Na Heri Shaaban, TimesMajira Online
Namba zinaongea; ndivyo unavyoweza kusema kutokana na utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM uliofanywa na Diwani wa Kata ya Kivule, Nyansika Getama katika miradi mbalimbali ya maendeleo uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 7.
Diwani Nyansika ambaye aliingia madarakani mwaka 2020 kwa kupata kura 4,250 anaongoza kata hiyo yenye mitaa minne.
Akizungumza jana wakati wa kuwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Sekondari Misitu, alisema fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara katika kipindi cha mwaka 2020 hadi Juni 2024.
Alisema katika sekta ya elimu Sh 1,648,400 zimetumika kuboresha elimu ya msingi wakati Sh 1,891,200 zimetumika kuboresha elimu ya sekondari, Sh bilioni 2.2 zimetumika katika sekta ya afya na Sh zaidi ya Sh bilioni 2 zimetumika kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja, mitaro na kingo za mto.
Alisema wamenunua madawati 2,650, wamejenga vyumba vya madarasa 48, matundu ya vyoo 128 na ofisi za walimu katika Shule za Msingi Kivule, Serengeti, Bombambili, Misitu na Magore.
Aidha alisema katika Shule za Sekondari Abuu Jumaa, Misitu, Kerezange wamejenga vyumba 66, kununua viti na meza (1,420) pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo na ofisi za walimu.
Akizungumzia sekta ya afya alisema wamejenga majengo ya wodi ya wanawake (Sh milioni 240.2), wodi ya watoto (Sh milioni 316.5), jengo la macho na meno (Sh milioni 412), jengo la upasuaji (Sh milioni 191.2) na jengo la kuhifadhia maiti (Sh milioni 78.9) katika Hospitali ya Wilaya ya Kivule.
Nyansika alisema pia ujenzi wa jengo la chuo cha uuguzi unaendelea na hadi sasa Sh bilioni 2.1 zimetumika kati ya Sh bilioni 5 zinazotarajiwa kutumika.
Kwa upande wa barabara alisema Barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola itajengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Pia amesema wamejenga barabara, madaraja, vivuko, mifereji na kingo za mto Magole A, Mkolemba, Kivule, Mto Mbonde.
Diwani Nyansika alisema ujenzi wa kituo cha polisi kinachojengwa kwa ushirikiano wa nguvu za wananchi na halmashauri mpaka sasa Sh milioni 97 zimetumika na kwamba kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kitakuwa kinatoa huduma.
“Imani ya kura zaidi ya elfu nne inaendelea kunipa uwezo wa kusema katika ngazi ya halmashauri na Serikali Kuu, mmeniheshimisha sana, mmenipa ushirikiano mkubwa,” amesema Nyansika.
Baadhi ya wananchi waliozungumza katika mkutano huo walimpongeza diwani Nyansika kwa jitihada zake za kuleta maendeleo ya katika kata hiyo.
Pia walimuomba aendelee kutatua changamoto zilizopo hasa kukosekana usafiri wa daladala katika baadhi ya maeneo, migogoro ya uuzwaji viwanja unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wenyeviti, urasimishaji wa makazi na Kivuko cha kwa Mbonde.
Kwa upande wake Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Omary Kumbilamoto, alisema halmashauri itamalizia ujenzi wa kituo cha polisi.
Pia alisema mwezi ujao watatangaza zabuni za ujenzi wa barabara ambapo baadhi ya barabara za Kata ya Kivule pia zitafikiwa.
Kuhusu uuzwaji viwanja unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wenyeviti wa mitaa, Kumbilamoto aliahidi kulifuatilia suala hilo kwa kushirikiana na diwani huyo na mtendaji wa kata hiyo na kuonya vikali watu waache kutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini