Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
WATUMISHI wa umma nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu mkubwa ili utumishi wao ulete matokeo chanya kwa watu na jamii iendelee kuwaamini.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Clement Sangu alipokuwa akiongea na Watumishi wa Umma kwa nyakati tofauti katika halmashauri ya Manispaa Tabora na Nzega Mji.
Amesema kuwa mtumishi wa umma ni mtumishi wa wananchi hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa bidii na uadilifu mkubwa kwa manufaa ya wale anaowatumikia.
Aidha amewataka kuwa wabunifu na kufanya mambo yanayogusa maisha ya wananchi ili waendelee kuiamini serikali yao inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri amesisitiza kuwa Rais Samia ndiye mtumishi namba moja wa wananchi hivyo akataka kila mwajiriwa wa serikali kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa wananchi ikiwemo kutatua kero zao.
‘Kila mtumishi wa umma ameajiriwa kwa ajili ya kutumikia wananchi, sio kufanya mambo anayotaka mwenyewe, serikali inataka kila mmoja alete matokeo chanya katika nafasi yake na si vinginevyo’, ameeleza.
Amesisitiza kuwa kutokutimiza wajibu kunasababisha hasara kubwa kwa serikali na jamii na kunaongeza malalamiko miongoni mwa wananchi, hivyo akawataka kutumia muda wao vizuri wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi.
Naibu Waziri amebainisha kuwa baadhi ya watumishi wanatumia muda mwingi kufanya mambo binafsi ambayo hayana tija kwa jamii, jambo ambalo halikubaliki, hivyo akawataka kubadilika vinginevyo serikali haitawavumilia.
Aidha amewataka kuwa na utendaji wa kimkakati ambao utachochea mafanikio makubwa katika maeneo yao ya kazi hivyo kupelekea wananchi kuendelea kujivunia serikali yao na kuiamini.
Ili kuboresha utendaji wa kila mtumishi, amewataka Waajiri na Maafisa Utumishi wa taasisi za umma zote kuhakikisha kila mwajiriwa mpya anapewa mafunzo ya kazi yake (induction course) ili utumishi wake ulete tija inayotakiwa.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato