Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA 5) unaofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.
Katika sherehe za ufunguzi wa mkutano huo Khamis aliwasilisha ujumbe maalumu wa Tanzania kuhusu mazingira ambapo alieleza jitahada za Tanzania ilizozichukua katika kukabilina na uharibifu wa mazingira.
Alizitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na kupambana na uharibifu wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki akisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo Tanzania imechukua hatua za kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji na matumizi ya mifuko hiyo.
Pia, Naibu waziri huyo aliongeza kwa kusema kuwa mwaka 2019 Tanzania ilitunga Kanuni kwa ajili ya utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki huku akieleza kuwa ili kufanikiwa unahitajika ushirikiano madhubuti wa kimataifa ikiwemo kuwa na sera ya pamoja na hatua madhubuti za pamoja za kuhakikisha dunia inakuwa salama.
Alisema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeendelea kutekeleza wajibu wake kama ilivyojieleza katika Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC) pamoja na Mkakati wa Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi (NCCRS) wa mwaka 2021-2026.
Naibu Waziri Khamis alisema kuwa mbali ya jitihada hizo pia, Tanzania imeendelea kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Inaelezwa kuwa takriban mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) ambayo yamepitisha maazimio yanayolenga kubuni makubaliano mwafaka ya kutokomeza taka za plastiki kwa kupunguza matumizi yake kutoka vyanzo vyake hadi baharini.
Aidha, wajumbe wa mkutano huo wanatarajia kufikia maamuzi ya pamoja katika hatua za mwanzo za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki ambayo itajwa kama chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira.
Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya chupa za plastiki milioni moja hununuliwa kila dakika kote ulimwenguni kwa matumizi ya maji ya kunywa huku mifuko ya plastiki zaidi ya trilioni 5 hutumiwa kila mwaka duniani.
Mkutano wa UNEA 5 uliofunguliwa Februari 28 unatarajiwa kuhitimishwa Machi 2, 2022 huku ukijumisha wajumbe mbalimbali wakiwemo mawaziri na wadau mbalimbali wa mazingira duniani.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best