Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava ameweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Magila- Gereza huku akieleza kuwa Mkoa wa Tanga una vyanzo vingi vya maji na wakiendele kutunza vyanzo hivyo, hawatakuwa na shida ya maji kwa muda mrefu ujao.
Ameyasema hayo Aprili 9, 2024 wakati alipotembelea mradi huo uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo mara baada ya kukagua na kujiridhisha aliweka jiwe la msingi ambao umefikia zaidi ya asilimia 90.
“Mkoa wa Tanga una vyanzo vingi vya maji, hivyo ni jukumu lenu kutunza vyanzo hivyo ili viweze kuwa endelevu na kuendelea kupata maji,nimeridhika na mradi wa maji kuanzia nyaraka na vielelezo vyote,ujenzi wake ni mzuri,malizieni huu mradi ili wananchi wanywe maji, lakini hata mimi maji nimeyaona,”amesema Mnzava.
Awali, akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Mei 31, 2022.
Huku lengo la mradi huo ni kutekeleza adhima ya Serikali ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi wapatao 4,543 wa vijiji vya Magila- Gereza, Nkalekwa na Mgobe ambao thamani yake ni milioni 775.7, kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF).
kazi zilizopangwa na kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji ambao upo asilimia 95, tanki la ujazo wa lita 300,000 kwa asilimia 95, BPT 5 kwa asilimia 95, mtaro na kufunga mabomba mita 26,314 kwa asilimia 80, Vilula (DPs) 28 kwa asilimia 90, alama za njia ya bomba 264 kwa asilimia 20 na valvu chemba 34 ujenzi wake bado.
“Ili uwe endelevu wananchi wameshirikishwa katika hatua zote za utekelezaji wake kwa sasa kimeundwa chombo cha kijamii cha Watumia Maji (CBWSO),pamoja na Serikali kufanikiwa kuondoa kero ya maji pia imewezesha wananchi wapatao 70 kupata ajira ya muda katika kipindi chote cha ujenzi wa mradi huu,”ameeleza Mhandisi Tupa.
Aidha vijana wapatao watano wameajiriwa na chombo cha kijamii cha watoa huduma ya maji ambacho ndicho chenye wajibu wa kuendesha mradi huu kwa niaba ya wananchi.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu