January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwitikio watoto kushiriki vita dhidi ya mabadiliko tabianchi 

Judith Ferdinand

Ni dhahiri kwamba baadhi ya taasisi za umma na binafsi nchini zimeanza kuitika wito uliomo kwenye maazimio ya majukwaa ya kitaifa na kimataifa kuhusu kuwaashirikisha vijana na watoto katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, badala ya kuwataja kama waathirika pekee.

Shirika la Watoto Ulimweguni (UNICEF) katika Ripoti ya Hali ya Watoto Duniani 2024 (SOWC 2024), linatoa wito unaotaka kuchukuliwa kwa hatua kadhaa za kuhakikisha watoto wanapewa haki zao katika mchakato mzima wa vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Miongoni mwa hatua hizo kwa mujibu wa UNICEF katika ripoti hiyo ya Novemba 2024 elimu kama nyenzo kwa watoto kumudu uhimili wa mabadiliko ya tabianchi. “Uwekezaji katika elimu kuhusu tabianchi kwa watoto unaweza kuwajengea uwezo wa kuchangia suluhisho la muda mrefu huku wakijijengea uhimili,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Wito wa utoaji wa elimu kama nyenzo wezeshi kwa watoto na vijana wa Tanzania, pia imeakisiwa katika ripoti ya “Watoto kwa Hatua za Mabadiliko ya Tabianchi: Sauti kutoka Tanzania” ambayo inasisitiza umuhimu wa kuingiza mtazamo wa watoto katika suluhisho la athari za mabadiliko hayo.

Kwa upande mmoja, ripoti hiyo inaonyesha udhaifu wa watoto na vijana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini kwa upande mwingine inaonyesha uwezo wao wa kuleta mabadiliko ikiwa uwekezaji wa kuwajengea uwezo utafanyika miongoni mwao kwa kuwapa mafunzo na elimu stahiki.

Sauti za vijana wa Tanzania, zilizokolezwa kupitia utafiti wa U-Report uliohusisha washiriki zaidi ya watoto 12,000, zinaonyesha hitaji la haraka la elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi. 

Asilimia 60 ya vijana waliyohojiwa waliona kuwa shule zao hazishughulikii ipasavyo mzozo wa tabianchi, licha ya asilimia 80 kukubaliana kwamba elimu kama hiyo ni muhimu kwa mustakabali endelevu. Hii inaonyesha hitaji la haraka la kuingiza mabadiliko ya tabianchi katika mtaala wa shule.

Wito huo na mwingine mwingi kuhusu elimu ya mabadiliko ya tabianchi kwa watoto na vijana, umeanza kupata mwitikio kwani katika shule ya msingi Magaka, Kata ya Kahama, wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza, wanafunzi wanashiriki katika masuala yahusuyo utunzaji wa mazingira na kupewa elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Katika shule hiyo kuna Klabu ya Mazingira inayoundwa na wanafunzi wenyewe kwa ajili ya kulinda mazingira shuleni hapo, ikijihusisha na shughuli za upandaji wa miti, kuitunza na kuhakikisha unakua vyema.

Katibu wa Klabu hiyo, Fides Samwel, anasema Klabu hiyo ya shule wanatumia pia kwa ajili ya kuelimisha wanafunzi wenzao juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na athari zinazoweza kutokea kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Ushirikishwaji huu wa watoto jijini Mwanza, pia unashabiliana na ule ulioko katika Manispaa za Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambako Shirika la We World Tanzania linatekeleza mradi wa ‘PAMOJA TUNABORESHA ELIMU’ unawashirikisha wanafunzi katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoko katika tovuti ya We World, mradi huo unatekelezwa katika shule za msingi 10 ambazo ni Mtoni Kijichi, Bwawani, Buza, Kibondemaji, Ally Hapi, Bunju A, Kheri Missinga, Kawe A, Tumaini na Mtambani.

Pamoja na mambo mengine, kupitia mradi wa ‘PAMOJA TUNABORESHA ELIMU’ shule hizo zimeanzisha Klabu za utunzaji wa mazingira zinazotoa fursa kwa wanafunzi kushiriki katika mijadala, kupanda miti katika mazingira ya shule zao na kuitunza pamoja na kulima bustani ndogo za mbogamboga.

Athari nchini Tanzania

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kuzinduliwa Mei, 2023, inataja afya, chakula, elimu, maji safi na salama, mazingira, faragha na familia kama haki zinazoathiriwa zaidi na  mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, wakati  wa uzinduzi wa ripoti  hiyo amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kituo hicho kwa Kanda nne nchini, zikijumuisha mikoa ya Pwani, Mwanza, Manyara, Dodoma, Kagera, Mbeya na Dar es Salaam wanawake na watoto wameathirika zaidi na mabadiliko hayo. 

Septemba 2, 2024 aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) Dkt. Ashatu Kijaji alitaja athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kuwa ni mabadiliko ya hali ya hewa, ongezeko la joto, mvua zisizo za kawaida, dhoruba za kitropiki na mafuriko makubwa.

Dk. Kijaji akizungumza kwenye Jukwaa la 24 na Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ua Fedha ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (UNFCCC), jijini Arusha anasema mabadiliko tajwa yanaathiri uchumi na mifumo ya ikolojia za kijamii hivyo zinahitajika juhudi za ziada kukabiliana nayo.

“Changamoto hizi zinasababisha hasara kubwa na uharibifu wa miundombinu ya maji, barabara, umeme na kilimo na kusababisha uhaba wa maji na chakula kwa matumizi ya binadamu na wanyama,”anasema Dk. Kijaji ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Desemba 3, 2023 akizungumza kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi na afya kutoka nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika Dubai, aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu,anasema mabadiliko ya tabianchi, yamesababisha ongezeko la magonjwa ya milipuko na vifo hususani katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara. 

Ummy anayataja magonjwa hayo kuwa ni kuhara, malaria, dengue na magonjwa mengine yasiyopewa kipaumbele kama usubi, chikungunya, kichocho, matende na magonjwa ya mfumo wa hewa. 

“Magonjwa ya aina hii yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ongezeko la joto na mvua kubwa au chache zinazoletelezea mafuriko au ukame katika maeneo mbalimbali,”anasema.

Mtazamo wa watoto

Fides ambaye ni Katibu wa Klabu ya Mazingira ya shule ya msingi Magaka,anasema yatokeapo mafuriko ambayo husababishwa na mvua nyingi, wao ukosa utulivu wa kimasomo na wakati mwingine kushindwa kufika shuleni kama ilivyo kalenda ya Serikali ambayo inamtaka mtoto kuhudhuria masomo kwa siku 194 kwa mwaka. 

“Mvua kubwa zikinyesha, tunaweza kuathirika kielimu, kwani baadhi ya sehemu ambazo tunatumia kwa ajili ya kujifunza zinaharibika, wakati mwingine madarasa kubomoka, na miundombinu mingine iliyopo shuleni kuharibika,” anasema Fides ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo.

Kauli yake inaungwa mkono na mwenzake, Brightness Boniface, ambaye ni Mwanahabari mtoto kutoka MYCN ambaye anasema mvua zinaponyesha nyingi kupita kiasi, hunasababisha mafuriko ambayo hufanya wao kushindwa kwenda shuleni kwani njia zote zinakuwa zimejaa maji au miundimbinu inakuwa imeharibika.

“Pia mafuriko yanapotokea yanatuathiri sisi watoto kisaikilojia kwani tunaweza kuchukuliwa na kupelekwa kwenye makazi ambayo ni tofauti na mazingira ya nyumbani hivyo kukosa utulivu,” anasema Brighrtness, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Nyakurunduma,wilayani Nyamagana.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Magaka, Mshongo Mmbaga, anasema mabadiliko ya tabianchi ni janga la Dunia na siyo Tanzania pekee,ikichangiwa na ongezeko la watu duniani, na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti  kwa ajili ya kupata aidha nishati kwa ajili ya kupikia kama kuni na mkaa, pia kwa ajili ya ujenzi.

“Mabadiliko hayo pia yanaathiri elimu za wanafunzi, mfano kunapokuwa na jua kali kupita kiasi linasababisha joto kali, hali hiyo inaweza kusababisha mwanafunzi kushindwa kuwa makini darasani wakati mwalimu akiwa anafundisha na badala yake anajikita zaidi kujipepea ili kupunguza makali ya joto,” anasema Mmbaga.

Mamlaka za mitaa 

Ofisa Elimu Watu Wazima Divisheni ya awali na msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Magembe Masalu,anasema  mabadiliko ya tabianchi yakitokea yanaweza  kuathiri maendeleo au maisha ya watoto hususani wanafunzi.

“Ikitokea mlipuko wa magonjwa uliosababishwa aidha na mafuriko, mtoto pia anaweza kuathiriwa na ugonjwa huo  jambo ambalo litasababisha kushindwa kuhudhuria masomo  kama ilivyo mwongozo wa  Wizara ya elimu,” anasema Masalu.

Kwa upande wake Ofisa Mradi wa ustahimilivu endelevu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto mkoani Mwanza kutoka shirika la Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza(MYCN), Nuru Masanja, anasema kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi   kipindi cha kiangazi, watoto wanathirika  hasa maeneo ya vijijini  au kata ambazo  bado maeneo hayo hayajapatiwa huduma ya maji.

“Hivyo wakati huo watoto hao hufuata maji mbali, huku wakilazimika kuamka asubuhi kabla ya kwenda shule. Katika utafiti wetu wa awali, Kata ya Shibula maji ni shida kuna shule haina maji kabisa,  hivyo analazika kufuata maji mbali kwenye kidumu asubuhi hiyo. Swali ni je ikifika mchana hasa mtoto wa kike akiwa kwenye hedhi anafanyaje,?.

“Inakuwa ni shida na changamoto kwenye mazingira kama hayo yanamfanya mtoto awe mnyonge darasani, ashindwe kushiriki vyema, utoro shuleni na mwisho wa siku anashindwa kufanya vizuri shuleni,”anasema Masanja.

Mabadiliko ya tabianchi

Mtaalamu wa masuala ya Maliasili na Mabadiliko ya tabianchi Dk. Baruani Mshale anasema: “Tukizungumzia mabadiliko ya tabianchi tunamaanisha yale mabadiliko yanayotokea katika viwango vya wastani wa hali ya hewa katika eneo fulani kwa muda mrefu. Siyo kwa kuangalia  labda asubuhi, mchana, jioni au vipindi tofauti katika mwaka. Hapana,”anasema Dkt.Mshale na kuongeza:

 “Ni ile hali ambayo sasa inaenda ikibadilika kwamba ukiangalia tabianchi, au hali ya hewa mathalani ya Lushoto (Tanga) ya mwaka 2023, ni tofauti na mwaka 1970. Kwa hiyo, tunasema tabianchi ya Lushoto imebadilika,”.

Katika maelezo yake ambayo yamenukuliwa na mtandao wa The Chanzo, mtaalamu huyo anafafanua akisema: “Mfano mwingine ni mvua. Inaweza kuwa tulizoea katika eneo fulani mvua zinanyesha kuanzia Machi mpaka  Juni na zinanyesha kwa kiwango fulani. Lakini unakuta kwamba eneo lilelile siku hizi mvua zinaanza kunyesha labda Aprili halafu kwa muda mfupi lakini mvua kubwa sana, na mwezi Mei mvua zinakata,”.

“Kwa hiyo, hapo tunasema tabianchi ya lile eneo, kwa kuangalia kigezo cha mvua, imebadilika kwa sababu sasa mvua zinanyesha katika kipindi ambacho sicho tulichozoea na kiasi cha mvua kinachonyesha sicho tulichokizoea vilevile,” anafafanua Dkt. Mshale.

Mtaalamu huyo anasema kwa Tanzania hali ya aina hiyo imeishatokea na ushahidi upo katika maeneo tunakoishi. “Ndiyo maana unasikia watu wanasema zamani palikuwa hivi na siku hizi pamekuwa hivi. Hiyo ndiyo inaashiria kwamba tabianchi ya lile eneo imebadilika kwa sababu ile hali ya hewa sasa katika muda mrefu imebadilika,” anasisitiza Dkt. Mshale.