December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wa Uhuru wataka mtandao dawa za kulevya kufichuliwa Tunduma

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline, Tunduma.

WAKAZI katika mji wa mpakani wa Tunduma, Wilayani Momba, Mkoa wa Songwe wametakiwa kushirikiana na serikali kufichua wanaoingiza na kusafirisha dawa za kulevya kupitia mpaka wa Tunduma.

Wito huo umetolewa leo Septemba 5, 2023 na mmoja wa Wakimbiza Mwenge wa kitaifa kwa niaba ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdalla Shaibu Kaim wakati akitoa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru katika eneo la Kilimanjaro katika Mji huo wa mpakani wa Tunduma, Wilayani Momba.

Amesema ni muhimu na wajibu wa kila mwananchi katika mji huo wa mpakani ambao una mwingiliano mkubwa kuhakikisha anakemea vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya, ikiwemo kutoa taarifa kwa vyomba vya dola ili wahudika watiwe nguvuni.

Amesema ili kuhakikisha vijana katika mji huo wa Tunduma na watanzania wengine hapa nchini wanabaki salama na kujikita katika shughuli za maendeleo ya ujenzi wa Taifa ni lazima mapambano dhidi ya dawa za kulevya iwe ya kila mtu.

Aidha, Mkimbiza mwenge huyo, Zainabu Mbetu amesistiza na kuwaasa wananchi juu ya mtumizi ya vyandarua, hasa vilivyotiwa dawa ya kuua mbu na kuonya jamii kuacha mara moja kubadili matumizi ya vyandarua hivyo ambapo alisema kuna baadhi ya wanachi wamekuwa wakivitumia kwa kuvulia samaki , kufugia kuku.

Kadhalika, kiongozi huyo wa mwenge wa uhuru aliwataka wale wanaopimwa na kubainika kuambukizwa ugonjwa wa malaria kutumia kwa usahihi dawa wanazopatiwa hospitalini na wasikatize dozi.

Ukiwa katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma Mwenge wa uhuru umepitia miradi tisa yenye thamani ya shilingi za kitanzania bilioni 3.08 mbayo yote imekubaliwa na Mwenge huo kuendelea na utekelezaji wake.

Mwenge wa Uhuru kesho utakamilisha mbio zake Mkoani Songwe kwa kukimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje na siku ya Septemba 02 utakabidhiwa Mkoani Mbeya.