March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nabii Mpanji afanya ibada maalum kuombea uchaguzi mkuu

Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya

KIONGOZI wa Kanisa la GMCL, Nabii David Mpanji, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025 bila hofu, akisisitiza kuwa uchaguzi si sababu ya kugombana bali ni fursa ya kuchagua viongozi kwa amani.

Akizungumza Oktoba 26, 2025 wakati wa ibada maalum ya kuombea uchaguzi mkuu iliyofanyika katika Kanisa la GMCL, eneo la Ilomba jijini Mbeya, Nabii Mpanji amesema. Tanzania imekuwa mfano wa amani barani Afrika na hivyo wananchi hawapaswi kuruhusu vurugu kuharibu zawadi hiyo kutoka kwa Mungu.

“Tumeona katika baadhi ya nchi watu wamepoteza mali, watoto na familia kutokana na uchaguzi. Nawaomba Watanzania tujitokeze kupiga kura kwa amani, kwani taifa hili ni kama zawadi kutoka kwa Mungu tumekuwa kimbilio kwa mataifa mengine,” amesema Nabii Mpanji.

Aidha, amekumbusha wanasiasa na wananchi kwa ujumla kuwa maisha yataendelea baada ya Oktoba 29, hivyo ni busara kila mtu kuhakikisha anabaki salama na kuendelea na majukumu ya kujenga taifa.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakitoa vitisho kupitia mitandao ya kijamii, lakini tuamini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Mimi binafsi baada ya kupiga kura nitarejea kanisani kuendelea na maombi, maana wajibu wa viongozi wa dini ni kuhakikisha amani inaendelea kuwepo,” amesisitiza.

Nabii Mpanji ameongeza kuwa kuwepo kwa amani ni nguzo ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi, hivyo kila mmoja anatakiwa kuwa mlinzi wa mwenzake na kushirikiana na serikali katika kudumisha utulivu wa nchi.

Kwa upande wao, waumini wa kanisa hilo waliungana na kiongozi wao katika wito huo wa amani.

Justa Mahondi, mmoja wa waumini wa GMCL, amewataka Watanzania wajitokeze kupiga kura kwa amani bila kuchochea vurugu.

“Tuchague viongozi tunaowaamini, lakini pia tuilinde amani tuliyonayo kwani tukiharibu amani, sisi na familia zetu ndio tutakaoumia,” amesema.

Naye Ezekiel Kabelege amesema amani iliyorithiwa kutoka kwa Baba wa Taifa haipaswi kuchezewa, akisisitiza jukumu la kila raia kuitunza na kutojikuta katika majaribu ya kuchochewa kufanya vurugu.

“Viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele kuhubiri amani, hivyo nasi ni wajibu wetu kusikiliza na kutenda yale wanayotuasa,” amesema Kabelege.