October 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Spika ataka mwarobaini kupunguza ajali za bodaboda

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azzan Zungu, ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kutafuta mwarobaini utakao punguza matumizi ya pombe aina ya (sungura) zisizo na vipimo kwa baadhi ya madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda kwani ndio chanzo cha ajali za barabarani.

Akizungumza katika hafla fupi ya kumuaga Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani aliyemaliza muda wake Jumanne Sagini (Mb) Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na kumkaribisha Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Daniel Sillo (Mb) ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi iliyofanyika jijini Dodoma amesema waathirika wakubwa wa ajali za bodaboda ni vijana kutokana na unywaji wa pombe wakiwa barabarani.

“Taifa limepoteza nguvu kazi kutokana na ajali za bodaboda ambazo zinasababishwa na unywaji wa pombe za gharama za chini, ukienda MOI Serikali inatibu vijana ambao wengi wao ni ajali za bodaboda hivyo naombeni msimamie katika kupunguza ajali na kutoa elimu pia sina budi kumpongeza Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani aliyemaliza muda wake Jumanne Sagini kwani sisi sote ni mashahidi kuwa juhudi zake za kupambana na ajali zimeonekana,”amesema Zungu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani aliyemaliza muda wake,Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini alimshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni kwa usimamizi mzuri na ushirikiano mkubwa alioutoa kwa kipindi chote ambacho akiwa Mwenyekiti.

Sagini amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake ni juhudi za wenyeviti na viongozi wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kwani hawakuwa nyuma na yote mazuri yaliofanyika ni ushirikiano wao wote kutokana na timu nzuri iliyoundwa ya ushindi na bado ipo inaendelea.

Kwa upande wake Mwenyekitiki mpya wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo ameeleza kuwa katika Bajeti ya Serikali ya 2024/2025 tayari Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeanza mchakato wa kununua vifaa vya kudhibiti ajali zikiwemo kamera ambazo zitafungwa baadhi ya miji na mitambo ya kisasa ya kukagua vyombo vya moto barabarani.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama (NUU) wakiongozwa na Mwenyekiti wao Vita Kawawa (Mb), pamoja na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.