November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Katibu Mkuu Mmuya: Tuendelee kujipanga kukabili maafa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya amezitaka Halmashauri zote nchini kuendelea kuwa na mipango madhubuti katika kujiandaa na kukabili maafa yanapotokea katika maeneo yao.

Ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Kuthibitisha na Kupitisha Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza Vihatarishi vya Maafa katika Wilaya ya Kyela Jijini Mbeya kilichohudhuriwa na wataalam wa kada mbalimbali kutoka Wilaya hiyo tarehe 25 Mei, 2022 pamoja na kamati ya maafa ya Wilaya.

Alisema Halmashauri zinapaswa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa katika maeneo yao huku akipongeza uwepo wa mpango huo ambao utasaidia katika kujiandaa na kuongeza ufanisi katika uratibu wa masuala ya maafa nchini.

“Naamini Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa katika Wilaya ya Kyela utasaidia na kuongeza ufanisi katika kukabiliana na maafa kwani unaainisha majukumu ya wadau wote wa maafa kabla maafa hayajatokea,”Alisema Mmuya.

Aidha alipongeza jitihada zinazofanya na Halmashauri hiyo katika kuendelea kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea hasa yale ya mafuriko ambayo yameendelea kuikumba Wilaya hiyo huku akiwasihi kuweke vipaumbele vya kibajeti katika kurahisisha utekelezaji wa mpango huo.

 “Natoa wito kwa Taasisi na Vitengo vyote vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kuzingatia vipaumbele vilivyomo kwenye Mpango huu kwa kuweka mikakati katika mipango ya bajeti zetu za kila mwaka”,alisisitiza

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyela Mhe. SACP Ismail Mlawa alisema Wilaya yake itaendela kutekeleza mpango huo kwa vitendo kwa kuzingatia umuhimu wake katika Wilaya yake huku akipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha zinazosaidia utekelezaji wa masuala ya maafa.

“Wilaya yetu imekuwa ikikumbwa na maafa ya mafuriko kutokana na hali ya kijiografia iliyopo hivyo mpango huu umekuja eneo sahihi na wakati sahihi nasi tunaahidi kuutekeleza kwa vitendo,”alisema SACP Mlawa

Akiwasilisha mada Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Mwatima alisema, kila mwananchi ana jukumu la kuendelea kujikinga na maafa kwa kuzingatia masuala ya maafa ni mtambuka hususani katika kutambua vihashiria vya maafa katika maeneo yanayowazunguka.

“Mpango umelenga kuwa suala la maafa ni mtambuka hivyo Taasisi ya Serikali na isiyo ya Serikali inayowajibu wa kushiriki kikamilifu katika kupunguza vihatarishi vya maafa kwa kutumia ujuzi na rasilimali zake, hivyo utekelezaji wa mpango na mkakati huu ni wajibu wa kila taasisi na kila mtu aliyepo katika eneo lake,”Alisema Mwatima.

Aidha mpango utasaidia kuweka mfumo madhubuti wa kujiandaa na kukabili maafa katika Wilaya pamoja na kuongeza uwajibikaji wa kila mdau katika Wilaya katika kujiandaa na kukabili maafa pamoja na kutambua wadau na rasilimali kabla ya maafa kutokea.

Akitoa taarifa ya uandaaji wa mpango huo katika Wilaya hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw. Ezekiel Magehema alisema kutokana na tathimini ya kubaini vihatarishi vya vya maafa na uwezekano wa kuathirika na uwezo wa kukabili maafa katika wilaya iliyofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa ufadhili wa UNICEF ambapo jumla ya kaya 144 zilishiriki katika utafiti huo na wataalamu kutoka Idara mbalimbali za halmashsauri zilihojiwa kupata uelewa juu ya masuala ya maafa.

Aidha, tathimini ilibaini kuwa Kyela inakabiliwa na majanga makuu matatu ikiwemo mafuriko, majanga ya wanyama wakali na waharibifu pamoja na magonjwa ya mlipuko ambapo ilipekelea kuwepo kwa mpango huu.

“Jumla ya Kata 13 zilibainika kuathiriwa na majanga aina ya mafuriko na baadhi ya miundombinu ya kutolea huduma muhimu za kijamii zipo katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko ambapo zinanapelekea kuathiriwa kwa makundi maalum ikwemo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu,”alisisitiza

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya akihutubia wakati wa kikao cha Kuthibitisha na Kupitisha Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza Vihatarishi vya Maafa katika Wilaya ya Kyela Jijini Mbeya tarehe 25 Mei, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela Mhe. SACP Ismail Mlawa akitoa salamu za Wilaya yake wakati wa kikao cha Kuthibitisha na Kupitisha Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza Vihatarishi vya Maafa



Mkuu wa Wilaya ya Kyela Mhe. SACP Ismail Mlawa (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw. Ezekiel Magehema wakiweka saini katika Nyaraka ya Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza Vihatarishi vya Maafa katika Wilaya hiyo ikiwa ni ishara ya kuridhia na  kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mapango huo.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wakifuatilia.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya (Mwenye tai waliokaa) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kyela Mhe. SACP Ismail Mlawa (kulia kwake) na wajumbe wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua kikao hicho.