Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Nsimbo.
MWENGE wa Uhuru umezindua Nishati safi ya Kupikia wenye thamani ya shilingi milioni 29 katika shule ya sekondari Nsimbo ambao umeokoa matumizi ya kuni tani milioni 1 na laki 5 kila baada ya miezi kadhaa shuleni hapo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi, Septemba 25, 2025 akizindua mradi huo wa Nishati Safi amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alikuja na kampeni hii baada ya utafiti kufanyika kwamba Watanzania wengi wanapata madhara ya kiafya kwa sababu ya matumizi ya kuni.

Ussi alifafanua ndani ya mkakati huo ambao ni wa miaka 10 Rais Dkt.Samia anataka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza chachu kufikia malengo yake ya kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2033.
Mkuu wa shule ya sekondari Nsimbo Restuta Msafiri, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Nishati Safi amesema mradi huo utahudumia wanafunzi kati ya 800 hadi 1000 na watumishi 32.
Mwl.Restuta amesema matumizi ya nishati hiyo umepunguza gharama za kupikia kutoka shilingi milioni 1 na laki 8 zilizokuwa zinatumika kwa kuni hadi shilingi milioni 1 na laki 581 hivyo kuokoa shilingi milioni 218 na laki 823.

“Nishati safi hii imeongeza uharaka na ufanisi wa maandalizi na utoaji wa chakula shuleni na kujikinga na magonjwa yatokanayo na natumizi ya nishati zisizo rafiki kwa binadamu na mazingira” Ameongeza.
Afisa Mazingira na Mratibu wa Nishati Safi Halmashauri ya Nsimbo Debora Msigwa amesema nishati hiyo imesaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa jambo ambalo linasaidia katika uhifadhi wa uoto wa asili.
Debora amesema suala la utunzaji wa mazingira ni jambo nyeti ambalo wanalishughulikia ipasavyo kupitia kutoa elimu kwa wananchi kuondokana na nishati isiyofaa huku akieleza madhara ya uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa kama vile kusababisha ukame na mmomonyoko wa ardhi.
Mkazi wa kijiji cha Mtapenda Shija Zachalia, amesema elimu ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia inapaswa kutolewa zaidi maeneo ya vijijini hivyo amewaomba wenye mamlaka kutoa elimu zaidi.
Vilevile ameishukuru serikali kwa kuwapatia mitungi ya gesi ya bei nafuu ambayo inawasaidia kupikia na kuepusha madhara yatokanayo na matumizi ya kuni na mkaa.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi