December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mzazi atoa vitenge vyenye thamani ya laki tatu kwa walimu shule anayosoma mwanae

Na Israel Mwaisaka,Timesmajiraonline, Rukwa

MMOJA ya Wazazi wa watoto wanaosoma shule ya msingi Kipundukala kata ya Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa ametoa motisha kwa Walimu wa shule hiyo kwa kuwanunulia vitenge doti 8 baada ya shule hiyo kufanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba baada ya kushika nafasi ya saba kiwilaya na tisa kimkoa.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa zawadi hiyo ya vitenge leo mwalimu mkuu wa shule hiyo Josephat Labani amewaeleza walimu wa shule hiyo kuwa mmoja wa wazazi wa Watoto wanaosoma katika shule hiyo Issa Kabuje ametoa zawadi ya vitenge kwa walimu wa shule hiyo kama Motisha kwao kutokana na maendeleo mazuri kwa shule hjiyo kuendelea kupandisha ufaulu kwa kila mwaka.

Amedai kuwa vitenge hivyo vimekabidhiwa ofisini kwake siku chache zilizopita na kuwa leo ni siku muhimu ya kukabidhiwa kila mwalimu zawadi yake ya kitenge iliyotolewa na mzazi huyo baada ya kuitambua kazi nzuri inayofanywa na walimu.

Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Angelina Mwampashi amempongeza mzazi huyo kwa hicho alichokifanya na kuwa mzazi huyo ameacha deni kwao la kuhakikisha Walimu wanaendelea kufundisha kwa moyo na kuwa kitendo hicho kilichofanywa na mzazi huyo kama kitafanywa na watu wengine kitaendelea kuwatia moyo Waalimu ya kufundisha kwa nguvu na moyo na kupata matokeo mazuri zaidi.

Amesema kuwa yeye kama kiongozi wa kamati ya shule atakachokifanya ni kujenga mshikamano uliopo kati ya wazazi na Walimu na kubwa ni kuona kiwango cha taaluma kinapanda kama walivyofanya sasa na kuwa hawapo tayari kumuona mwalimu atakayewarudisha nyuma katika mikakati waliyojiwekea ya kukuza taaluma.

Afisa elimu wa kata hiyo ya Namanyere Kasilida Milala amedai kuwa mzazi huyo ni mmoja ya watu waliofanya mabadiliko ya kifikra kwa kuwapongeza waalimu pale walipofanya vizuri na kuwataka wazazi kujenga ukaribu na walimu badala ya kutengeneza uadui kati yao na kuwa kitendo cha Issa Kabuje kutoa zawadi hiyo kimewatia nguvu walimu kuendelea kufundisha zaidi tena kwa moyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari Kabuje amedai kuwa vitenge hivyo vina thamani ya zaidi ya shilingi laki tatu na kuwa yeye ameamua kufanya hivyo baada ya kuona jitihada zinazofanywa na walimu wa shule hiyo katika kuinua taaluma.

Amefafanua kuwa Walimu wanafanya kazi kubwa kama sehemu ya Walezi wa Watoto wao na kuwa muda mwingi Watoto hao wanaishi na Walimu hivyo ipo sababu ya kuwamotisha kwa namna yoyote inayowezekana.