October 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wazindua zahanati Chitete kuhudumia wakazi 8,784

Na Moses Ng’wat, Momba

WAKAZI 8,784 wa Kijiji cha Chitete, Wilaya ya Momba mkoani Songwe, wanatarajia kuanza kupata huduma za afya karibu na makazi yao baada ya kuzinduliwa kwa zahanati mpya iliyogharimu Sh Mil 265.

Zahanati hiyo imezinduliwa Oktoba 9, 2026 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ambapo itapunguza changamoto ya wananchi kufuata huduma za afya katika maeneo ya mbali.

Akisoma taarifa ya mradi huo wakati wa uzinduzi, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Momba, John Mwita, amesema zahanati hiyo imekamilika na ipo tayari kuanza kutoa huduma kwa wakazi wa kijiji hicho.

Amesema ujenzi wa mradi huo umehusisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), nyumba ya mtumishi, ukarabati wa jengo la mama na mtoto pamoja na ujenzi wa matundu matatu ya vyoo.

Mwita amesema kukamilika kwa zahanati hiyo kutawawezesha wakazi 8,784 kupata huduma za afya karibu na makazi yao, hatua inayotarajiwa kupunguza usumbufu wa kutembea umbali mrefu kuzifuata.

“Tunaiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za mradi huu wa afya ambao mpaka sasa umekamilika na upo tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Mwita.

Kwa upande wake, Kiongozi huyo wa mjio za Mwenge, Mwang’onda amewataka wananchi kuitumia zahanati hiyo ipasavyo ili wanufaike na uwekezaji uliofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za afya.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha huduma muhimu za kijamii, ikiwamo afya, zinawafikia wananchi karibu na makazi yao ili kupunguza changamoto za upatikanaji wake.

“Wananchi wanatakiwa wanufaike na mradi huu ipasavyo na si kwa mateso, kwani dhamira ya Serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinasogezwa karibu na wananchi,” amesema Mwang’onda.