Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Neli Msuya ametembelea na kukagua mitambo midogo ya kusukuma maji ya Igombe na Kayenze ili kujiridhisha na ufanisi wake.
Pamoja na kutazama namna bora ya kuendelea kuimarisha utendaji wake ili kupanua wigo wa huduma kupitia mitambo hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya maji.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Septemba 1, 2023, Mkurugenzi huyo aliambatana na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa MWAUWASA, Mhandisi, Robert Lupoja, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga.
Lengo ni kushirikisha na wadau hao ikiwemo RUWASA ili kubadilishana uzoefu na kuona namna bora ya kuimarisha upatikanaji wa maji hususani maeneo ya pembezoni mwa Wilaya ya Ilemela.
“Tunahitaji kushirikiana kwa karibu na wenzetu wa RUWASA na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kuhakikisha huduma kwenye maeneo yetu inaimarika, sote ni watoto wa baba mmoja yaani Wizara ya Maji na dhamira yetu ni moja nayo ni kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji,” amesema Neli.
Amesema ziara hiyo mbali na ukaguzi wa mitambo midogo ya maji ya Igombe na Kayenze lakini pia imelenga kuainisha maeneo ambayo MWAUWASA inaweza kushirikiana na RUWASA kupata ufumbuzi wa kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji pamoja na kutanua wigo wa usambazaji wa maji kwenye maeneo yenye changamoto.
Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wasimamizi wa mitambo hiyo kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa maeneo wanayohudumia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na ratiba maalum ya matengenezo zuifu (preventive maintanance) ili kuepuka athari inayoweza kujitokeza endapo mitambo itapata hitilafu.
Kwa upande wake Mhandisi Godfrey Sanga amemuhakikishia ushirikiano huku akithibitisha utayari wa RUWASA katika kuhakikisha inafanya kazi kwa karibu na MWAUWASA ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kumtua mama ndoo ya kichwani.
Ziara hii inafuatia mpango mkakati aliyojiwekea Mkurugenzi Neli wa kuimarisha huduma ya maji jijini Mwanza kwa kushirikiana na wadau zikiwemo taasisi mbalimbali za Serikali.
Kwa sasa mitambo hiyo ya Igombe na Kayenze inahudumia wateja 623 kutoka maeneo ya Kabangaja, Igombe, Shibula, Igogwe, Mwakarundi, Masemele, Kabusungu, Semba A na B, Muuhonze A na B, Kayenze, Lutongo, Iponyabugali, Kayenze ng’ambo, Sangabuye, ilekako, Nyafla na Igalagala.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua