Na Yusuph Mussa,TimesmajiraOnline,Korogwe
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa kongole kwa Mradi wa Maji wa Miji 28 kwa Mkoa wa Tanga unaojengwa kwenye miji ya Korogwe, Muheza, Pangani na Wilaya ya Handeni, na kusema una hadhi ya nchi inayoendelea, na utakuwa mkombozi kwa wananchi 860,000.
Amesema pongezi ziende kwa Rais wa Tanzania Dkt. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo na miradi mingine inayofanana na huo, na kuongeza kuwa mradi huo utaupa heshima Mkoa wa Tanga, na kuleta tija kwa wananchi kuweza kupata maji.
Ameyasema hayo Februari 14, 2026 alipofika kukagua chujio la mradi huo linalojengwa Kijiji cha Mswaha, Kata ya Mswaha- Darajani, Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe.

“Na leo hii tunakuja kuuona mradi mwingine unaofurahisha hata kuungalia tu. Ni mradi wenye hadhi ya kiongozi anaejali mambo ya maendeleo. Mradi huu kwa nchi nyingine ungetekelezwa mmoja kwa nchi nzima, lakini kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka fedha hapa ili zisaidie Wilaya ya Korogwe, Wilaya ya Muheza, Wilaya ya Handeni na Wilaya ya Pangani.
“Mikakati kama hii inaendelea maeneo mengine. Waziri (wa Maji, Jumaa Aweso), niliweka Jiwe la Msingi mradi wa aina hii kule Mwanza. Pia umeelezea kuna mradi wa aina hii kule Tunduma, umeelezea kuna mradi mwingine unaendelea kule Mara. Huyu ndiye Rais anaejali maendeleo ya wananchi wake, na haya sio maneno yangu mimi mgeni niliyekuja hapa, ninyi wenyewe mmeona shughuli zinazoendelea hapa, mmeona majengo yanayojengwa hapa” alisema Dkt. Mwigulu.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri alisema Mradi wa Maji Miji 28 kwa Mkoa wa Tanga utahudumia wananchi wa miji ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani.
Mhandisi Waziri alisema mradi huo umetokana na mradi uliokuwepo awali wa Handeni Trunk Main (HTM) uliojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GTZ) na sasa GIZ mwaka 1974, na ulitakiwa ufanyiwe matengenezo makubwa ya miundombinu baada ya miaka 20 yaani mwaka 1994, lakini hakuna matengenezo makubwa yaliyofanyika kwa miaka 50.
Amesema mradi wa awali na wa sasa ambao chanzo chake ni Mto Pangani, na kidakio (Intake) kikiwa kimejengwa Kijiji cha Mswaha, wilayani Korogwe, ulikuwa unazalisha maji lita milioni nne (4) kwa siku na kuhudumia wananchi 180,000 kwenye vijiji 60, lakini mradi wa sasa unakwenda kuzalisha lita milioni 52 kwa siku na kuweza kuhudumia wananchi 860.
Mhandisi Waziri alisema ukiacha miji itakayohudumiwa na maji hayo, vijiji 180 vitavyozunguka bomba hilo pia vitanufaika na maji hayo.

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini CPA Charles Njama amesema wakati wanafanya kampeni kwenye Uchaguzi Mkuu, mwaka 2025, kero kubwa ya wananchi ilikuwa maji, lakini kutokana na mipango ya Serikali katika kutatua changamoto hiyo, shida ya maji Mji wa Korogwe itakuwa historia.
“Wakati wa kampeni moja ya changamoto kubwa iliyokuwa inalalamikiwa na wananchi ni maji. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea mradi mkubwa wa maji. Uzalishaji wa maji kwa sasa Jimbo la Korogwe Mjini ni lita 3,800,000 kwa siku, lakini mahitaji yetu kwa siku ni lita 6,200,000, hivyo tuna upungufu wa lita 2,500,000, lakini mradi huu unakwenda kutuletea maji wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini lita milioni 10.5 kwa siku.
“Lakini pia, tuna mradi mwingine ambao ujenzi wake umefikia asilimia 15, Mradi wetu wa Ndemaha ambao utatuletea maji lita milioni 6.2 kwa siku. Hivyo kwa miradi hii miwili itakapokamilika itatupatia lita milioni 17.7 kwa siku, na kufanya tuwe na ziada ya lita milioni 11.1. Hivyo niwaombe wananchi waendelee na uvumilifu, kwani hii shida tunakwenda kuimaliza kabisa.
CPA Njama alisema anafahamu jitihada za Serikali kuweza kupeleka maji kwa wingi kwa wananchi, lakini ameiomba Serikali, inapojenga miradi ya maji, pia iimarishe miundombinu ya maji, hasa kwenye mji mkongwe kama Korogwe ambao miundombinu yake ina zaidi ya miaka 50, na ni chakavu.
“Lakini Waziri Mkuu, moja ya changamoto tunayokwenda kuiona mbele ni usambazaji wa miundombinu ya maji. Miundombinu ya maji tuliyonayo sasa ni chakavu, tuliongea na kushauriana na wataalamu wetu, ni vizuri tuweke kipaumbele na kuhakikisha kwamba miundombinu inakwenda kusambazwa vya kutosha, ili maji yanapofika mjini Korogwe wananchi wote wanufaike na maji hayo, na yaweze kukidhi matarajio yao” alisema CPA Njama.


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama