January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwili wa Mwandishi Riziki Abraham waagwa

Na James Mwanamyoto, Dodoma

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Mary Mwakapenda kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro, amepongeza utendaji kazi wa marehemu Riziki Abraham wa kuitekeleza vema kaulimbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE wakati wa uhai wake kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, maarifa na weledi. 

Mume wa marehemu Riziki Abraham, Joseph Michael Kiringo (wa kwanza kulia) na mwanae wa kike (wa pili kulia kwake) wakiwa na waombolezaji wengine kwenye ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Mary Mwakapenda ametoa pongezi hizo, wakati wa Misa Takatifu ya kumuombea marehemu Riziki Abraham iliyofanyika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Padri Gaetano Maswenya akihubiri wakati wa misa ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bi. Mary Mwakapenda akiwasilisha salamu za rambirambi za Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Mary amefafanua kuwa, marehemu Riziki alikuwa ni mtumishi mwema aliyetekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kuongeza kuwa, alikuwa akishirikiana vema na wanatasnia wenzie kutekeleza majukumu ya kitaifa, hivyo anapaswa kuenziwa na wanahabari kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mhe. Rais ya KAZI IENDELEE.

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Habari – MAELEZO Bw. Rodney Thadeus akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Naye, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Habari – MAELEZO, Rodney Thadeus akizungumza kwa niaba ya Mkutugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, amesema, Riziki alikuwa ni mwepesi wa kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu majukumu yanayotekelezwa na Sekretarieti ya Ajira hivyo, taifa limempoteza mtu muhimu ambaye bado alikuwa akihitajika kuuhabarisha umma.

“Tangu nimfahamu marehemu Riziki sijawahi kusikia juu ya taarifa yoyote ambayo aliitoa na ikaleta sintofahamu katika jamii, huu ni uthibitisho tosha wa umahiri wake,”amesisitiza Thadeus.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini Tanzania (TAGCO), Abdul Njaidi, amesema marehemu Riziki, alifanikiwa kutekeleza jukumu kubwa la kutangaza shughuli zinazotelelezwa na taasisi zote alizozitumikia ikiwa ni pamoja na mafanikio yaliyopatikana. 

Njaidi ameeleza kuwa, marehemu Riziki alikuwa hawezi kufanya jambo la kitaaluma bila kuuliza au kuomba ushauri wa kitaaluma hivyo ameacha mfano mzuri wa kuigwa. 

Mhandisi Samweli Tanguye akielezea namna walivyofanya kazi na marehemu Riziki Abraham wakati wa ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu huyo, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Afisa Utumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bi. Neema Kivugo akisoma wasifu wa marehemu Riziki Veneranda Abraham wakati wa ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma.

James Mkuwa, aliyekuwa akishirikiana na marehemu Riziki kutunza nyumba ya mapradri “Betania House” iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam amesema, marehemu alikuwa ni mtu asiyejikweza kwani baada ya kifo chake ndio amefahamu marehemu alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Amesema, marehemu Riziki mpaka mauti yanamkuta amekuwa akitekeleza jukumu lake la kutoa habari kwani muda wote alikuwa akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya afya yake tangu aanze kuumwa na kuongeza kuwa, hakika amefia taaluma yake ya habari.

Kwa niaba ya Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Mhandisi Samweli Tanguye amesema, marehemu Riziki ameifanya kazi ya kuitangaza taasisi kwa kiwango cha kutukuka kwa kipindi cha miaka 10.

Mhandisi Tanguye ameeleza kuwa, marehemu amezunguka nchi nzima bara na visiwani kuitangaza taasisi, hivyo ameingia katika historia kwa kuwa msemaji wa kwanza wa Sekretarieti ya Ajira ambaye alitekeleza majukumu yake kwa ufanisi na mafanikio makubwa.

Kutokana na maelezo kuhusu umahiri wa marehemu Riziki Abraham enzi za uhai wake, Padri Gaetano Maswenya ametoa pole kwa mume wa marehemu na familia ya wanahabari kwa kuondokewa na mtu makini na shabiki mwenzie wa yanga, hivyo ametoa wito kwa wanatasnia na waumini kuendelea kumuombea. 

Marehemu Riziki Veneranda Abraham amefanya kazi Ofisi ya Makamu wa Rais Mwaka 2005 hadi 2010 na mwezi Novemba 2011, alihamishiwa Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Cheo ambacho amekitumikia hadi umauti ulipomfika tarehe 22 Juni, 2021.