Na Judith Ferdinand, Daud Magesa ,TimesMajira Online Mwanza
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Halmashauri, wametakiwa kuhakikisha wanasimamia na kudhibiti mianya ya uingizwaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki ilipigwa marufuku na serikali.
Agizo hilo limetolewa Februari 22,mwaka huu jijini hapa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati alipotembelea dampo la Buhongwa kwa ajili ya kujionea utendaji kazi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza.
Ambapo ameeleza kuwa bado kuna watu wanapenyeza mifuko ya plastiki ambayo haipo kwenye ubora ambao Serikali imeelekeza wanakazi kubwa ya kufanya kila mwenye jukumu lake aende akatekeleze maelekezo hayo.
Ameeleza kuwa wamegundua na wameona katika dampo hilo la Buhongwa kuna taka nyingi sana za plastiki hali inayomaanisha zinatoka mitaani maana yake bado kuna watu wanatengeneza mifuko ya plastiki ambayo serikali imeikataza.
“Natoa maelekezo na wito kwa kila kamati zinazohusika zikiwemo za ulinzi na usalama,NEMC, wasimamizi wa mazingira,wazee wa halmashauri wote wa majiji na miji,hakikisheni kwamba mnasimamia mianya yote inayo penyeza taka na mifuko ya plastiki ambayo ni hatari kwa maisha ya wananchi,”ameeleza Khamis na kuongeza kuwa
“Serikali ilipiga kabisa marufuku mifuko ya plastiki kuingia, kutengenezwa na kutumiwa nchini,maana yake tukiwa tunaiona hapa jalalani maana yake inatengenezwa huko na inatengenezwa kinyume na ile mifuko ambayo ilitakiwa kutengenezwa,”.
Hivyo ameeleza kuwa kazi iendelee na ikafanyike ili wanaojishughulisha na kupenyeza mifuko ya plastiki ambayo imekatazwa na serikali hatua za kisheria kama zilivyowekwa zichukuliwe dhidi yao hakuna namna nyingine.
“Kinyume na hayo kila siku tutakuwa tunalia plastiki,plastiki inachukua muda mrefu kuoza hadi miaka minne na nyingine haiozi kabisa mwisho wa siku unakwenda kusababisha changamoto kwa wananchi,”ameeleza Khamis.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa,wamegundua kuwa taka zinazotolewa mitaani na kupelekwa Dampo katika magari zinadondoka njiani,na hakuna anayeshuka na kusimamisha gari kwa ajili ya kuzoa na kurudisha ndani ya gari zinaachwa.
“Natoa maelekezo kuwa magari yote yanayobeba taka kutoka mtaani kuketa kwenye dampo yafunikwe ili lengo na madhumuni taka zisianguke na kuendelea kuleta athari, unafika wakati unapita barabarani unakutana na mfuko wa pampers na takataka nyingine ambazo mwisho wa siku zinakwenda kuleta athari kwa wananchi.
Pia ameeleza kuwa mtaani kuna watu wanalalamika kwamba wanalipa fedha kwa ajili ya kuzolewa taka zao lakini taka zinaachwa hazichukuliwi wahusika hawapiti na wanachukua muda mrefu kupita kuchukua taka.
“Ikiwa wananchi wanalipia hii huduma ya usafi wa taka maana yake taka zichukuliwe kwa wakati ili zisije zikaleta athari na ndio maana tukaweka haya madampo maalumu ili malengo na madhumuni tusije kuleta athari kwa wananchi,”.
Sanjari na hayo ameagiza eneo la dampo la Buhongwa papandwe miti ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Nimeona katika eneo hili kuna majani ya kawaida hakuna miti,tupandeni miti maeneo haya kwani eneo ni kubwa na kwa ile miti ambayo inaweza kustahimili mazingira ya hapa tuipande ili kuwe na miti mingi ambayo itadhibiti athari za mabadiliko ya tabia ya nchi,”ameeleza Khamis.
Katika hatua nyingine ameeleza kuwa Rais ameipatia Wizara hiyo kiasi cha bilioni 3, kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa na madampo ya kisasa ambayo yapo kisayansi zaidi.
“Hii ndio adhima ya serikali kuhakikisha kwamba pamoja na mambo mengine Serikali kupitia Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais,inakwenda kutengeneza madampo ya kisasa ambayo hayataendelea kuathiri wananchi,”.
Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Desderius Polle,wakati akisoma taarifa ya mradi wa dampo la kisasa la Buhongwa ambalo lina helta 33.81,ameeleza kuwa halmashauri hiyo huzalisha taka tani 357 kwa siku kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo nyumbani, maeneo ya biashara,viwandani pamoja na taasisi za umma na binafsi.
“Halmashauri ya Jiji la Mwanza lina uwezo wa kuhudumia tani 265 kwa siku ambazo kabla ya kusafirishwa kwenda dampo hutunzwa na kuhifadhiwa kwenye vyombo maalumu ya kikusanyia taka ngumu 23,zilizopo kwenye Kata 18 za halmashauri,”ameeleza Polle.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa dampo hilo Polle ameeleza kuwa utekelezaji wake ulianza mwaka 2010 na kukamilika 2020 kupitia mradi wa Tanzania Strategic Cities project kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Denmark(DANIDA), uliogharimu takribani bilioni 8.9(8,952,980,847.95).
“Tumefanikiwa kuzuia uchaguzi wa Mazingira unaosababishwa na utupaji hivyo wa taka ngumu,harufi mbaya inayotokana na kuoza kwa taka ngumu, kutengeneza mazingira ambayo urejeshaji taka ngumu inafanyika kwa usimamizi wa kitaalam na kuongeza kipato Cha halmashauri,”ameeleza Polle.
Diwani wa Kata ya Buhongwa Joseph Kabadi, ameeleza kuwa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo Halmashauri hiyo Madiwani walienda mikoa mingine kujifunza namna ambavyo wanasimamia madampo.
“Kabla ya dampo hili wananchi wanaozunguka eneo hili walikuwa wanatusumbua kutoka na harufu iliokuwa inatoka kwa sasa hakuna harufu na malalamiko yoyote,niiombe halmashauri taka zinapigika hapa wazifukie vizuri na kwa wakati,”.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza Elizabeth Nyingi, ameeleza kuwa Mwanza kwa sasa inaonekana kuwa safi hivyo ametoa wito kwa watumishi wa mazingira kwa kuwahimiza kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji.
“Mazingira ni uhai,nimeona hapa taka za plastiki siyo afya kwa mazingira kwaio niwaombe sana watumishi wetu wa mazingira wa halmashauri tujitahidi sana kuweka mkazo kwenye hizi taka za plastiki ni mbaya sana kimazingira.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa