June 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWAUWASA yaendelea na jitihada za kuhakikisha maji yanapatikana

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), inaendelea kutekeleza jitihada na mipango ya upatikanaji wa huduma ya maji Kata ya Lwanhima wilayani Nyamagana mkoani hapa.

Ambapo mtandao wa usambazaji maji katika Kata ya Lwanhima unaendelea kuboreshwa ili kuwezesha wananchi kunufaika na mradi wa chanzo cha maji Butimba.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),Neli Msuya,amebainisha hayo Mei 21,2024 alipotembelea Kata ya Lwanhima kwa lengo la kukagua hali ya upatikanaji wa huduma baaada ya miundombinu ya maji inayopeleka huduma ya maji katika Kata hiyo kuathiriwa na ujenzi wa barabara ya Igoma- Buhongwa.

“Nimefika hapa kukagua hali ya huduma ya maji lakini pia kuzungumza na viongozi katika Kata hii ya Lwanhima kuhusiana na hali ya upatikanaji wa huduma pamoja na jitihada na mipango inayoendelea kutekelezwa na Mamlaka,” amefafanua Neli.

Sanjari na hayo Neli amefafanua jitihada za muda mfupi,kati na za kudumu zinazotekelezwa na Mamlaka katika kuboresha huduma ya maji kwenye maeneo yanayohudumiwa na MWAUWASA.

“Katika hatua za muda mfupi mamlaka inalaza mabomba ya usambazaji maji kwa awamu katika mitaa hasa yenye changamoto ili kuboresha mfumo wa usambazaji,” amesema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Lwanhima Marko Swalala ameeleza kuwa amekuwa akishirikishwa kuhusu mipango inayohusu miradi ya maji.

“Tunakushukuru kwa ujio wako hapa, hii inaonyesha dhamira ya kipekee ya kulipatia ufumbuzi suala la changamoto ya maji katika kata yetu, huu ndio utumishi wa umma. Tunakushukuru, hakika unatupa ushirikiano,”Swalala.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Neli alitembelea na kukagua miundombinu ya kusafirisha maji iliyoathiriwa sambamba na kuzungukia mtandao mzima unaotumika kusambaza maji eneo la Kata ya Lwanhima na tenki la Sahwa ya Juu.