Joyce Kasiki
KATIKA kufika malengo ya Taifa ya Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26 ) Serikali kupitia mradi wa Boost inatarajia kujenga vyumba vya madarasa ya awali elfu kumi na mbili (12,000) pamoja na michezo ya watoto kwa kutumia pesa kutoka serikali Kuu,mapato ya ndani ya halmashauri,wadau na michango ya wananchi.
Hii ni kutokana na umuhimu mkubwa kwa watoto kujifunza katika mazingira bora hasa wakiwa wadogo yanavyoweza kujifunza vyema na kwa haraka na kumudu stadi za kusoma,kuandika na kuhesabu kabla ya kuingia darasa la kwanza
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt.Festo Dugange ,mradi wa Boost umebuniwa kutokana na umuhimu wa elimu kwa mtoto mdogo ambapo serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kufundishia watoto wa darasa la awali kupitia miradi mbalimbali .
“Na madarasa yale tumehakikisha yanakuwa na sifa za kumvutia mtoto yamejengwa na kuwekwa vitu vya kujifunzia, lakini pia yanakuwa na michoro ya herufi,wanyama kwa maana ya vitu vinavyoelezea kwa picha na kuonesha namna ambavyo mtoto anaweza kujifunza , kutamani kusoma na hatimaye kupunguza utoro kwa watoto hao.’’
Dkt Dugange ameongeza kuwa serikali ilishaelekeza mamlaka zote za serikali za mitaa nchini kuhakikisha kwamba madarasa ya awali yawe ni kipaumbele kwa mapato ya ndani ya halmashauri ili kuwezesha watoto ambao hawajafikiwa namadarasa hayo waweze kufikiwa.
“Serikali imeendelea kujenga kila mwaka madarasa ya awali na shule shikizi lengo ni kuhakikisha kila watoto wanapofikisha angalau miaka minne na kuendelea wanakuwa na madarasa ya awali,kwa sasa maelekezo ni kwamba kila shule ya msingi ni lazima iwe na darasa la awali na kunakuwa na walimu wa darasa hilo lakini pia imeondoa ada,
“Na hayo yote yamesaidia lakini pia jamii imeelimika ambapo kwa sasa kukuta mtoto wa miaka mitano haendi shule,ni aghalabu sana ,watoto hao wengi sasa wapo wanasoma kwenye shule za serikali bila gharama na wanaendelea kupewa elimu pamoja na malezi na makuzi ,kwa hayo ni mafanikio makubwa sana katika kujenga Taifa ,”anasema Dkt Dugange
Mratibu wa Mradi wa Watoto Wetu Tunu Yetu unaotekelezwa na Shirika la CiC Faraji Paragha anasema,kati ya kipindi cha 2020 hadi 2024 Shirika hilo limeweza kuzifikia shule zote 831 katika mkoa wa Dodoma madarasa yamekuwa changamshi huku walimu 837 wakipatiwa mafunzo ya kufundisha darasa la elimu ya awali.
Anasema kati ya shule hizo 831,vyumba vya madarasa 290 vimefanyiwa ukarabati,ofisi za walimu na vyumba 32 vimejengwa upya katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.
Aidha anasema,kutokana na umuhimu wake,shirika hilo pia limetoa mafunzo kwa Maafisa elimu kata 204 na walimu wakuu 831 kwa lengo la kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi juu ya elimu ya watoto wa darasa la elimu ya awali.
“Matokeo makubwa ni kuongezeka kwa utayari kwa watoto wanaoingia darasa la kwanza na kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), kabla ya kuingia darasa la kwanza na kuwawezesha kujifunza kwa haraka zaidi,
“Pia imepunguza idadi ya watoto wsiojua kusoma na kuhesabu ,walimu wameongeza ujuzi stadi na maarifa katika kumudu darasa la elimu ya awali kwa sababu walimu walio wengi ni walimu wenye taaluma ya ualimu na hawana taaluma ya kufundisha darasa la elimu ya awali.”anasema Paragha
Paragha anasema ,kuna ongezeko la kipaumbele na uwekezaji katika darasa la elimu ya awali ambapo shule nyingi zimetenga darasa maalum kwa ajili ya watoto hao,pia watoto wanapata uji shuleni na hivyo kuongeza ari ya kupenda shule.
Baadhi ya walimu wa darasa la elimu ya awali wanaipongeza serikali na wadau hasa CiC kwa juhudi wanazofanya kuhakikisha darasa hilo linapewa kipaumbele .
Mwalimu wa darasa la awali katika shule ya msingi Nkuhungu Jijini Dodoma Emma Maria anasema kupitia mradi wa shule Bora darasa la awali limeboreshwa katika shule hiyo na hivyo kuendelea kuleta matokeo chanya katika ujifunzaji na ufundishaji wa watoto hao.
“Naishukuru Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya darasa la elimu ya awali kupitia miradi mbalimbali,lakini pia naishukuru CiC kwa mafunzo kwa sisi walimu wa darasa hili ,maana kwa mfano mimi ni mwalimu wa kawaida tu kwa hiyo kabla sijapata mafunzo iliniwia vigumu sana kufundisha watoto,
“Lakini kupitia mafunzo hayo sasa nina mbinu nyingi za kufundisha na kulimudu darasa langu lenye watoto 132,na sipati shida kutokana na wingi wao.’anasema Maria
Selina Kadelewe mwalimu kutoka shule ya msingi Songambele ,Kongwa mkoa wa Dodoma anasema mafunzo kwa walimu,uboreshaji madarasa na miundombinu ya darasa la elimu ya awali,imekuwa ni chachu kwa walimu,wanafunzi na hata wazazi na hivyo kupunguza utoro.
“Siku hizi watoto hawa wanapewa kipaumbele,lakini zamani hawakuonekana umuhimu wao,kwa mfano darasa langu lilikuwa chini ya mbuyu,
“Lakini sasa baada ya mafunzo ya walimu hadi viongozi wetu shuleni na kwenye kata,umuhimu umeonekana, sasa darasa la awali ni zuri lina mlango na madirisha ya vioo.”anasema Kadelewe
Hassan Juma mkazi wa Nkuhungu anaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuwekeza kwa watoto huku akiomba elimu zaidi ya malezi watoto wadogo itolewe kwa jamii,wazazi na walezi ili waone umuhimu wa elimu ya darasa hilo lakini kushiriki kwenye kuandaa zana za watoto shuleni na hata nyumbani ili wajifunze kwa urahisi
Mradi wa Boost ni mwendeleo wa juhudi za SERIKALI kutekeleza wajibu wake pamoja na kuitikia wito wa wadau wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto likiwemo shirika la kuhudumia watoto wenye changamoto mbalimbali (CiC) katika kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu kwa darasa la elimu ya awali.
Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ,tafiti mbalimbali za kisayansi duniani zinasisitiza kwamba ,msingi imara unatakiwa ujengwe katika miaka ya awali ya mtoto na kwamba huo ndio wakati muhimu wa kuwekeza kwenye maisha ya mwanadamu.
More Stories
SHUWASA yaboresha mtambo wa kuchakata takakinyesi
Daktari ajishindia milioni 100,fainali NMB Bonge la Mpango
Majaliwa ataka tenki la Kisesa lianze kutoa maji Februari