Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Hanang
Mwenge wa Uhuru umetua Mkoa wa Manyara ukitokea Mkoa wa Singida,ambao utatembelea jumla ya miradi 57 yenye thamani ya bilioni 149.5.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava , wakati wa mapokezi ya Mwenge huo katika Kijiji cha Gehandu wilayani Hanang mkoani humo.
Sendiga amesema Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Manyara utakimbizwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 7 ambazo ni Hanang, Mbulu Wilaya, Mbulu Mji, Babati Wilaya, Babati Mji, Kiteto na Simanjiro kwa mzunguko wa kilometa 980.5.
Pia utaweka mawe ya msingi miradi 17 yenye thamani ya bil.134.1, kuzindua miradi 8 yenye thamani ya bil.3.4, kufungua miradi 4 yenye thamani ya bil.1.3 na kukagua miradi 28 yenye thamani ya bil.10.7.
” Mchangnuo katika uchangiaji wa miradi hii ni kama ifuatavyo, nguvu za wananchi milioni 102.5, Serikali Kuu bilioni 72.8, Halmashauri milioni 169.7 huku wadau wengine wakichangia bilioni 76.5,” amesema Queen Sendiga.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kuibua, kuanzisha , kuchangia na kuitekeleza miradi hiyo pamoja na wadau wa maendeleo ambao wameweza kuchangia shughuli za maendeleo katika Mkoa huo.
” Tunafahamu mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024 ni mbio Maalum kwani zinatimiza miaka 60 Tangu zilipoanza, lakini pia imetimia miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na vilevile imetimia miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tangu ilivyoasisiwa na viongozi wetu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Kalume ( Mungu azilaze roho zao Mahali pema peponi),”amesema Sendiga.
Hata hivyo Mkuu huyo amefafanua kuwa pamoja na jumbe zingine za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2024, Mkoa wa Manyara umejianda kuupokea ujumbe mahususi unaosema ” Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu”.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa