December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Gekul awataka Wasanii kutumia Mitandao kwa manufaa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amewataka Wasanii nchini kuitumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kutangaza kazi zao ili zifahamike, kukuza sekta ya Sanaa nchini na kuwaletea maendeleo badala ya kutangaza mambo yao binafsi ambayo hayana tija.

Pia, amewataka Wazazi wa Wasanii kulinda hadhi za watoto wao kwa kutowahusisha kwenye migogoro yao ya mahusiano pindi baba na mama wanapofarakana kwani wanawaingiza kwenye historia isiyofaa katika maadili ya Kitanzania.

Gekul aliyasema hayo leo, katika ziara yake kwenye Ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kulitaka Baraza hilo kuongeza umakini katika kusimamia na kuimarisha maadili na mienendo ya wasanii nchini.

“Kama kuna kitu Watanzania hawaridhishwi nacho ni kitendo cha msanii kuelezea maisha yake binafsi katika mambo ambayo hayana tija. Unamkuta Msanii anaweka taarifa zake binafsi mitandaoni kwamba nimezaa na huyu, nina wanawake kadhaa, hii inadidimiza utamaduni wetu, wanatuharibia kizazi hiki ambacho kinakua kuona kwamba ni fasheni kueleza mahusiano kwenye mitandao,” amesema Gekul.

Aidha amesema ni muhimu Sheria na Kanuni zinazosimamia sekta ya Sanaa zikasimamiwa ipasavyo ili kuhakikisha wanaondokana na vitendo hivyo ambavyo amevitaja kuwa vinashusha hadhi ya Wasanii nchini.

“Hivi hakuna Sheria inayowabana, si ipo? au adhabu na fine zimekuwa ndogo sana? Tunasimamia kwa kiasi gani hizo kanuni?, amehoji Naibu Waziri na kueleza kuwa watanzania wanatamani kuwafahamu Wasanii wao kwa mambo mazuri ya kujenga jamii zetu na si kwa mambo yao binafsi.