Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Mwanza
MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mwamini Malemi, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake ya kuifungua nchi, kuongezeka fursa za uwekezaji kwa kuendeleza miradi ya kimkakati ambapo kwa upande wa Mfuko umeweza kupata wanachama wapya kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi pamoja na kukusanya michango.
Mwamini amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua Mkutano wa 52 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF lililofanyika jijini Mwanza.
Amesema NSSF itaendelea kusimamia maono ya Serikali ya awamu ya sita, kuwafikia wanachama waliopo katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kwa kuwapa elimu na kuwaandikisha kwenye Mfuko.
“Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza, Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya ndani ya miaka hii mitatu ya uongozi wake ikiwa ni usimamizi thabiti wa miongozo ambayo amekuwa akiitoa kwa kuwezesha sekta ya hifadhi ya jamii nchini,” amesema Bi. Mwamini.
Amemuhakikishia Rais Dkt. Samia kuwa NSSF itaendelea kusimamia maono ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha kuwa Watanzania waliopo katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi wanasajiliwa na kujiunga na NSSF pamoja na waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.
Naye, Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia imechangia mafanikio ya NSSF kutoka trilioni 4.8 mwezi Machi, 2021 hadi kufikia trilioni 8.1 hivi sasa sawa na ongezeko la asilimia 67.
“Wakati Serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani mwezi Machi 2021, thamani ya NSSF ilikuwa ni shilingi trilioni 4.8 lakini hivi sasa kwa mujibu wa hesabu ambazo hazijakaguliwa thamani ya Mfuko ni trilioni 8.1 sawa na ongezeko la asilimia 67,” amesema Mshomba.
Amesema NSSF kwa namna ya pekee wanamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa aliyofanya ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake kwa sababu kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri wa sekta binafsi katika miradi ya kimkakati, mazingira mazuri ya uwekezaji ambapo kwa upande wa NSSF imekuwa ikipata wanachama wapya na kukusanya michango.
Mshomba amesema pia mafanikio ya NSSF yamechangiwa na Bodi ya Wadhamini, Baraza la Wafanyakazi pamoja na watumishi wote.
Ametoa rai kwa waajiri wa sekta binafsi kuendelea kutekeleza sheria kwa kuwasilisha michango, kusajili wafanyakazi wapya ili kuuwezesha Mfuko kulipa mafao kwa wakati kwani kutowasailisha michango ya wanachama kunasababisha usumbufu ikiwemo Mfuko kushindwa kulipa madai ya mwanachama kwa wakati stahiki.
“Moja ya sababu ambazo zinafanya tuchelewe kulipa kwa wakati ni pale ambapo anakuja mstaafu lakini hana michango, katika hali ya kawaida inatuwia vigumu kutekeleza jukumu hilo, hivyo ni muhimu kila mwajiri kutimiza wajibu wake kwa kulipa michango kwa wakati,” amesema Mshomba.
Amesema NSSF inaendelea kuweka juhudi kubwa kuhakikisha waajiri wote wa sekta binafsi wanatimiza takwa la kisheria la kuwasilisha michango kwa wakati pamoja na kuboresha huduma kwa wanachama na wadau.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua