Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Ujenzi Godfrey Kasekenya,ameziagiza Wakala wa Barabara nchini TARURA na TANROADS kuzifanyia kazi kwa wakati taarifa zinazoletwa na watumiaji wa barabara.
Huku akiilekeza Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kufuatilia na kuhakikisha taarifa na malalamiko yanayoletwa na watumiaji wa barabara yanafanyiwa kazi kwa wakati na Wakala wa Barabara hizo ikiwemo Tarura na Tanroads.
Naibu Waziri huyo Kasekenya ametoa maagizo hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia chi mwenye miundombinu ya barabara na uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara,iliyofanyika jijini Mwanza.
Ambapo ameeleza kuwa ameziagiza Wakala wa Barabara hizo kuzifanyia kazi kwa wakati taarifa zinazoletwa kwao na watumiaji wa barabara kwa lengo la utekelezaji.
“Upatikanaji wa taarifa za hali ya barabara kwa wakati ni moja ya njia muhimu za kutunza miundombinu ya barabara.naipongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kubuni mfumo wa kielektroniki utakaotumiwa na wananchi na watumia barabara kufuatilia na kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya hali ya barabara katika maeneo yao,”Ameeleza Kasekenya.
Pia ameendelea kwa kuziagiza Wakala wa Barabara kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye madaraja na makalavati ili kuepuka kutokea kwa majanga makubwa kama lile la Kiyegeya.
Aidha amezitaka kuingia mikataba ya muda mrefu ya matengenezo ya kawaida ya barabara ili kuziba mashimo yanayotokea barabarani ndani ya saa 48 kwa mujibu wa makubaliano kati ya Bodi na Wakala wa Barabara.
“Naziagiza Wakala wa Barabara kwa kushirikiana na Bodi, kubainisha maeneo hatarishi ya barabara ambayo huathiriwa na mvua mara kwa mara na kuchukuwa hatua stahiki pamoja na kukamilisha manunuzi ya kazi za matengenezo ya barabara kwa wakati kabla ya majira ya mvua na kuzitekeleza kikamilifu,”ameeleza Kasekenya.
Meneja wa Mfuko wa Barabara Eliud Nyauhenga, ameeleza kuwa
kwa zaidi ya kipindi cha miaka 20 iliyopita wameshuhudia uharibifu mkubwa wa mara kwa mara wa miundombinu ya barabara kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa kupita kiasi zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Uharibifu huo ni pamoja na kusombwa kwa madaraja na makalavati kunakoleta usumbufu na hasara kubwa kwa wasafiri na wasafirishaji na kusababisha gharama kubwa kwa Serikali.
“Mfano wa karibuni ni kuzolewa kwa daraja la Kiyegeya mwaka 2020 ambako kulisimamisha kwa muda shughuli za usafiri na usafirishaji kupitia barabara ya Morogoro – Dodoma ambayo inatumiwa na mikoa ya kati, Kanda ya Ziwa na nchi jirani kama Rwanda, DRC Congo na Burundi,kutokana na kusombwa kwa daraja hilo,serikali ililazimika kutumia takribani bilioni 10.89 kujenga daraja jipya na barabara unganishi,”ameeleza Nyauhenga.
Ameeleza kuwa pamoja na ufuatiliaji wa kila siku bodi kila mwaka hufanya tathmini ya utendaji wa Wakala wa Barabara kupitia wataalam elekezi kwa kutumia mfumo wa kutathimini kazi za barabara kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Ambapo vigezo vinavyotumika kufanya tathmini ya utendaji ni umakini katika maandalizi ya mradi, usanifu wa mradi, taratibu za manunuzi, ujenzi au matengenezo ya mradi na kufunga mradi (project closure).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) Joseph Haule, ameeleza kuwa sekta ya barabara ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Bila usafiri wa uhakika wa barabara, ni vigumu wananchi kunufaika na huduma za kijamii na kiuchumi ambazo zinatolewa na kuwezeshwa na Serikali ikiwemo elimu, afya na upatikanaji wa masoko,”ameeleza Haule.
Ameeleza kuwa,miundombinu hiyo inakabiliwa na changamoto zinazopelekewa na mabadiliko ya tabia ya nchi katika nchi mbalimbali duniani kama mvua kubwa,joto kali,upepo mkali pamoja na kuzidishwa kwa uzito wa magari barabarani.
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2020 thamani ya mtandao wa barabara zilizorasimishwa ni trilioni 21 sawa na asilimia 16.
Makumu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) Octavian Mshiu, ameeleza kuwa bodi hiyo itahakikisha kwamba wanasimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliotolewa na Naibu Waziri huyo kwa ukamilifu na kwa weledi wa hali ya juu.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa