goli 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Machi 10 kwenye uwanja wa Mohammed V ambapo goli pekee lilifungwa na Soufiane Rahimi dakika ya 54 kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji Carlos Protas kuunawa mpira katika eneo la 18.
Licha ya kupata ushindi huo lakini pia Raja walifanikiwa kumiliki mchezo huo kwa asilinia 76 dhidi ya 24 za wapinzani wao na kufanikiwa kupiga pasi 636 ambazo zilizaa mashuti 13 huku matatu pekee yakilenga lango dhidi ya Namungo waliopiga pasi 213 na kupiga mashuti sita na mawili yalilenga lango.
Kutokana na takwimu hizo, Namungo leo wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanalipa kisasi kwa wapinzani wao ili kuweka heshima katika mashindano hayo kwani hadi sasa wenyeji hao ni timu pekee ambayo imepoteza mechi zake zote nne na kukaa mkiani kwa Kundi D.
Kuelekea kwenye mchezo huo, kocha mkuu Hemed Seleman ‘Morocco’ amesema kuwa, wamjiandaa kupambana kwa hali na mali katika mchezo huo ili kupata matokeoa mazuri ambayo yatawafanya kuweka angalau rekodi ya kushinda katika hatua hiyo.
Amesema, kama kocha ana matumaini makubwa ya kutoa upinzani mkali kwa wapinzani wao ambao walishakutana nao katika mchezo wa kwanza na kuwapa wakati mgumu katika uwanja wao wa nyumbani.
Morocco amesema kuwa, wamefanya maandaliai ya kutosha na wachezaji wake wameonesha morali kubwa katika mazoezi yao ya mwisho waliyofanya jana hivyo wanatarajia kila kitu kitakwenda kama walivyopanga.
“Kisaikolojia wachezaji wote wapo vizuri na tutahakikisha tunapambana ili kupata matokeo mazuri, ninaamini kuwa licha ya ubora wa wapinzani wetu lakini wachezaji wangu wataingia uwanjani kwa kujiamini wakiongozwa na nidhamu ambayo pia itatuongezea morali ya ushindi katika mchezo huu wa mwisho kwenye ardhi ya nyumbani,” amesema kocha Morocco.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania