September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mzee wa Masaptasapta ashinda kesi dhidi ya Azam media Group

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mpishi maarufu Nchini Master Chef Fred Uisso, alimaarufu kama Mzee wa Maspatasapta, leo tarehe 16 August, 2024 ameshinda kesi dhidi ya AZAM MEDIA GROUP na Wenzake watatu baada ya Azam kumtangaza mpishi huyo kupitia channel yake ya Sinema Zetu kipindi kinachorushwa na Azam TV.

Matangazo hayo yaliyorushwa kwa zaidi ya week mbili katika kipindi cha mwezi August, 2023 yalionesha kuwa Mpishi maarufu huyo atahudhuria katika Tamasha la Wapi Muziki na Misosi Festival, 2023 lililoandaliwa na EX-Nihio Ltd kampuni inayomilikuwa na Paul Mashauri. Mpishi huyo maarufu anayemiliki mgahawa wake wa vyakula vya asili uliopo Kijitonyama, alimfikisha Azam Media Group, Ex-Nihio pamoja na Paul Mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai kwamba wadaiwa hao wameupotosha umma kwa kuuhadaa kuwa atashiriki katika Tamasha hilo suala ambalo si la kweli.

Katika Mahakama ya Kisutu, Master Chef Fred Uisso ameiomba Mahakama kuwataka wadaiwa kumlipa Fidia ya Madhara ya Jumla kwa kuwa matangazo yake yaliuhadaa umma suala lililopelekea kukosa biashara katika Mgahawa wake.

Hivyo Mahakama baada ya kusikiliza shauri hilo kwa takribani mwaka mmoja, jana limefikia maamuzi kwa kuwataka wadai kumlipa fidia ya madhara ya Jumla kiasi cha shilingi Milioni 100 pamoja na gharama za uendeshaji wa shauri hilo.

Itakumbuka pia, tarehe 25, August, 2023 Mahakama hii ya Kisutu ilizuia kutofanyika kwa Tamasha hilo baada ya Master Chef Fred Uisso kufungua shauri la kuzuia kufanyika kwa Tamasha hilo la Wapi Muziki na Misosi, 2023 Festival lililopagwa kufanyika katika viwanja vya Posta Kijitonyama.

Akizungumza kwa kifupi, Wakili Msomi Ferdinand Makore aliyemuwakilisha Mdai, mara baada ya kutoka Mahakamani, amesema Haya maamuzi ya leo yanatoa fundisho kwa watu wote wanaopenda kutumia majina ya watu kwa ajili ya umaarufu wa majina hayo, kwa kuwaamiisha umma kuwa Fulani Atakuwepo, suala ambalo mara nyingi huwa ni uongo na hufanya hivyo kwa lengo la kupata watu wengi hivyo Mahakama imetamka wazi kuwa neno Fulani Atakuwepo bila kupata ridhaa yake kabla ya Tangazo husika ni kosa kisheria. Ameongeza Wakili Makore.