Na Jacline Martin,Timesmajiraonline
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeamua kuvalia nguja suala la nishati safi ya kupikia.
Lengo la hatua hiyo ya Rais Samia ni kuboresha maisha ya Watanzania hasa kinamama. Ustawi wa mwanamke wa Tanzania unahatarishwa na namna anavyotafuta nishati na aina ya nishati anayopikia.
Wataalam wanasema lisaa limoja jikoni ni sawa na sigara 300, sasa hapa unategemea ustawi utatoka wapi? Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia nane tu ya Watanzania ndio wanatumia nishati safi ya kupikia.
Kutokana na idadi hiyo kuwa ndogo Rais Samia, ameishatoa maelekezo ifikapo mwaka 3034 ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Lakini pia katika kuhakikisha hilo linafanikiwa alielekeza kuandaliwa kwa Mkakati na Mwelekeo na pia kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi.
Tayari maelekezo yake yamefanyiwa kazi, ambapo juzi tumeshuhudia akizindua Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya kupikia, Rais Samia anasema asilimia 90 ya kaya nchini zinatumia kuni na mkaa.
Anasema anafahamu athari za kudumu za matumizi ya kuni na mkaa, hivyo madhara yake ni makubwa. Anasema moja ya sababu ya kutotumia nishati safi ya kupikia ni gharama na uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo.
Anasema tatizo la matumizi ya nishati safi ya kupikia ni mtambuka linahitaji nguvu za pamoja, hivyo mkakati huo unatoa mwongozo wa kitaifa kwa wadau wote kuhakikisha nchi yetu inafikia lengo iliyojiwekea kwa asilimia 80 kwa Watanzania wanatumia nishati ya kupikia ifikapo mwaka 3034.
Rais Samia anasema sema hatua mbalimbali zimeainishwa kufikia lengo hilo. “Tukifanikiwa kufikia lengo hilo tutapunguza gharama za nishati ya kupikia, tutaongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na tutaongeza uwekezaji kwenye nishati safi.” Anasema.
Anasema mkakati huo utachangia jitihada za Serikali kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kutokana na uhalibifu wa misitu ambao uchangiwa na shughuli za kibinadamu
Anafafanua kuwa inakadiriwa hekta 469,000 za misitu zinakatwa kila mwaka nchini. Anasema nishati za kuni na mkaa ni moja ya chanzo kikuu cha upotevu wa mistu hiyo.
Kutokana na kasi kubwa ya upotevu wa mistu hiyo, hata upatikanaji wa kuni na mkaa utakuwa wa shida. Anasema jambo hilo linasababisha baadhi ya wananchi kutumia muda mwingi zaidi kutafuta nishati ya kupikia kuliko kutafuta chakula chenyewe.
Kwa mujibu wa Rais Samia mbali na athari za kimazingira, inakadiriwa kuwa Watanzania zaidi ya 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupikia, ambapo kiasi kikubwa huchangia na uvutaji wa moshi.
“Kama tunavyowekeza kuokoa maisha ya mama na mtoto, vivyo hovyo, hatuwezi kukubali kuendelea kupoteza sehemu ya nguvu yetu ya taifa hasa wanawake kwa sababu ya matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia,” anasema.
“Tutumie mkakati huu kama nyenzo muhimu kutuongoza kufikia azma hii ya kuokoa akina mama kupitia maradhi ya kupumua yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Kwa ujumla tukitafakari athari za mazingira ni wazi ukosefu wa nishati safi ya kupikia unarudisha nyuma jitihada za maendeleo katika nchi yetu.
Safari yetu ya maendeleo haiwezi kupiga hatua kubwa ikiwa asilimia 90 ya wananchi wenzetu bado wanatumia nishati isiyo rafiki,” anasema.
Anasema mkakati huo wa kitaifa ni jitihada za kuwaleta pamoja wadau wote kuangazia suala la nishati safi ya kufika. Anawataka kutambua kwamba kila mdau ana nafasi na jukumu katika kufanikisha mkakati huu.
Kwa upande wa Serikali anasema wanalo jukumu la kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu nishati safai ya kupikia na kutunga sera wezeshi kufikia mkakati huo.
Ili kufikia lengo la matumizi ya nishati safi ya kupikia, Rais Samia ametoa maagizo sita, likiwemo la kumtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuandaa katazo kwa taasisi zote zinazohudumia watu kuanzia 100 kutotumia mkaa na kuni kupikia.
Rais Samia anasisitiza kuwa baada ya miezi mitatu kutoka sasa ifikapo Agosti, mwaka huu kusiwe na taasisi inayohudumia watu kuanzia 100 inayotumia mkaa na kuni.
Maagizo mengine aliyotoa Rais Samia ni kuitaka Wizara ya Nishati ihakikishe inawafikishia mkakati huo wadau wote muhimu kwa manufaa ya wananchi na wadau kwa ujumla. Pia ametaka mkakati huo utafsiriwe kwa kiswahili na kingereza.
Aidha, Rais Samia anaitaka Wizara ya Nishati ikae na wadau wanaohusika serikalini na sekta binafsi kubaini maeneo ambayo yakifanyiwa kazi yatasaidia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa gharama himilivu.
Tatu, Rais Samia anaitaka wizara hiyo ishirikiane na wadau kuhakikisha wanakuwa na mfuko wa kuendeleza nshati safi ya kupikia ifikapo 2025. Aliitaka wizara na wadau waje na sheria itakayoanzisha mfuko huo na watajua namna ya kutafuta fedha ya kuendeleza mfuko huo.
Nne, Rais Samia anaitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI iboreshe mikataba wanayoingia na wakuu wa wilaya ilikuongeza kifungu cha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kipengele cha kupima utendaji kazi wao.
Pia anasema ni vizuri TAMISEMI iwatambua wadau wanaotekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia ili mafanikio yanayopatikana yaweze kupelekwa maeneo mengine. Alitaka sekta binafsi ifunguliwe njia.
Agizo la tano, anaitaka REA kujipanga vizuri kutekeleza majukumu yao yaliyomo kwenye Mkakati wa Taifa wa Matumizi wa Nishati Safi ya Kupikia.
Sita, anasema miezi mitatu ijayo ifikapo Agosti, Waziri Majaliwa aandae taarifa ya utekelezaji, kwani walisema taasisi zote zenye kuhudumia watu zaidi ya 100 zisitumie mkaa na kuni.
Anamuagiza Waziri Mkuu kuandaa katazo la kupiga marufuku taasisi zote zinazohudumia zaidi ya watu 100 kutumia kuni na mkaa. Alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ya lazima na sio anasa tena.
Aidha, anaagiza Wizara ya Nishati kuongoza Watanzania kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa wananchi kwa bei inayohimilika.
Aidha, anasema wanatarajia sekta binafsi kuongeza uwekezaji pamoja na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia sehemu mbalimbali nchini, lakini pia walete teknolojia rahisi inayowezesha wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao.
“Kwa mfano kulipia kadri anavyotumia kama inavyofanyika kwa umeme au maji,” anasema Rais. Anasema moja kati ya maonesho ya mazingira aliyoshiriki aliona wametengeneza mtungi ambao mtu analipa jinsi anavyolipia.
“Kuna mitungi inajazwa mtu kama ana 10,000 anatumia gesi ya elfu 10, ikimalizika mtungi unakata hata kama gesi ipo mpaka ulipe waje wakufungulie utumie tena,” amesema Rais Samia.
Anataka watu hao watafutwe au wajitokeze ili wafanye nao kazi katika eneo hilo. Aidha, aliagiza kuvutia uwekezaji kwenye uzalishaji wa majiko banifu na sanifu ya umeme na kuhamasisha uzalishaji wa vifaa na mitungi ya gesi asilia hapa hapa nchini.
Anasema hatua hizo zitakuza uwekezaji na ajira kwa vijana na zitasaidia kupunguza gharama za nishati. Alisema yapo masuala yanawataka Serikali na sekta binafsi kukaa pamoja ya kuongeza ubunifu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazochangia matumizi madogo ya nishati hiyo.
Rais Samia anasena waangalia namna wanavyoweza kuendeleza kuongeza matumizi ya nishati ya umeme kwa ajili ya kupikia. Aliwataka watu wabadilike.
Aidha, anasema sekta binafsi wana kazi ya kufanya kwa kuwezesha wadau wa sanaa kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati ya kupikia.
Ili kufanikiwa hilo, anasema wanahitaji ushirikiano wa wadau wote. Alihimiza sekta binafsi ijengewe mazingira ya kwenda hadi vijijini kwenda kupeleka vituo vya kujazia mitungi.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu IlemelaÂ
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika