Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amewahimiza Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuwajali wateja (custumer care) pindi wanapofuata huduma ili kujenga taswira nzuri ya Serikali kwa umma.
Ndejembi ametoa wito huo kwa Watumishi wa Umma wilayani Sumbawanga, wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Ndejembi amesema, kumekuwa na mtizamo hasi kuwa katika Utumishi wa Umma baadhi ya watumishi hawawajali wateja jambo ambalo halijengi taswira nzuri ya Serikali kwa wananchi.
“Hatuna budi kuwajali watumishi wenzetu tunaowahudumia na wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ndejembi ameongeza kuwa, Serikali haifanyi biashara, hivyo lengo lake kuu ni kutoa huduma bora kwa wananchi ili wanufaike na uwepo wa Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imedhamiria kuwapatia huduma stahiki.
Akizungumzia kuhusu mienendo ya Watumishi wa Umma, Mhe. Ndejembi amesema ni lazima izingatie miiko na maadili ya Utumishi wa Umma ili kulinda na kujenga taswira nzuri ya Serikali kwa umma.
“Tusiwe wa kwanza kuvunja Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo, hivyo ni lazima tufanye kazi kwa uadilifu,” Mhe. Ndejembi amehimiza.
Aidha, Ndejembi amesema kwamba hakuna wakati mzuri kama huu wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa Watumishi wa Umma, hivyo watumishi wanapaswa kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais za kuhimiza masilahi yao kwa kutekeleza majukumu ya kila siku kikamilifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Sebastian Waryuba amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya yake na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa.
Amesema ili wananchi wa Manispaaa ya Sumbawanga wapate faraja ni lazima kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Ndejembi ili kufikia azma ya Rais ya kuboresha huduma zinazotolewa na Serikali kwa wananchi.
Ndejembi amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto