December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mzee wa Bwax afunika ‘Kitaa food Fest’ Mbagala

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MSANII wa muziki wa singeli, Mohammed Rashid maarufu Mzee wa ‘Bwax’, mwishoni mwa wiki alifanya onyesho la aina yake katika Tamasha la chakula la Coca-Cola maarufu ‘Kitaa Food Fest’ Mbagala, jijini Dar es Salaam.

Msanii huyo aliporomosha burudani ya aina yake iliyoibua shangwe kubwa kwa mashabiki waliohudhuria Tamasha hilo. Hata hivyo Mzee wa Bwax aliimba nyimbo zake mbalimbali zikiwemo ‘Kafubaa’, ‘Kisimu, Changu’, ‘Kikao’, ‘Nikilewa’, ‘Mapenzi’, ‘Akutake Nani’’ na ‘Nimeokoka’.

Katika Tamasha hilo, ambalo lilikua kivutio kikubwa kwa wakazi wa Mbagala, lilidhihirisha umaarufu wa msanii huyo na uwezo wake wa kuwasisimua wapenzi wa muziki wa Singeli.

Burudani ya Mzee wa Bwax ilikuwa ni sehemu ya matukio mbalimbali yaliyopangwa katika tamasha hilo la Coca-Cola Kitaaa Food Fest, ambalo liliwaleta pamoja wakazi wa Mbagala kwa lengo la kutoa fursa ya kufurahia chakula, na burudani ya muziki.

Aidha, katika tamasha hilo, wafanyabiashara wa Chakula maarufu ‘Mama Lishe’ walipata nafasi ya kuonyesha ujuzi wao wa kupika vyakula mbalimbali vya asili huku wakipokea mwitikio mzuri kutoka kwa washiriki.

Akizungumza baada ya onyesho hilo, Mzee wa Bwax alieleza furaha yake kwa jinsi wakazi wa Mbagala walivyojitokeza kwa wingi na kushiriki burudani.

“Nimefurahi sana kuwa sehemu ya tukio hili, Coca-Cola wamefanya jambo kubwa kwa kuwaleta watu pamoja. Ni muhimu kwa matukio kama haya ambayo yanafanya jamii kuungana na kufarahi kwa pamoja,” alisema msanii huyo.