Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dodoma
MOJA ya mikakati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyojiwekea ya kuimarisha uadilifu katika utendaji kazi wake ni pamoja na uundaji wa kamati za kudhibiti uadilifu ndani ya mamlaka hiyo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali hapa nchini.
o
Hayo yamesemwa na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Msafiri Mbibo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa makatibu wa kamati hizo za kudhibiti uadilifu ndani ya mamlaka hiyo.
“Kama mnavyofahamu Tanzania imeingia katika uchumi wa kati, hivyo kama tunataka kuhakikisha tunadumu katika uchumi huu wa kati au tunaenda zaidi ya tulipo ni lazima jamii yetu iendeshe mambo yake kwa uadilifu mkubwa na taasisi kama TRA ambayo ni nyeti ni lazima tuboreshe eneo la maadili ili kuwa na nidhamu katika suala zima la ukusanyaji kodi,” amesisitiza Mbibo.
Amesema kuwa,TRA ina jukumu la kukusanya kodi kwa niaba ya Serikali na jukumu hilo haliwezi kutekelezwa kwa ufanisi bila kuwa na watumishi waadilifu ikiwa ni pamoja na uwepo wa mfumo imara unaosimamia uadilifu.
“Jukumu la TRA ni kukusanya kodi ambazo zinahusisha fedha, na sisi sote tunajua kwamba, fedha zina ushawishi mkubwa lakini hata wateja wetu ambao ni walipakodi wanaweza kuwashawishi watumishi wetu ili wasilipe kodi kulingana na uhalisia wa kodi zao na hivyo kupunguza fedha za Serikali. Tukumbuke kwamba, tukiimarisha uadilifu tutaongeza mwamko wa wananchi kulipa kodi kwa hiari,” amesema.
Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Ndani ya mamlaka hiyo, Amiram Lekey alisema kuwa, lengo la mkakati huo ni kupunguza rushwa kwa kutumia mbinu za kuzuia na kupambana na rushwa hasa katika sekta zenye vishawishi vya rushwa ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania.
“TRA imeunda kamati hizi katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya taasisi, mkoa, wilaya na vituo vya kodi ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Mpango mkakati wa mamlaka wa kupambana na rushwa wa awamu ya tano ulioanza mwaka 2017 hadi 2022.
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo makatibu wa kamati hizo za kudhibiti uadilifu ndani ya mamlaka hiyo, yanashirikisha makatibu wa kamati za kudhibiti uadilifu za idara zilizopo ndani ya TRA, Chuo cha Kodi (ITA), TRA Zanzibar, vituo vya kodi na mikoa yote hapa nchini.
Baada ya ufunguzi huo, Naibu Kamishna Mkuu huyo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania alifanya ziara ya kikazi katika ofisi za TRA zilizopo Wilaya ya Chamwino na Kongwa hapa jijini Dodoma ambapo amewataka watumishi wa ofisi hizo kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanavuka malengo ya ukusanyaji kodi waliyopangiwa katika wilaya zao.
“Katika utekelezaji wa majukumu yenu hakikisheni mnatenda jambo jema hata kama kuna changamoto mnazokumbana nazo bila kusahau kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na heshima kwa watu wote,” amesema Mbibo.
Mbibo amepata fursa ya kumsalimia Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Suleiman Serera ofisini kwake ambapo pamoja na mambo mengine, walipata fursa ya kujadiliana mipango mbalimbali ya kuongeza mapato wilayani humo.
Naibu Kamishna Mkuu huyo anaendelea na ziara yake katika maeneo mbalimbali mkoani hapa ikiwa na dhumuni la kutembelea ofisi za TRA na kuzungumza na watumishi kwa ajili ya kuwapa hamasa ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika majukumu yao ya kila siku.
More Stories
Kishindo Mkutano wa Nishati leo, kesho Dar
Puma Energy Tanzania yampongeza Rais Samia kwa mazingira mazuri ya uwekezaji, yang’ara tuzo za TRA
CHAMUITA wamtunuku Tuzo Msama