Judith Ferdinand
Kisiwa cha Bezi kilichopo ndani ya Ziwa Victoria,wilayani Ilemela mkoani Mwanza,ni miongoni mwa maeneo ambayo huduma za afya zimekuwa kama ndoto kwa wakazi wake.Na hapa maisha ya mama na mtoto yamekuwa hatarini si kwa sababu ya ugonjwa pekee bali ukosefu wa huduma za afya kisiwani humo.
Kadhalika umbali wa huduma za afya ambazo hulazimika kuzifuata ng’ambo, ukosefu wa vituo vya afya, usafiri wa dharura na uhaba wa wataalamu wa afya.
Ambapo wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakishuhidia vifo vya mama na mtoto vitokananvyo na uzazi,hali inayowatia hofu wakina mama pindi wanapopata ujauzito kwani tumaini la kuwa hai linapotea.

Natumia takribani saa 4,kutoka katikati ya jiji la Mwanza nikitumia usafiri wa daladala,pikipiki na kivuko cha Mv.Ilemela ambacho kinatia nanga majira ya saa tano na dakika 40 asubuhi kwenye gati la Bezi.Nabisha hodi ndani ya kisiwa cha Bezi na mwenyeji wangu hapa ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kisiwani hapo James John,anaye nipokea na kunikutanisha na baba aliyepoteza mke na mtoto tumboni wakati wa kujifungua.
Huyu si mwingine ni Hassan Nagabona baba wa watoto watano,mkazi wa Kisiwa cha Bezi,baada ya kutambulishwa kwake ananza kwa “Ninaamini kama zahanati ingekuwepo au kama tungepata boti ya mwendo kasi, mke wangu na mtoto wangekuwa hai mpaka sasa,”.
Hali ilivyokuwa wakati wa ujauzito
Nagabona anasema kuwa kipindi cha ujauzito mke wake huyo ambaye sasa ni marehemu hakuwai kupata changamoto yoyote licha ya kwamba hakutaka kuhudhuria kliniki.
“Nilikuwa namlazimisha kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito lakini alikataa,kwa sababu vituo vya kutolea huduma vipo mbali,mimba hiyo ilikuwa nzao ya sita na hutukuwahi kutumia njia ya uzazi wa mpango kwani naamini tupo duniani ili kuzaa na kuongeza na kifo ni mipango ya Mungu,”anasema Nagabona.

Nini kilisababisha kifo cha mke wake
Nagabona anasimulia kuwa usiku wa Desemba 13, 2019,ni siku ambayo ataisahau maishani mwake,baada ya kumpoteza mke wake na mtoto aliyekuwa tumboni.
Mzazi huyo aliyekuwa katika harakati za kuleta maisha mapya duniani, lakini akajikuta akikabiliana na kifo.
“Usiku wa saa nne,mke wangu alianza kuumwa uchungu,ikabidi niende kutafuta usafiri wa mtumbwi kwa ajili ya kumuwahisha kituo cha afya Sangabuye,lakini haikuwa bahati kwani usiku huo nilikuta mitumbwi yote imeenda doria,”anasimulia kwa huzuni Nagabona.
Nagabona anasema,baada ya kukosa mitumbwi hakukata tamaa aliendelea na jitihada za kutafuta msaada kwa ajili ya kuokoa uhai wa mke wake na mtoto aliopo tumboni kwa kukimbilia kwa wakunga wa jadi.
“Lakini wote walinyanyua mikono kwa hofu, wakikataa kutoa msaada. Wakati narudi nyumbani bila msaada wowote,nilimkuta mke wangu ameishafariki akiwa bado hajajifungua(mtoto akiwa tumboni),” anasema Nagabona.
Kauli hii ya kukosa msaada inaungwa mkono na Basilimaki Masatu, mkunga wa jadi ambaye alianza kazi hiyo mwaka 2008 baada ya kurithi maarifa kutoka kwa shangazi yake aliyekuwa mganga wa jadi, anasimulia kuwa amekuwa akiwasaidia wanawake kujifungua kwa miaka mingi hadi pale alipoacha baada ya tukio la kifo kilichomvunja moyo.
“Nilikuwa natoa msaada bila matatizo. Wengi walinijua na waliponifikia nimesaidia wajawazito wengi sikumbuki idadi. Lakini kuna siku nilikataa kwenda kumsaidia mama mmoja kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Nasikitika kesho yake nikasikia mama huyo amefariki pamoja na mtoto akiwa tumboni,”anasema Basilimaki na kuongeza:
“Tangu siku hiyo wakasema hawataki mtu azalishe mtu humu,hatutaki mkunga humu inatakiwa mtu akiwa mjamzito wakati wa kujifungua lazima aende hospitali.Baada ya katazo na mimi naogopa mtua akinufaua na mwambia aende hospitali kama ikishindikana kujifungua ishindikane akiwa huko siyo hapa kwangu,”.
Basilimaki anasema,tangu ameanza kusaidia wajawazito wa kisiwa cha Bezi na visiwa jirani hajawai kuzalisha mama akafariki au mtoto,hivyo aliweza kuokoa maisha ya mama na mtoto.
“Sijisikii vizuri bali najisikia vibaya kuona wanawake na watoto wachanga wanapoteza maisha kutokana na kukosa huduma wakati wa kujifungua lakini nitafanyaje wakati wameisha piga marufuku.Tangu nimeacha huduma nimeisha shuhudia vifo takribani vitano kikiwemo cha aliyeshindwa kumsaidia wakati anaumwa,kingine nilikuwa nimesfiri,kingine mama alijifungulia gesti akapoteza maisha,”.
Mmoja wa wakazi wa Kisiwa cha Bezi,Esther Warioba,anasema,wanawake kisiwani humo huishi kwa hofu mara wanapojigundua kuwa na ujauzito kwani wengi wamepoteza maisha,ambapo kati ya mwaka juzi na mwaka jana,kuna mama alipoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma na msaada wakati wa kujifungua.
“Wanawake tulijitahidi huku na huku kumnusuru yeye na mtoto wake lakini jitihada zetu hazikuzaa matunda mama yule na mtoto walipoteza maisha,kitendo kilichoacha simanzi kwenye mioyo yetu.Uongozi wa mtaa ukaazimia kwamba mama anapokuwa mjamzito akifikisha miezi nane arudi kwao lakini haikuwzekana au akapange karibu na kituo cha afya akisha jifungua atarejea kisiwani humo,”anasema Esther na kuongeza:
“Kwani hatujui uchungu utauma saa ngapi kwani asilimia kubwa hatutumii njia ya uzazi wa mpango hivyo hatujui mimba ilipatikana linin a ikizingatiwa wanawake wengi wa kisiwani hapa hawahudhurii kliniki kwa sababu zipo mbali,hivyo unashtukia tayari uchungu umeanza kuuma na mara nyingi unakuwa ni usiku na kupata usafiri muda huo ni changamoto,”.
Esther anasema,tumaini la wajawazito kisiwani hapo ni kutoka kwa wakunga wa jadi akiwemo anaishi eneo la mperani ambao wamekuwa wakiwasaidia wajawazito lakini wengine wanawashinda wanapoteza maisha.

Mbinu wanazotumia wakunga kuokoa maisha ya wajawazito
Wakunga wa jadi ni tumaini la wajawazito waliopo kisiwani Bezi licha ya kutosomea wala ya kuwa na taaluma hiyo,lakini hapa Basilimaki Masatu,anaeleza mbinu wanazotumia kuzalisha na kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Anasema,mtu akija anaumwa uchungu kwanza ananza kwa kumuomba Mungu kisha atamkalisha chini na kumuelekeza kusubiri wakati huo yeye akivaa mpira mkononi kisha kumpelekea mkono kutokana na uzoefu atajua kama mtoto ameisha geuka au yupo karibu kuzaliwa.
Kisha atamuelekeza kusubiria na ukifika muda atamwambia kusukuma na baada ya hapo atafanikiwa kuzaa hivyo kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha mama na mtoto anawasafisha na kuwapa huduma muhimu.
“Wakati nawahudumia sijawahi kuhisi hatari yoyote ya mama na mtoto kupoteza maisha au damu nyingi,jambo hili linanifanya ni mshukuru Mungu maana hakuna kifo kilichowahi kutokea,”anasema Basilimaki na kuongeza:
“Mungu ni muweza wa yote ndio aliyenisaidia kuokoa uhai wa mama na mtoto,unapoenda kumsaidia mtu inabidi usali,nilikuwa namwambia Mungu tendo ambalo limekuja mbele yangu naomba unisaidie,huyu mtu atoke akiwa salama,wewe ndio ulimpandisha kwenye mti naomba umtereshe kweli Mungu anasikia maombi,”
Kwa upande wake Pendo Waryoba, anasema kuwa changamoto kubwa kisiwani hapo ni ukosefu wa kituo cha afya na usafiri wa uhakika,ili kufika kituo cha afya cha Sangabuye, ni lazima kutumia mtumbwi unaotumia zaidi ya saa tano.
Pendo anasema,mtumbwi si usafiri wa dharura ni hatari, na aghali kwani wanalazimika kukodi kwa shilingi 100,000,ambayo si kila mtu anaweza kumudu gharama hiyo.
“Mara nyingi, wajawazito hupata uchungu usiku wakati ambao hakuna usafiri wowote unaopatikana kwani usafiri wa kivuko cha Mv.Ilemela ufanya kazi kwa muda tu asubuhi na jioni na siyo usiku.Ukichelewa kupata mtumbwi, unakuta mama amezidiwa na kupoteza maisha yeye na mtoto,”anasema Pendo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kisiwa cha Bezi,James John,ana unga mkono kauli za wananchi wake juu ya ukosefu wa huduma za afya kituoni humo hali inayochochea vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi.
“Mjamzito akiumwa uchungu hata saa saba usiku,lazima Mwenyekiti au mjumbe wa Serikali za Mitaa agongewe hodi ili angalau amtafutie usafiri wa kumfikisha kwenye huduma.Mpaka utafute injini,mtumbwi unaweza kutumia takribani saa mbili,mjamzito afuatwe na kufikishwa kwenye mtubwi na kufikishwa kwenye kituo cha afya Sangabuye unaweza kutumia takribani saa sita hali ambayo ni hatari kwa uhai wa mama na mtoto,”anasema John.
“Tumeisha wahi kupitia majanga ya mama kupoteza maisha pamoja na mtoto wakati wa kujifungua au akiumwa uchungu kwa kukosa huduma ya uzazi.Lakini pia juzi juzi tu hapa mradi wa ujenzi wa zahanati ukiwa unaendelea kuna mama mjamzito alinusurika kupoteza maisha lakini mtoto alifariki,”.
John,anasema,hatari ni kubwa kisiwani hapo kwa uhai wa mama na mtoto,ambapo anasema kuna vifo vitatu vya hivi karibuni kikiwemo cha mwanaume mmoja alipoteza mke na mtoto wakati wa kujifungua na walishindwa kufanya lolote pia yupo mama aliyenusurika huku mtoto akifariki.
“Mara nyingi mama mmoja ndio anawasaidia wajawazito kujifungua kisiwani hapo, lakini bado jitihada zake hazitoshi kwani kila mwaka wamekuwa wakipoteza mama mjamzito pamoja na mtoto takribani mmoja.Nakumbuka kama miaka mitatu iliopita tulipoteza wamama watatu kutokana na uzazi,”anasema John.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Dkt.Maria Kapinga,anasema,Kisiwa cha Bezi hakina zahanati na wananchi wake wanategemea huduma kutoka kwa watoa huduma za afya wa kujitolea au kusafiri mpaka Sangabuye au Kayenze kwa ajili ya kupata huduma hizo zikiwemo za uzazi.
Dkt,Kapinga anasema,changamoto kuu katika utoaji huduma kisiwani humo ni ukosefu wa kituo cha afya cha kudumu,wajawazito kujifungulia nyumbani bila msaada wa kitaalamu.
Pia umbali mrefu uliopo hadi kwenye vituo vya afya vya karibu,kwani wanahitaji usafiri wa majini ambao sio wa uhakika,uhaba wa wahudumu wa afya waliobobea kwenye huduma ya mama na mtoto pamoja na vifaa tiba.
“Idadi ya vifo vya uzazi vilivyoripotiwa katika kisiwa cha Bezi kwa kipindi cha mwaka 2020-2025,mwaka 2020 kifo 0,2021 kifo 1,2022 kifo 0,2023 kifo 1 kilichotokea kwenye jamii(community death),2024 kifo 0 na 2025 kifo 0,”.
Hata hivyo kwa mujibu wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma Aprili 9,mwaka huu ,alisema kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 Februari 2025.
Nini kifanyike kuokoa maisha ya mama na mtoto kisiwani Bezi
Hassani Nagabona,anasema,endapo kungekuwa na kituo cha afya au boti ya mwendo kasi(ambulance boti),kwa ajili ya kuwakimbiza katika kituo cha afya Sangabuye au Kayenze mke na mtoto wasingepoteza maisha.
“Ombi langu tufanyiwe msaada wa haraka za zahanati ikamilike na wahudumu wa afya wawepo wa kutosha pamoja na vifaa tiba kwani kwa sasa wanawategemea wenye maduka ya dawa na wakunga wakujitolea ambao hawana taaluma,”.
Kwa upande wa Novatus Cheusi, mmoja wa wakazi wa Kisiwa cha Bezi, anasema,endapo wangepata boti ya mwendo kasi au ambulance ya majini,wangeokoa maisha ya wengi.Mama akianza uchungu, wangeweza kumfikisha haraka hospitalini badala ya kutumia saa sita kwa mtumbwi wangetumia dakika 15 tu.
“Katika maisha yangu kisiwani hapa nimewahi kushuhudia mama mjamzito akipoteza maisha eneo la mperani ambaye alipata changamoto ya uzazi na kukosa huduma.Kama mwananchi sikujisikia vizuri kuona mwenzangu anapoteza maisha na mtoto tumboni kwa sababu ya kukosa huduma ya haraka ya kujifungua,”.
Hata hivyo Basilimaki Masatu amabaye ni mkungawa jadi kisiwani humo,anasema kwa sasa ili kukomesha vifo hivyo iwawezeshe wakunga wa jadi kwa kuwapatia mafunzo waweze kushirikiana na wataalamu wa afya kuokoa maisha ya mama na mtoto kisiwani humo hadi wakati zahanati itakapoanza kutoa huduma.

–



More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama