November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge kutembelea miradi 13 ya maji Tanga

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Tanga

Miradi ya maji 13 kwenye halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga inatarajiwa kutembelewa na Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya uzinduzi, kuweka jiwe la msingi na ukaguzi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Aprili 5,2024 Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo ameeleza kuwa ujenzi wa mradi wa maji Kwakibuyu uliopo Wilaya ya Pangani utazinduliwa ambao umejengwa kwa gharama ya milioni 594.2,utahudumia wananchi 5,868.

Tenki la Mradi wa Maji Kwediyamba, Halmashauri ya Mji Handeni

Pia ameeleza kuwa mradi wa maji Kwamazara, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni utazinduliwa umejengwa milioni 131.8 na ukihudumia wananchi 1,650 huku ujenzi wa mradi wa maji Magila- Gereza, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe unaojengwa kwa kiasi cha milioni 775.7 na kunufaisha wananchi 6,120, utawekewa jiwe la msingi.

“Ujenzi wa mradi wa maji Bokwa- Mafulila, Wilaya ya Kilindi utawekewa jiwe la msingi unaojengwa kwa gharama ya milioni 765.2,utanufaisha wananchi 8,883,mradi wa maji Potwe, Wilaya ya Muheza utakaogharimu kiasi cha milioni 443.7, utanufaisha wananchi 4,763, na utawekewa jiwe la msingi,”ameeleza na Mhandisi Lugongo kuongeza kuwa

“Ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji Gombero wilayani Mkinga utawekewa Jiwe la msingi ambao utagharimu kiasi cha bilioni 3.1 utahudumia wananchi 6,357,”.

Mhandisi Lugongo ameeleza kuwa mradi mwingine kwenye Wilaya ya Mkinga ni ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji Mapatano unaojengwa kwa gharama ya bilioni 1.5 huku ukihudumia wananchi 9,151 Ambapo Mwenge wa Uhuru utafanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi.

Katika Wilaya ya Lushoto, Mwenge wa Uhuru utafika kwenye mradi wa maji Magamba utafanya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo unaojengwa kwa kiasi cha bilioni 1.8 utanufaisha wananchi 31,107 wa Mji wa Lushoto na viunga vyake.

Huku Halmashauri ya Bumbuli mradi wa maji Funta utawekewa Jiwe la msingi unaojengwa kwa kiasi cha milioni 832.6 na kuhudumia wananchi 6,185.

Tenki la Mradi wa Maji Kwakibuyu, Wilaya ya Pangani

Pia amesema miradi hiyo yote ipo chini ya taasisi ya RUWASA huku mradi uliopo chini ya Tanga- UWASA ni ule wa uboreshaji huduma ya maji kwenye Jiji la Tanga ambao Mwenge wa Uhuru utafanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wake wenye gharama ya bilioni 2.3 na utahudumia wananchi 26,563.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa kwa miradi ambayo ipo chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM), Mwenge wa Uhuru utazindua uboreshaji wa miundombinu ya maji katika Mji wa Korogwe ambao utanufaisha wananchi 18,782 na umegharimu kiasi cha bilioni 1.5.

“Mradi wa maji Kwediyamba uliopo Halmashauri ya Mji Handeni utawekewa jiwe la msingi unaojengwa kwa gharama ya bilioni 1.2 utanufaisha wananchi 5,746,”.

Nyumba ya Mitambo (Pump House) Mradi wa Maji Bokwa, Wilaya ya Kilindi

Aidha ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru utatembelea mradi wa maji Majani Mapana uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambao ulizinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 uliojengwa kwa gharama ya milioni 395 utanufaisha wananchi 2,521.

Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Tanga utakimbizwa kwenye halmashauri 11 kuanzia Aprili 9 hadi 19, mwaka huu.

Tenki la Mradi wa Maji Gombero, Wilaya ya Mkinga