Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
TIMU ya Namungo FC imetamba kuendeleza ubabe kwa Maafande wa JKT Tanzania katika mchezo wao wa kiporo namba 241 wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) utakaochezwa leo kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Namungo itaingia katika mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa goli 3-2 walioupata katika mchezo wa Mei 2 wa Kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation Cup’ uliowapeleka katika hatua ya robo fainali.
Katika mchezo huo, Namungo ilioneka kuwa bora zaidi huku wakipawa magoli yaliyofungwa na Reliants Lusajo dakika ya 23’, 27 na 43 huku yale ya JKT yakifungwa dakika ya 71 na Musa Said pamoja na Najim Magulu aliyefunga dakika ya 88 kwa mkwaju wa penalti.
Licha ya kupanga kubeba alama zote tatu lakini huenda Namungo wakakwaa kisiki baada ya kocha wa Maafande hao, Abdallah Mohamed ‘Bares’ kudai kuwa hatokubali kupoteza mchezo wa pili mfululizo kwa Namungo tena wakiwa katika Uwanja wao wa nyumbani
Akizungumza na Mtandao huu wakati timu hiyo ilipotembelea Bunge, Mwenyekiti wa timu hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Hassan Zidadu amesema kuwa, kama viongozi wana Imani ku bwa na kikosi chao kuweza kufanya vizuri na kuondoka na alama zote tatu.
Amesema, kwa mujibu wa kocha wao mkuu Hemed Seleman ‘Morocco’ mkakati wake ni kushinda mechi zao zote za viporo ili kuweza kukusanya pointi zitakazowaweka katika nafasi nzuri zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu.
“Tunajua kuwa baada ya kuwafunga katika mchezo wa FA mchezo wetu wa leo utakuwa mgumu zaidi kwani nao wamepanga kulipa kisasi. Morali tuliyonayo tunaamini itatuongoza kwenye ushindi kwani mkakati wa kocha wetu, Morocco ni kushinda mechi zote za viporo zilizo mbele yetu pamoja na kushinda mechi zetu nyingine kwani mkakati wetu ni kumaliza Ligi msimu huu tukiwa katika nafasi tano za juu,” amesema Zidadu.
Akizungumzia mchezo huo, Lusajo amesema kuwa, kama wachezaji wamejiandaa kupambana ili kupata ushindi kwani wanatambua wazi ugumu watakaokutana nao katika mchezo huo.
“Tunaamini tutapata matokeo mazuri kwani lengo ni kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu katika mchezo huu na katika kila mchezo wa Ligi ulio mbele yetu kwani hadi saa tuna alama 31 baada ya kucheza mechi 22 hivyo ikiwa hili litafanikiwa basi tuna uwezo wa kumaliza msimu tukiwa katika nafasi tano za juu kama ilivyokuwa msimu uliopita,”.
Hata hivyo kuelekea kwenye mchezo huo, Nahodha wa Maafande hao, Frank Nchimbi amesema kuwa, baada ya kupoteza mchezo katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro hawatakubali kupoteza mchezo mwingine kwa wapinzani wao.
Amesema, tayari walishatambua kosa lao lilikuwa wapi na kufanyia marekebisho na sasa kazi yao kubwa ni kuchukua alama zote tatu ndani ya dakika 90 katika uwanja wao wa nyumbani.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania