Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MWENYEKITI wa Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Bernadetha Ndunguru, amefungua Warsha ya Utoaji Taarifa kuhusu viwango vipya vya ubora na miongozo mbalimbali ya utoaji wa elimu ya ufundi stadi, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uelewa wa Watanzania kuhusu nafasi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi Nchini (TVET).
Akifungua warsha hiyo Novemba 18,2025 , Ndunguru ameweka wazi kuwa kazi kubwa ya Baraza na watendaji wote wa sekta ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi ni kuwaaminisha Watanzania, hususan vijana, kwamba kuchagua mwelekeo wa Elimu ya Mafunzo ya ufundi si dalili ya kushindwa au kupotea njia kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya watu.
Amesema kuwa Taifa kwa sasa linahitaji nguvu kazi yenye ujuzi wa vitendo, na hivyo wahitimu wa TVET wanapaswa kuwa sehemu muhimu katika uchumi unaotegemea ujuzi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo , serikali inawekeza kwa kiwango kikubwa katika ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika kila wilaya, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa vijana wanaohitimu kutoka kwenye vyuo hivyo hawarudi mitaani wakiwa hawana ajira au ujuzi unaowawezesha kufanya kazi kwa kujitegemea.
“Tunapowahakikishia kuwa wanapohitimu hawatakosa ajira, basi lazima tuwape stadi za kutosha na ujuzi unaowawezesha kuhimili ushindani katika soko la ajira,” amesema
Ndunguru amesisitiza kuwa dhamira ya Taifa kwa sasa ni kujenga uchumi unaoongozwa na watu wenye ujuzi katika sekta mbalimbali, hivyo vyuo vya TVET vina jukumu kubwa la kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa na umahiri unaohitajika.
Amesema kuwa iwapo wahitimu watakuwa hawaajiriki, basi itakuwa changamoto kubwa kwa uwekezaji mkubwa ambao serikali imeufanya katika uboreshaji wa miundombinu na programu za ufundi stadi.
Aidha, katika hotuba yake Ndunguru, amekumbusha nukuu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akifungua Bunge la 13 pamoja na ile ya kampeni zake, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwajengea vijana ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Amesema kauli hiyo ya Rais inaendelea kuwa dira muhimu ya NACTVET katika kuhakikisha kuwa mfumo wa TVET unaimarishwa kupitia viwango sahihi, taratibu madhubuti na miongozo inayokidhi mahitaji ya wakati na yale ya soko la ajira.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa viwango vipya vya ubora hauwezi kufanikiwa kama taasisi hazitasoma, kuelewa na kutekeleza kikamilifu miongozo iliyowasilishwa.
Ameonya kuwa ubora katika TVET hauji kwa bahati, bali unahitaji mpango thabiti, nidhamu ya kufuata kanuni na dhamira ya pamoja ya kuboresha utoaji wa mafunzo. Kwa msingi huo, Baraza litaendelea kutoa miongozo, kujenga uwezo na kutoa msaada unaohitajika ili kuhakikisha utekelezaji wa nyaraka hizo unakuwa wa ufanisi na endelevu.
Ametoa wito kwa taasisi zote za TVET kuvitumia viwango vipya vya ubora na miongozo iliyowasilishwa kama nguzo muhimu ya kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na usimamizi wa taasisi, ili hatimaye kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, umahiri na uwezo wa kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi.
Sambamba na hilo, amewahamasisha wadau kuendelea kushirikiana na Baraza kwa kutoa maoni na mrejesho wakati wa utekelezaji, akieleza kuwa maoni hayo ni muhimu katika kufanya maboresho ya baadaye ili kuhakikisha viwango vinaendelea kuwa vya kisasa na vinavyotekelezeka kulingana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama