February 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti ALAT afanya dua kumshukuru Mungu kwa uhai

Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online Bukoba

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ( ALAT )Taifa ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Bukoba, Murshid Ngeze amefanya dua ya kumshukuru mwenyezi Mungu baada ya kunusurika na kifo katika ajali iliotokea Desemba mwaka 2022,ambayo ilisababisha kupoteza mguu wake mmoja.

Dua hiyo imefanyika Februari 24,2025 kKata ya Rukoma iliyopo Bukoba Vijijini,ambayo imefanywa na viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Mchungaji Mathias Buberwa kwa niaba ya Askofu Abednego Keshomshahara wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania( KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi,Padri Achileus Rugemalira Paroko wa Parokia ya Ichwandimi na Shekhe wa Wilaya ya Bukoba Twahir Said.

Ngeze,amesema hakuna anayeweza kuzuia ajali isitoke lakini hatasahau katika maisha yake jinsi fuso lilivyotaka kumsaga mzima mzima,lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu alimsaidia akaweza kukwepa na kuguswa baadhi ya viungo vyake vya mwili na kupelekea kupoteza mguu wake mmoja.

“Nimepata funzo kuwa ukipata ajali huruhusiwi kunywa maji, kwa sababu nilipata kiu sana nikaomba maji ya kunywa nikapewa, wakati nataka kunywa akatokea kijana mmoja akapiga chupa ya maji niliyoshika ikadondoka na maji yakamwagika kwanza nilimchukia.Kijana yule akaniangalia na kuniambia kaka utakufa hapa kisha akaniambia subiri nakuja,akarudi na mpira wa baiskeli na kunifunga miguu yangu yote miwili,”amesema na kuongeza:

“Alipomaliza kunifunga miguu akaniambia ungekunywa maji usingemaliza dakika tano ungepoteza maisha,kwa sababu maji yanasukuma damu ingeenda kwa kasi na kutoka nyingi, na amenifunga ili kuzuia damu na niweze kuwahi hospitali,nilimpigia Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani na walifika kunisaidia,”amesema Ngeze.

Hata hivyo amesema,hatasahau kauli iliyotolewa na Askari kuwa huyu hata tukimpeleka hospitali ameshafariki lakini Mungu ni mkubwa yupo anadunda.Ambapo baada ya kuzinduka kwa ajili ya maandalizi ya upasuaji kwa mara ya kwanza,alimuona aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI wakati huo Angela Kairuki,akasema amefika hapo kwa maelekezo ya kusimamia matibabu yangu.

Sanjari na hayo amesema kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan,amesimamia hatua zote za matibabu yake ikiwemo gharama za matibabu aliyoyapata.

“Nilikua naumia,najiuliza mke wangu nitamuachaje na watoto,nimesaidiwa na wengi shukrani za pekee zimuendee Rais wa Samia Suluhu Hassan,nilipewa madaktari bingwa wawili ambao ni Dk.Boniface na Dk.Antony wa kusimamia matibabu yangu katika hospitali ya Taifa Muhimbili,”amesema Ngeze na kuongeza:

“Tukiwa India na mke wangu aliugua madaktari wakasema anaumwa zaidi kuliko mimi walipotaka kumhudumia kwa upendo wake kwangu aliwaeleza madaktari wanihudumie mimi kwanza hakuwa mbali na mimi kipindi hicho chote Mungu ambariki”anasema Ngeze.

Kwa upande wake Faris Buruan Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Kagera na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM )Taifa ,amesema ajali ilikuwa mbaya hawakutegemea kama mwaka 2025 angeweza kufika akiwa bukheri wa afya.

Baruan,amesema vijana wa Mkoa wa Kagera hawawezi kwenda kinyume na kusudio la Mwenyezi Mungu kwa sababu uhai alionao Ngeze ni kusudio la Mungu hivyo vijana watasimama naye kuhakikisha anaendelea kuwatumikia wananchi.

Katibu Mkuu wa ALAT Taifa Mohammed Maje,amesema Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa Ngeze ni kielelezo cha mfano wa kuigwa na jamii katika maisha, kwani haijalishi amepitia magumu kiasi gani lakini ameendelea kusimama imara kutekeleza majukumu yake kama Diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba pia Mwenyekiti wa ALAT Taifa.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima,amewasisitiza wanawake kuwa wavumilivu na kutoikimbia familia pindi waume zao wanapopata changamoto mbalimbali ikiwemo ugonjwa.