November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWAUWASA kutanua mtandao wa maji Nansio

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Ukerewe

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza(MWAUWASA) Neli Msuya,amesema uwezo wa mtambo wa kuzalisha maji wa Nebuye ni lita milioni 8.6 kwa siku na hivyo kinachofanyika sasa ni kutanua mtandao wa maji sambamba na kuhamasisha wananchi kujiunga na mfumo wa maji.

Neli ameyasema hayo akiwa wilayani Ukerewe mkoani Mwanza katika ziara yake ya kikazi ya kukagua ufanisi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Nebuye unaohudumia wakazi wa Mji wa Nansio,pia alipata fursa ya kumtembelea Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pius Msekwa ikiwa ni siku ya kumbukizi ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Amemueleza Msekwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wizara ya Maji kupitia MWAUWASA za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Mwanza pamoja na Mji wa Nansio.

“Tunatarajia kutanua wigo wa upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Nansio, tunatekeleza adhima ya Rais Samia kupitia Waziri wetu wa Maji Jumaa Aweso ya kumtua Mama wa Nansio ndoo ya maji kichwani,” amesema Neli.

Kwa upande wake Msekwa ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na amepongeza Serikali kwa dhamira yake ya kuboresha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Nansio.

Pia Msekwa amemzawadia Mkurugenzi huyo wa Neli nakala ya kitabu alichokisaini cha ‘Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere” cha Mwaka 2012 alichokiandika.