January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Namna watoto wanavyoweza kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Judith Ferdinand

“Athari za mabadiliko ya tabianchi hazijalishi umri wala hadhi, lakini sisi watoto tumekuwa waathirika zaidi. Tunaomba msaada kutoka kwa Serikali, jamii, mashirika na wazazi.Ili sisi watoto, tuwe sehemu ya mapambano haya dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Nchi yetu itakuwa ya kijani na yenye afya ikiwa watoto tutashirikishwa kikamilifu katika juhudi hizi,”anasema Bryton George Mwanahabari mtoto kutoka shirika la Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza(MYCN).

Kwani mabadiliko ya tabianchi yamekuwa moja ya changamoto zinazokumba Dunia leo, na athari zake ni dhahiri, hasa kwa watoto,ikiwemo ukame, mafuriko, uharibifu wa miundombinu ya shule, na changamoto nyingine nyingi zinazohusiana na mazingira. Hata hivyo, watoto hawawezi kuwa watazamaji tu katika mapambano haya wanahitaji kuwa sehemu ya suluhisho.

Je?,ni kwa namna gani watoto na vijana wanaweza kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,unagana na mwandishi wa makala haya kujua hayo yote.

Timesmajira Online ilibisha hodi wilayani Ilemela mkoani Mwanza na kuzungumza na Mwanahabari mtoto kutoka shirika la Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza(MYCN),Bryton George,anasisitiza umuhimu wa kuelimisha watoto juu ya mabadiliko ya tabianchi na kuwawezesha kushiriki katika juhudi za kupambana nayo.

Bryton anasema,upandaji miti ni moja ya njia bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwani miti ina mchango mkubwa katika kuimarisha mazingira na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu pamoja na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Kwani sababu moja wapo inayochangia mabadiliko ya tabianchi ni ukataji wa miti ovyo bila kufuata utaratibu wala kuzingatia msemo wa “panda miti, kata mti” pamoja na uchomaji wa misitu. Na kwa mujibu wa mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 2021-2031,inakadiriwa kuwa kiasi cha hekta 469,420 za misitu,hukatwa kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za kibinadamu ,ikiwemo kukata miti kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa hivyo kuchangia kuongezeka kwa ukame nchini pamoja na athari za kiikolojia.

Kwa mujibu wa mpango kazi wa utekelezaji wa kampeni kabambe ya hifadhi na usafi wa mazingira ya 2021-2026,takribani asilimia 16 ya eneo la nchi tayari limegeuka kuwa jangwa.

“Naamini upandaji miti ni njia moja ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake,ambayo kwa sehemu kubwa yamekuwa yakituathiri watoto.Hivyo katika siku zetu za kumbukizi ya kuzaliwa wazazi na jamii kwa ujumla watupe miti ili tusherekee kwa kupanda miti hiyo, kwa mfano mtoto anatimiza miaka 11 apande miti 22, mra mbili ya umri alionao,hii itakuwa ni hatua ya kujenga tabia ya kutunza mazingira tangu tukiwa wadogo hivyo katika kukua kwetu itakuwa ni utamaduni wetu,” anasema Bryton na kuongeza:

“Tukisha ipanda miti hiyo tuifanye kama rafiki yetu kwa kuitunza,kuipenda na kuijali, pamoja na kuhakikisha tunaimwagilizia kila siku ili iweze kukua vizuri na kuifanya Tanzania ya kijani,”.

Hata hivyo shirika la MYCN,halijabaki nyuma,linahamasisha jamii na watoto kuhusu umuhimu wa kupanda miti, na kuelimisha kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Ofisa mradi wa Ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto Mkoa wa Mwanza kutoka MYCN,Nuru Masanja, anasema kupitia mradi huo,wameweza kuzifikia shule mbili za Nyamagana na Ilemela kutoa elimu kwa wanafunzi kisha kupanda miti ikiwa ni njia ya kuhamasisha watoto hao kujua umuhimu wa kupanda miti kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Nyamagana tulifanya kwa shule ya sekondari Lwan’hima Kata ya Lwan’hima ambapo tulipanda miti 100 na tuliwafikia watoto takribani wanafunzi 1044,Ilemela tulifanya shule ya msingi Magaka Kata ya Kahama 1052,tulipanda miti 105,huko kote tulipanda miti ya matunda zaidi kuliko ya kivuli kwa sababu walimu walisisitiza hivyo,”.

Mwanafunzi wa shule ya msingi Magaka,Fedis Samweli,anasema walipokea na kupanda miti shuleni kwao kutoka shirika la MYCN,na kisha kupewa elimu ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na namna ya kuitunza miti hiyo,ili iweze kukua vizuri na kuwasaidia katika kukabiliana na upepo mkali katika maeneo ya shule,kupata kivuli pamoja na hewa safi inayotoka kwenye mimea,kupunguza joto na kusaidia wanafunzi kujisomea vyema.

“Najivunia shirika la MYCN, baada ya kuja hapa shuleni kwetu na kutupa miti pamoja na kutuelimisha, kwani limetufanya na sisi watoto tujue umuhimu wa kupanda miti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,na kujiona kuwa pia sisi ni sehemu ya mapambano hayo,”anasema Samweli.

“Miti 105,ambayo shule yetu ilipatiwa na shirika la MYCN,imekuwa chachu kwa wanafunzi kujua kumbe kile wanachofundishwa darasani kuhusu kutunza mazingira ndicho,pia wamejua kuwa nao wa nafasi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuwa sehemu ya upandaji miti shuleni hata nyumbani na kuitunza,”anasema Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Magaka Mshongo Mmbaga.

Elimu ya mabadiliko ya tabianchi kwa watoto

Mwanahabari mwingine mtoto kutoka MYCN, Brightness Boniface, anasema athari za mabadiliko ya tabianchi zinawakumba watoto kwa njia nyingi, hasa katika upatikanaji wa elimu.

Brightness anasema,mafuriko, ukame, na uharibifu wa miundombinu ya barabara na shule yanayotokana na mafuriko, vinaathiri watoto kwa kiasi kikubwa, kwani hawawezi kwenda shuleni au wanalazimika kubadili mazingira yao ya maisha.

Hii inadhihirisha haja ya elimu ya mabadiliko ya tabianchi kuanzia shule za msingi ili watoto waweze kuelewa ni kwa namna gani mabadiliko haya yanavyowaathiri, na pia waweze kuwa mabalozi wa elimu hii katika jamii zao.

“Elimu hii inapaswa kuwa endelevu,siyo tu kwa watoto,pia kwa jamii na wazazi wao.Watoto wanapojengewa uelewa wa mabadiliko ya tabianchi, wanaweza kuwa na mchango katika kuhakikisha familia na jamii zao zinakabiliana na changamoto hizi kwa njia endelevu,na kufanya kila mtu suala la kutunza mazingira ni maisha yake ya kila siku na atayatunza bila kushurutishwa,”.

kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004,inaeleza kuwa,mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza mazingira, na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira.

Athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto,changamoto

Nuru anasema,athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa kubwa kwa watoto, kwani wanakutana na changamoto za kisaikolojia na kiuchumi. Mfano mzuri wa hii ni pale ambapo watoto wanakosa huduma za msingi kama maji safi na salama kutokana na ukame au mafuriko,elimu,afya.

Itakumbukwa mwaka 2023,mwishoni Katesh Hanang mkoani Manyara yalitokea mafuriko ya matope yaliosababishwa na mvua nyingi zilizonyesha,na kusababisha maafa kwa jamii hiyo ikiwemo watoto baadhi yao walipoteza maisha,na kusitisha kwa muda kuendelea na masomo huku wakiondolewa kwenye makazi yao na kuwekwa kwenye kambi hali ambayo iliwaathiri kisaikolojia.

Sanjari na hayo katika maeneo mengine, kama vile ya uvuvi, athari za mabadiliko ya tabianchi zimewalazimisha wazazi kuhama kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji, na hivyo kuathiri familia nzima hasa watoto kwani wanajikuta wanajilea wenyewe baada ya wazazi kwenda eneo jingine kutafuta samaki kwa ajili ya kipato cha familia.

“Mabadiliko haya pia yanawafanya watoto kushindwa kuendeleza masomo yao ipasavyo, hasa wakati wa mafuriko na ukame. Watoto wanapozuiwa kwenda shule kutokana na mabadiliko haya, wanakosa fursa ya kupata elimu bora ambayo ni muhimu kwa ustawi wao,” anasema Brightness Boniface Mwanahabari mtoto wa MYCN.

Brightness,anasema Serikali inapaswa kusimamia na kutekeleza sera na sheria zinazozingatia mazingira,ili kudhibiti ukataji miti ovyo na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala za kupikia ambazo ni rafiki kwa mazingira ikiwemo,gesi ya kupikia, biogesi na umeme wa jua.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki za Dunia za mwaka 2023,idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia,imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kidogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.9 mwaka 2021,ambapo kiwango hicho ni chini ya kiwango cha wastani cha dunia cha asilimia 71 kwa mwaka 2021.

Hata hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Mei,2024,alizindua mpango mkakati wa miaka kumi (2024-2034),wa kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ,ukiwa na lengo la kuhakikisha unafikia asilimia 80 ya wananchi ambao wanatumia nishati hiyo kwa kipindi hicho.

Mchango wa wadau katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa watoto

Wakati Serikali inahamasisha matumizi ya nishati mbadala, pia inapaswa kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa watu wa rika zote kuhusu njia bora za kukabiliana na mabadiliko haya.

Katika kuhakikisha watoto wanakuwa sehemu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini nchini(RUJAT),kwa ufadhili wa shirika la We World ,lilitoa semina kwa waandishi wa habari juu ya kuandika habari za athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto na vijana.Pia namna watakavyotumia taaluma yao kuhamasisha watoto na vijana kuwa sehemu ya mapambano ya mabadiliko ya tabianchi.

Ofisa Mradi wa Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa watoto Mkoa wa Mwanza kutoka MYCN,Nuru Masanja anasema kuwa mradi huo ni wa miezi 12 unataokamilika Machi mwaka 2025 kwa ajili ya majaribio kwa awamu ya kwanza, ambao unatekelezwa kwa Kata 6 Wilaya ya Ilemela na Kata 11 Wilaya ya Nyamagana.

Una lengo la kuwafikia watoto 100,000 katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana, kwa kutoa elimu kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na njia za kukabiliana nazo. Watoto hawa watakuwa mabalozi wa elimu hii katika familia zao na jamii zao Mwanza.Huku lengo kuu ni kuelimisha watoto, wazazi, na jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kukabiliana nazo.

“Wanufaika wa moja kwa moja ni Wanahabari watoto kutoka MYCN pia Baraza la Watoto Mkoa wa Mwanza ngazi za Wilaya na Mkoa,pia watoto (wanafunzi),shuleni,jamii ,wazazi na walimu,lengo ni kutambua athari zinazowakabili watoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi,”anasema Nuru.

Sababu za watoto kutoshirikishwa

“Kabla ya kuja na mradi huu, tulibaini changamoto ya kutokuwepo ushiriki wa watoto na vijana,katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.Ushiriki wao ni mdogo kwa sababu jamii inaamini kuwa watoto hawana uelewa , wala hawawezi kusaidia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,”anasema Nuru.

Nuru anasema,pia tamaduni zinachangia watoto kutoshirikishwa katika mapambano hayo,huku akitolea mfano jamii ya Mwanza wanaamini mtoto hawezi kufanya kitu chochote cha kimaendeleo au kukabiliana na jambo kama ilivyo kwa mabadiliko ya tabianchi hivyo inaamua kuwaacha nyuma.

“Sisi tukawaza tufanye nini ili watoto waweze kushirikishwa,cha kwanza tukasema tuwape elimu juu ya mabadiliko ya tabianchi ni nini,athari zake,sababu,madhara na vitu vingine na namna ambavyo wataweza kukabiliana nazo pindi itakapo tokea,”anasema Nuru na kuongeza:

“Pia kuimarisha mifumo ya kiserikali ambayo inalenga watoto pamoja na vijana,kama mabaraza ya watoto,kwani tunaamini mabaraza hayo yatapeleka mambo ya watoto kwenye ngazi ya Serikali,kupitia wao mtoto anaweza kujumuishwa katika shughuli mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,”.

Ambapo mpaka sasa wameweza kutoa elimu kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi kwa wanahabari watoto 25 na 40 kwa Baraza la Watoto,Ilemela na Nyamagana.

Nini kifanyike

Licha ya juhudi zinzzofanywa na Serikali na mashirika mbalimbali,Nuru,anasisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii nzima iungane kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu sahihi kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

“Jamii inapaswa kutambua kuwa mabadiliko ya tabianchi hayahusishi tu kilimo, bali pia biashara, usafiri, na sekta zingine muhimu. Kama jamii itashirikiana, watoto wataweza kutunza mazingira na kutoa mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya kijani,”.

Kama ilivyoelezwa na Bryton, kupanda miti ni sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, watoto wanapaswa kushirikishwa katika kupanda miti kwa wingi.

“Hii ni njia ya kutunza mazingira na kujenga kizazi kijacho cha watu wanaojali na kutunza mazingira. Hakika, tunahitaji miti kwa sababu inasaidia kupunguza joto la Dunia, hupunguza upepo mkali, na pia inasaidia kuimarisha mazingira kwa kutoa kivuli na hewa safi,”.