Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Chande amebariki rasmi ujio wa Bahati Nasibu mpya ya Taifa, inayosimamiwa na Kampuni ya ITHUBA, katika hafla iliyofanyika Januari 21 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Ujio wa Bahati Nasibu hiyo ni moja ya hatua katika kuinua Sekta ya michezo ya kubahatisha nchini Tanzania.
Kampuni ya ITHUBA, inayoongoza barani Afrika, katika kuendesha michezo ya Bahati Nasibu, imelenga kuleta mapinduzi katika sekta hiyo, kuchochea maendeleo ya kitaifa, na kutoa fursa kwa kila Mtanzania kushiriki.
Akizungumza mara baada ya kubariki ujio huo Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande ameipongeza Kampuni ya ITHUBA kwa kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini hususani katika sekta ya michezo.
“Leo ni siku ya kihistoria kwa Tanzania, kwa kumkaribisha ITHUBA kama mwendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa, tunatoa kipaumbele katika suala zima la uvumbuzi, uaminifu, na uwazi huku tukileta jukwaa litakalochochea ukuaji wa uchumi, ajira mpya, na miradi ya maendeleo ya kitaifa kwa ajili ya kuinua maisha ya wananchi.
“Kila tiketi itakayouzwa itachangia kuboresha michezo, elimu, na miradi ya kijamii, Bahati Nasibu ya Taifa hii ni mfano wa jinsi michezo ya kubahatisha inavyoweza kutumika kama chombo cha maendeleo endelevu huku ikiwaletea washiriki furaha,” amesema Naibu Waziri Chande.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa ITHUBA Group, Charmaine Mabuza umesisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika maendeleo ya Tanzania.
“ITHUBA inajivunia kushirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa. Dira yetu ni kutoa uzoefu wa hali ya juu wa michezo ya Bahati Nasibu kwa uwazi, kuburudisha, na kusaidia maendeleo endelevu.
“Bahati Nasibu hii si tu kuhusu michezo bali pia ni sehemu ya kuinua jamii zetu na kuwekeza katika mustakabali bora wa Tanzania,” amesema Mabuza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa GBT, Balozi Modest J. Mero amesema Bahati Nasibu ya Taifa itazingatia viwango vya juu vya uwazi na haki lakini pia, umuhimu wa uadilifu katika mpango huo. Hivyo sifa ya ITHUBA katika uwajibikaji wa kimaadili na uvumbuzi unaifanya Kampuni hiyo kuwa mshirika bora.
“Bodi ya Michezo ya Kubahatisha itahakikisha Bahati Nasibu ya Taifa inafanya kazi kwa uwazi na uaminifu kama jukwaa salama linalochangia malengo ya kiuchumi ya Tanzania,” amesema Balozi Mero.
Fursa za Kusisimua za Michezo kwa Wote;
Bahati Nasibu ya Kitaifa itakuwa na mkusanyiko wa michezo mbalimbali ya kuvutia iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kuwashirikisha na kuwaburudisha Watanzania, ikiwa ni pamoja na LOTTO, TAMBA NA NAMBA, SPIN4CASH, na TOBOA CHAP CHAP. Tiketi zinaanzia bei ya Shilingi 100 tu za Kitanzania, kuhakikisha kila mtu anaweza kushiriki.
Mapato ya tiketi yatatumika kufadhili maendeleo ya michezo katika ngazi ya msingi, uwezeshaji wa vijana, na miradi muhimu ya kijamii, kuimarisha jukumu la Bahati Nasibu ya Taifa kama chombo cha maendeleo ya kijamii.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania