Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
NAHODHA mkuu na beki tegemeo wa klabu ya Yanga, Lamine Moro amepanga kufanya makubwa zaidi kwa timu yake msimu huu huku akitaka kuweka rekodi itakayoacha alama kwa misimu kadhaa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL).
Beki huyo ambaye hadi sasa ameshapachika wavuni mabao manne katika mechi muhimu dhidi ya Mbeya City na Mtibwa Sugar ambazo zote walipata ushindi wa goli 1-0 huku bao lingine akifunga katika mchezo dhidi ya Mwadui ambao timu hiyo ilipata ushindi mnono wa goli 5-0, anahaha kuvunja rekodi yake aliyoiweka akiwa anaitumikia klabu ya Buildcon FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Zambia ambapo alifanikiwa kufunga goli saba.
Hadi sasa beki huyo anafungana kwa idadi ya magoli na mshambuliaji Michael Sarpong ambaye pia ana goli nne alizofunga katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons, Biashara United, Simba pamoja na katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.
Beki huyo ambaye ameonesha kiwango bora msimu huu ameweka wazi kuwa, atahakikisha anafunga goli kila atakapopata nafasi kwali licha ya matamanio makubwa ya kuipa ushindi timu yake lakini pia anahitaji kuweka rekodi bora msimu hu una kuacha alama ndani ya VPL.
“Nimekuwa na kawaida ya kufunga kila ninapopata nafasi, kwa sasa tunapotafuta ushindi ni muhimu kupambana na kuhakikisha timu inashinda lakini pia ninachokihitaji ni kuweka rekodi bora itakayofanya nikumbukwe hata kama nitatimkia katika timu nyingine nje ya Tanzania, ” amesema Lamine kupitia mtandao rasmi wa klabu ya Yanga.
Itakumbukwa kuwa, kiwango, nidhamu, na hamasa aliyoionesha nyota huyo ilimfanya kocha Kaze kumpa cheo cha unahodha akiamini kuwa ni kiongozi bora kwa wenzake ndani nan je ya uwanja.
Lakini pia baada ya mechi zao za hivi karibuni, kocha mkuu wa Yanga, Cedric Kaze ameonesha kuvutiwa zaidi na kazi ya beki huyo huku akiweka wazi kuwa, toka awali alijuwa kuwa Lamine ni mchezaji mzuri hasa katika mipira iliyokufa na angekuwa na msaada mkubwa kwao jambo linaloongeza morali ya upambanaji kwa timu.
Hadi katika mechi nyingi anazoanza, amekuwa kiunganishi mzuri hasa katika kuimarisha safu ya ulinzi na kumlinda kipa Metacha Mnata katika eneo lake kwani kwa kushirikiana na wenzake wamekuwa wakifanya kazi ya ziada pia kwa kuwasaidia walinzi wa pembeni.
Katika mechi 16 ambazo wamezicheza Yanga hadi sasa, wameruhusu goli sita pekee lakini wakifanikiwa kupachika wavuni goli 25 baada ya hivi karibuni kuanza kupata ushindi wa goli nyingi na kupunguza presha aliyokuwa nayo kocha Kaze.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania