Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto
Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Yusuph Makamba, amesema Mradi wa Maji Kijiji cha Mahezangulu hautakuwa na faida kama wananchi wataendelea kuharibu chanzo cha maji.
Makamba alisema kwa miaka 84 aliyoishi hapa duniani, maji ya bomba yalikuwa hayajafika kijijini kwake, hivyo kwa Serikali kufikisha maji hayo ni jambo kubwa ambalo wamanchi wa kijiji hicho wanatakiwa kujivunia kwa kupata mradi huo.
Aliyasema hayo Juni 27, 2022 mbele ya waandishi wa habari ambao walifika Kijiji cha Mahezangulu kilichopo Kata ya Mahezangulu, Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, ili kuona hali ya upatikanaji wa maji, na kuzungumza na wananchi kujua wamepokea vipi mradi huo, na wakati huo kuona changamoto za mradi huo.
“Mwenyekiti wa Kijiji na watendaji wako, mnatakiwa kuwaondoa wakulima wanaolima pembeni ya chanzo cha maji. Lakini pia mnatakiwa kutoa elimu kwao ili kuondoka eneo hilo na kutorudi tena kulima kwenye chanzo hicho. Kama hamtawaondoa, mradi huu wa maji hautakuwa na faida tena kwa wananchi sababu chanzo kitakuwa kimekauka” alisema Makamba.
Makamba ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijjni (RUWASA) kwa kupata maji ya bomba tangu Juni 24, 2022, baada ya maji hayo kufika nyumbani kwa mzee Makamba, Kitongoji cha Kwemchungwa, Kijiji cha Mahezangulu.
“Mimi nimezaliwa mwaka 1938, lakini maji yamefika kijijini kwangu Mahezangulu nikiwa na miaka 84. Lakini pia baba yangu alifariki akiwa na miaka 91, na babu yangu mzee Makamba alifariki akiwa na miaka 100, hao wote hawakufanikiwa kuona maji ya bomba yakiingia kwenye Kijiji cha Mahezangulu. Leo hii katika Kitongoji changu cha Kwemchungwa, tumeswali msikitini tukitumia maji ya bomba, kwani mpaka msikitini tumewekewa Kituo cha Maji (Kilula). Na sio kitongoji changu tu ninachoishi mimi ndiyo kimepata maji, bali kuna vitongoji vingine katika Kijiji cha Mahezangulu nao wamepata maji.
“Pongezi zangu zimuendee Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba na Waziri wa Maji mwanangu Jumaa Aweso. Niliwaambia wananchi nikiwa nazungumza kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, Dodoma, kuwa kwa Serikali ya Samia tutakula asali… na kweli sasa tunakula asali” alisema mzee Makamba.
Makamba pia aliishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma ya umeme na barabara, kwani miaka 50 iliyopita kuzungumzia umeme kuwa ungeweza kufika Kijiji cha Mahezangulu ilikuwa ni ndoto, lakini sasa maji, umeme na barabara vimeweza kufika kwenye kijiji hicho.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahezangulu Seif Shekidele alisema watachukua hatua za haraka kuona wananchi waliolima pembeni ya chanzo cha maji wanaondoka ili kuona mradi huo wa maji unakuwa endelevu, huku akiwataka RUWASA kuangalia vyanzo vingine vya maji vitatu ili kuongeza wigo wa upatikanaji maji kwenye kijiji hicho.
“Naahidi kufanya kazi ya kuwaondoa wananchi waliolima kwenye chanzo cha maji ili kulinda upatikanaji wa maji kwenye kijiji chetu. Ila napenda kutoa wito kwa RUWASA. Kijiji cha Mahezangulu kina vitongoji kumi, lakini maji haya yatafika kwenye vitongoji vitano tu. Hivyo, ili kuongeza upatikanaji maji kwenye vitongoji, mnatakiwa kuja kuangalia vyanzo vingine vitatu vilivyopo kwenye kijiji chetu” alisema Shekidele.
Mwananchi wa Kijiji cha Mahezangulu Fadhila Almasi alisema walikuwa na shida ya maji kwenye kijiji chao, lakini wanamshukuru Mbunge wa Jimbo la Bumbuli ambaye pia ni Waziri wa Nishati January Makamba kwa kuweza kuwapelekea maji, umeme na barabara.
Mwananchi mwingine wa kijiji hicho Abbas Ngw’andu alisema kwa Serikali kupeleka mradi wa maji kwenye kijiji hicho ni ukombozi mkubwa, kwani wananchi hasa wanawake, walikuwa wanakwenda kutafuta maji kwenye miporomoko mikali, na baadae kuanza kupanda milima, na kuwachukua zaidi ya saa sita.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga alisema Mradi wa Maji Mahezangulu ni wa sh. milioni 246.7, ukiwa na mtandao wa bomba zenye urefu wa mita 8,300, huku tanki la mradi huo likiwa na uwezo wa lita 90,000, na kuna vilula 15, huku wananchi zaidi ya 3,000 wakinufaika na mradi huo.
Sizinga alisema moja ya changamoto kubwa ya mradi huo ni baadhi ya wakulima kwenye chanzo cha maji. Wananchi wamelima hadi mita tano kutoka kwenye chanzo cha maji, wakati chanzo cha maji kinatakiwa kiachwe kati ya mita 30 hadi 60. Hivyo amewataka wananchi waweze kuondoka eneo hilo ili kulinda chanzo cha maji.
“Kipaumbele cha kwanza cha maji ni watu kunywa maji, na siyo kunyweshea mazao. Ni wajibu kwa viongozi wa vijiji kuweza kuwaondoa wanaolima kwenye chanzo cha maji. Chanzo cha maji kinatakiwa kuachwa kuanzia mita 30 na kuendelea” alisema Mhandisi Sizinga.
Waandishi wa habari walifika kwenye chanzo hicho cha maji na kukuta wananchi wamelima miwa, maharage, mahindi na magimbi hadi mita tano kutoka kwenye chanzo, jambo ambalo ni tishio kwa mradi huo. Lakini pia walikuta chanzo hicho maji yamepungua sana, ikielezwa mchana huo maji yatakuwa yamechepushwa kwenda kumwagilia mashamba ya wakulima.
More Stories
Makundi maalumu kupewa kipaumbele kupiga kura uchaguzi serikali za mitaa Lushoto
Ujenzi wa Hospitali ya rangitatu wafikia asilimia 69
Wafanyabiashara wakutana Dar,kujadili hali ya biashara