December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Namna ya kubadili mtindo wa maisha, kuboresha afya

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Arusha

WIKI ya Magonjwa Yasiyoambukiza imeanza kufanyika kitaifa mkoani Arusha kwa wananchi kufundishwa mbinu mbalimbali za kuepuka magonjwa hayo na pia kuyakabili.

Mbinu hizo zinaendelea kutolewa kwa msukumo wa kipekee hapa Arusha kwa muda wa wiki moja na zitatamatika Jumamosi wiki hii.

Kumalizika kwa wiki ya hii siyo mwisho wa elimu hii bali itaendelea kutolewa kwa njia tofauti pengine bila msukumo mkubwa kama huu ambao unafanywa na viongozi wa kitaifa pamoja na wataalamu waliobobea kwenye Nyanja ya afya.

Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Pauline Gekul ndiye aliyezindua wiki hii akisema kitaifa yanafanyika mkoani Arusha lakini kila mkoa unaadhimishwa kwa namna yake.

Anasema ni jambo la kutiliwa mkazo kwa sababu magonjwa haya yanaongezeka kwa kadri miaka inavyoongezeka hivyo ni muhimu Watanzania kuchukua jukumu la kutumia mbinu za kitaalamu kukabiliana nayo.

“Miaka ya 1990 tafiti zilifanyika na kuonesha magonjwa hayo yanasababisha vifo vya watu kwa asilimia 20, lakini sasa tafiti zinaonyesha yanachangia vifo vya Watanzania kwa asilimi 33 na maeneo mengine inafika asilimia 40,” anasema Gekul.

Anabainisha ubaya mwingine uliopo kwenye NCD ni kwamba yanawakumba hata watoto, hivyo kusababisha vifo kwa watu wakiwa na umri mdogo ulio chini ya miaka 60.

Akatahadharisha kuwa wafanyakazi wa maofisini, akitolea mfano walioajiriwa serikalini, kuwa wapo hatarini kuugua magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu hutumia muda mrefu kufanya kazi zao wakiwa wamekaa.

“Wafanyakazi wa Serikali wapo hatarini kuugua magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kutumia muda mrefu kufanya kazi ofisini ,” alionya na kuongeza pia kuwa wakati wa kwenda na kutoka ofisini hutumia magari.

Anasema kuwa wataalamu wa afya wanaonya kuwa watu wasiofanya mazoezi mara kwa mara wanakuwa hatarini kuugua magonjwa yasiyoambukiza.

Anasema kama mtu hafanyi mazoezi na anakula mara tatu kwa siku ni hatari kwa afya yake kwa sababu haviwezi kutumika kikamilifu na badala yake kujirundika mwilini na kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, matatizo ya moyo, kisukari, saratani na uzito kupita kiasi.

Anasema mazoezi hufanya mwili kutumia chakula cha ziada mwilini na kuufanya mwili kuwa mkakakamavu na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

Kaulimbiu ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza mwaka huu ni ‘Badili mtindo wa maisha boresha afya’ na Gekuli anaelezea kuwa inalenga kuwahamasisha watanzania kuamka na kuachana na tabia pamoja na mitindo itakayowafanya waugue magonjwa yasiyoambukiza.

Miongoni mwa tabia hizo anazitaja kuwa ni kutofanya mazoezi, kula vyakula vyenye wingi wa mafuta, sukari na chumvi.

Tabia nyingine ni matumizi ya tumbaku, dawa za kulevya na unywaji wa pombe uliokithiri.

Anasema kuwa takwimu za magonjwa yasiyoambukiza zinaonesha kuwa yanachangia vifo vywa watu milioni 41 kila mwaka ulimwenguni sawa na asilimia 75 ya vifo vyote.

“Magonjwa haya siyo tishio tu ulimwenguni bali hata hapa Tanzania. Hapa nchini katika miaka 60 magonjwa haya yalikuwa yanasababisha vifo asilimia 20 lakini kwa sasa yanachangia zaidi ya asilimia 33 hadi 40 kwa baadhi ya mikoa,” anaonya.

Ofisa Michezo wa Mkoa wa Arusha, Mwamvita Okemo, anasema “Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo chanzo cha hamasa ya kufanya mazoezi tangu akiwa Makamu wa Rais na sasa anayapa msukumo wa kipekee.

Baadhi ya watu walioshiriki matembezi maalumu ya ukakamavu maalumu wakiwa kwenye uzinduzi wa Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza uliofanyika hapa jijini Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Wonanji Thomas anasema maadhimisho hayo ya wiki ya kitaifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanafanyika wakati takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zikionyesha kwamba magonjwa hayo yanaongezeka duniani kote na kuathiri nyanja zote kimaisha, kiuchumi, kiafya na kijamii.

“Takwimu za WHO za mwaka 2016 zinaonyesha magonjwa hayo yanachangia Zaidi ya vifo milioni 41, ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea katika mwaka huo,” anasema Dk Wonanji.

Anafafanua kwamba magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha yale ambayo hayawezi kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine huku akiyataja baadhi kuwa ni pamoja na shinikizo la juu la damu, kisuksri, saratani, pumu,magonjwa ya akili na Siko seli.

Kwa mujibu wa Dk Wonanji, magonjwa hayo yanachangiwa na vihatarishi vinavyofanana na ambavyo vinatokana na tabia na mtindo wa Maisha.
“Hapa tunazungumzia vilevi hususan tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi au kazi zinazoytumia nguvu na kutozingatia kanuni lishe,” anabainisha.

Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Dkt Godwin Mollel anasisitiza kuwa utafiti uliofanyika nchini mwaka 2018, unaonesha watu wazima milioni 2.6 sawa na asilimia 8.7 wanatumia tumbaku, huku utafiti mwingine wa mwaka 2012 ukionyesha matumizi ya pombe kupita kiasi ni asilimia 29.3 na kwamba asilimia 34.7 ya watu wana unene uliokithiri.

Dkt Mollel anaweka wazi kuwa kwa hapa Tanzania, taarifa ya hali ya magonjwa yasiyoambukiza kwenye jamii inaoneshaongezeko kwa watu 800,000 kwa kipindi cha kati ya mwaka 2018 hadi 2020.

“Mwaka 2018, watu 4,018,180 waliugua magonjwa yasiyoambukiza, lakini kufikia 2020 wameongezeka hadi kufikia 4,795,827. Inaadiriwa wagonjwa wenye shinikizo la juu la damu ni asilimia 26, huku zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa hao wakiwa hawatumii dawa zozote,” anaeleza Dk Mollel.

Naibu Waziri huyo wa afya anasema ongezeko hilo ambalo kwa kadirio ni la watu 800,000 katika kipindi cha miaka miwili linatisha na kwamba kila Mtanzania anapaswa kuchukua hatua kuepuka magonjwa hayo yanayohatarisha maisha hata kuathiri uchumi.

Dk. Mollel ananukuu taarifa za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) kuwa zinabashiri katika miaka 20 tangu mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa hayo zitafikia dola za Marekani trilioni 47, fedha ambazo zingeweza kutumika kupunguza umasikini kwa watu bilioni 2.5 kwa miaka 50.

“Kwa nchi za uchumi wa kati na chini, magonjwa haya yatagharimu mataifa hayo jumla ya dola za Marekani trilioni saba kati ya kipindi cha mwaka 2011 hadi 2025.

“Makadirio yanaonesha gharama za huduma kwa magonjwa hayo itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya afya, huku ugonjwa wa kisukari pekee ukigharimu Zaidi ya dola za Marekani bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya afya duniani,” anasema Dk. Mollel.