November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wa Uhuru wapokelewa Songwe,miradi ya zaidi ya bilioni 15 kuzinduliwa

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Momba.

MWENGE wa Uhuru umepokelewa leo Septemba 2, 2023 mkoani Songwe ukitokea Mkoa wa Rukwa ambapo utazindua, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 47 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 15 ikihusisha miradi ya sekta za afya,elimu,maji pamoja na utunzajj wa mazingira .

Akisoma taarifa ya miradi hiyo mara baada ya kukabidhiwa mwenge huo katika kijiji cha Kamsamba na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Lazaro Komba, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Fransis Michael amesema kuwa miradi hiyo imetekelezwa kwa fedha za serikali pamoja na nguvu za wananchi hivyo kukamilika kwake itasaidia kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wananchi kwenye maeneo yao.

Amesema Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Songwe utapitia miradi 47 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 15 na kati ya miradi hiyo, miradi 10 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 3,itazinduliwa huku miradi 5 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 1, itafunguliwa.

Dkt. Michael ameongeza kuwa, miradi mingine 15 yenye thamani ya zaidi yacmilioni 248,itakaguliwa, wakati miradi 11 yenye thamani ya zaidi ya milioni 10, itawekewa mawe ya msingi pamoja na miradi 6 yenye thamani ya milioni 25.62 itatembelewa.

Pia amesema kuwa Mkoa huo utatumia mbio za Mwenge wa Uhuru kuendelea kuhamasisha jamii ya Watanzania kuhusu mapambano dhidi ya rushwa,ugonjwa wa Ukimwi na changamoto ya dawa za Kulevya.

Vilevile amesema katika kuhakikisha Mkoa unalinda mazingira umeendelea kulinda na kusimamia misitu ya asili yenye jumla ya hekta 489,871, ambapo kati ya hiyo misitu ya Serikali Kuu ina ukubwa wa hekta 406,160.89 huku ya halmashauri ina ukubwa wa hekta 9,633.44, ya Vijiji hekta 73,763.99 na ya watu binafsi ni hekta 313.67 .

Aidha katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Michael amesema Mkoa umeendelea kutekeleza, kuratibu na kusimamia zoezi la upandaji miti katika Halmashauri na Mkoa umejiwekea lengo la kupanda miti 7,500,000 kila mwaka.

Mwenge wa uhuru utatembelea Halmashauri tano za Mkoa wa Songwe na baadae kuukabidhi mkoani Mbeya Septemba 7, 2023 katika kijiji cha kikuti wilayani Rungwe baada ya kumaliza mbio zake wilayani Ileje .