January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NACONGO yatarajia kupata viongozi wapya Julai

Na Penina Malundo,Timesmajira,online

BARAZA la Taifa la Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACONGO), linatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu, unaotarajiwa kufanyika Julai 8, mwaka huu na kutoa wito kwa makundi mbalimbali hususani wanawake kujitokeza katika chaguzi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Dar es Salaam Mwenyekiti wa NACONGO, Wakili Flaviana Charles amesema uchaguzi huo umetangazwa baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima kuunda Kamati ya mpito ya watu 10 kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kusimamia.

Amesema fomu zitaanza kuchukuliwa rasmi Juni 21 mwaka huu katika Ofisa za Maendeleo ya Jamii Wilaya katika wilaya 139 nchini na mwisho wa kurudisha fomu ni Juni 24 mwaka huu.

Wakili Charles amesema Juni 25, mwaka huu uchakataji wa fomu za wagombea wa baraza katika ofisi hizo na kazi hiyo itafanywa na Kamati ya Taifa ya Uchaguzi.

“Ifikapo Juni 26 mwaka huu, uchaguzi katika ngazi za wilaya utaanza huku Juni 28 uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza katika ngazi ya mkoa ambapo Julai 5 hadi 8 mwaka huu, utakuwa ni uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa baraza, kamati ndogo na wajumbe wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali,” amesema.

Amesema Julai 9 hadi 10 mwaka huu, utakuwa uapisho na makabidhiano ya nyaraka na ofisi na kuanza kazi kwa watumishi hao.

Wakili Flaviana alihimiza wenye sifa, kuwania nafasi hizo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na makundi maalumu yakiwamo ya watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Foundation for Civil Society, Francis Kiwanga amesema baraza hilo ni muhimu katika taasisi hususan kwenye kazi zote hizo za kusimamia masuala ya uchaguzi.

“Rai yetu sisi kwa Asasi zote za Kiraia, kila mtu aweze kushiriki na watu wachukue fomu na kugombea nafasi hizi zilizotangazwa,” amesema na kuongeza;

“Ushiriki wa wanawake katika uchaguzi huu ni muhimu sana, hivyo tunatoa rai yetu watu wajitokeze ili baraza liwe shirikishi zaidi na wadau wenye upana”.