Na Mwandishi Wetu, Mwanza
HATIMAYE viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA) wamekutana na viongozi wa klabu ya Mbao FC ya jijini humo kujadili mikakati itakayosaidia timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kusalia ndani ya ligi hiyo msimu ujao.
MZFA na Mbao wamekutana baada ya mwezi uliopita chama hicho kutaka timu zote za mpira wa miguu zinazoshiriki Ligi mbalimbali mkoani humo kujifanyia tathimini katika ushiriki wao kwenye Ligi hizo ili kujinusuru na janga la kushuka daraja.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa MZFA, Leonard Malongo, aliliambia Majira kuwa, baadhi ya klabu ikiwemo Mbao inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) hazikuwa katika nafasi nzuri hivyo ni muhimu kufanya tathimini kwa muda huu wakati Ligi zikiwa zimesimama kutokana na hofu ya kusambaa kwa ugonjwa wa Corona.
Msimu huu haujawa mzuri kwa Mbao kwani hadi Ligi inasimama, timu hiyo ilikuwa inashika nafasi ya 19 wakiwa na pointi 23 baada ya kushinda mechi tano, sare nane na kupoteza mechi 16 ukilinganisha na ule uliopita mbao pia walinusurika kushika Daraja baada ya kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya 16 baada ya kujikusanyia pointi 45.
Kwa sasa timu hiyo ina kazi kubwa ya kuhakikisha endapo hali itakuwa shwari kuruhusu mechi zilizosalia kuchezwa ili kumaliza msimu kuhakikisha wanashinda mechi zao zote tisa zilisalia ili kumaliza Ligi wakiwa na pointi 50.
Akizungumza na Majira kuhusu mikakati waliyoweka kwenye kikao hicho, Malongo amesema kuwa, jambo la kwanza walilokubaliana ni kuhakikisha timu hiyo inasalia na kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Amesema, wanaelewa kwa sasa klabu hiyo inakabiliwa na matatizo mengi lakini wao kama Chama ni jukumu lao kuita wadau mbalimbali ili kuangalia ni namna gani wanaweza kuisaidia timu hiyo kubaki Ligi Kuu.
Moja ya ajenda zitakazojadiliwa kwenye kikao na wadau wa soka Jijini hapa ni kuiwezesha kiasi cha fedha timu hiyo ambazo zitatumika kwa ajili ya shughuli zote muhimu za kiutendaji.
Malongo amesema kuwa, kwa mara kadhaa klabu imekuwa ikikumbana na matatizo lukuki katika mechi zao za ugenini hivyo anaami ni kuwa endapo Ligi itaendelea basi wadau hao wa soka wataisaidia timu hiyo katika safari zake ili kuweza kupata matokeo mazuri yatakayowaondoa kwenye hatari waliyopo sasa.
“Klabu ya Mbao imekuwa ikikumbana na changamoto nyingi hivyo katika kikao tulichokaa na viongozi wao tumeweka mikakati kadhaa ikiwemo kuhakikisha timu hii inasalia Ligi Kuu pamoja na kuwataka wadau kuiwezesha fedha ambazo zitasaidia kuisapoti timu hata katika safari zake za mechi za ugenini,” amesema Malongo.
Pia wamekubaliana ni muhimu kuwalipa wachezaji wa klabu hiyo stahiki zao ikiwemo kuwaongeza na motisha ambayo itawapa nguvu ya kupambana zaidi ili kuibakiza timu Ligi Kuu.
Amesema, endapo mikakati hiyo itatekelezwa ipasavyo na kila kitu kwenda kama kilivyopangwa basi hakuna kitakachoizuaia timu hiyo kubali Ligi Kuu kwani wanaeleza uwezo wa wachezaji wao katika kuipambania klabu hiyo kutoshuka Daraja,” alisema kiongozi huyo.
Kwa sasa amewataka wachezaji wa klabu hiyo kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na Corona huku wakiendelea kujifua binafsi ili pale serikali itakaporuhusu michezo kuendelea wawe na hari ya kuapambana na kutimiza mikakati waliyoiweka.
Hata hivyo kiongozi huyo ametaka Vyama vyote vya soka vya Wilaya kuhakikisha vinasimamia ipasavyo agizo la Serikali la kutoruhusu mchezo wa aina aina yoyote kwani ikibainika kuna yeyote anayekaidi agizo hilo basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Kwa sasa wakazi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla tunatakiwa kuendelea kuwa watulifu na kufuata maagizo ya serikali huku tukiendelea kuomba janga hili liishe haraka na kila kitu kiendelee kama kilivyokuwa awali kabla ya mlipuko wa ugonjwa huu, ” amesema Malongo.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM