Judith Ferdinand
Leo Oktoba 14,2023 tunakumbuka kifo cha Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa awamu ya Kwanza wa Tanganyika kwa sasa ni Tanzania ambaye alifariki Oktoba 14,1999.
Ikiwa ni mwaka wa 24 sasa tangu alipo fariki ambapo miongoni na vitu alivyokuwa akisisitiza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika hotuba zake mbalimbali ni pamoja na falsafa yake ya kupiga vita adui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini ambavyo vyote hivyo vikifanyika taifa hili litakuwa miongoni mwa nchi itakayoendela zaidi duniani.
Hata hivyo mpaka sasa bado maono na falsafa zake za kuhakikisha nchi ya Tanzania inafika mbali kimaendeleo zinaendelea kuishi kwani taasisi mbalimbali,viongozi wanaoendelea kumuenzi kwa vitendo.
Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), imekuwa ikimuenzi Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa vitendo kupitia falsafa yake ya kupiga vita adui umasikini,ujinga na maradhi.
Falsafa ya kupiga vita Maradhi
Akizungumza na Majira Oktoba 11,2023 Makao Makuu ya MWAUWASA Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa mamlaka hiyo Mhandisi Robert Lupoja anaeleza kuwa wamekuwa wanaenzi falsafa ya kupiga vita maradhi(magonjwa) moja kwa moja.
Mhandisi Lupoja anaeleza kuwa katika huduma yao ya huduma ya maji safi na usafi wa mazingira utagundua moja kwa moja kwamba wanatekeleza na kuenzi falsafa ya Mwalimu Nyerere katika masuala ya kupiga vita maradhi.
“Unapozungumzia maji safi ni maji ya kunywa ambayo ukiyanywa hayajatibiwa vizuri basi utapata maradhi,ukikosa maji ya kusafisha mwili unapata maradhi vilevile ata baada ya maji kutumika yanatakiwa kuhakikisha tunayakusanya na kurudishwa katika hali ya usafi ambapo tunayatibu na kuyarudisha kwenye mazingira yakiwa safi,”anaeleza Mhandisi Lupoja.
Anaeleza kuwa MWAUWASA kwa suala la maradhi kwa falsafa ya Mwalimu Nyerere wanaitekeleza kikamilifu kwani wanao mtambo mkubwa ambao unatibu maji wa chanzo cha maji Capripoint chenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 90 kwa siku.
“Tunaposema mtambo unazalisha,unatibu maji kisha tunasambaza katika mitandao ya mabomba na kufikia wateja wetu,hivi karibuni tunaenda kupokea mradi mpya wa chanzo cha maji Butimba ambacho kimejengwa na serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ambacho kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku unaogharimu takribani bilioni 70,”anaeleza Mhandisi Lupoja.
Pia anaeleza kuwa chanzo cha maji Butimba kina eneo la chujio kwa maana ya tiba wamekiboresha zaidi kuliko cha Capripoint ambacho kina uwezo mkubwa wa kutibu maji kabla ya kumfikia mtumiaji na kuzalisha maji ya kunywa moja kwa moja watakuwa wamelenga falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kupiga vita maradhi.
“Kitakapo kamilika kwa sasa tunajua Jiji la Mwanza Lina upungufu wa maji wa lita milioni 70 kwa siku kwani uhitaji ni lita mlioini 160 huku chanzo cha Capripoint kinauwezo wa kuzalisha lita za maji milioni 90 tu kwa siku, tunaishukuru serikali kuwekeza na kujenga chanzo hicho itasaidia kupunguza changamoto ya watu kupata maji kwa mgao na wengine kukosa kabisa tutakuwa tumeboresha huduma ya maji safi hivyo kusaidia wananchi kuepuka magonjwa,”.
Aidha anaeleza kuwa kwa upande wa maji taka MWAUWASA inaenzi falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kupiga vita maradhi kwa kuhakikisha kuwa maji taka yanayozalishwa yanatibiwa na baadae yanaachiwa kwenda katika mazingira yakiwa katika hali nzuri.
“Tunayo mabwawa makubwa Butuja ambayo yanauwezo wa kusafisha maji taka yanayozalishwa na wakazi wa Jiji la Mwanza katika kiwango kinachokubalika kwa kurudisha ziwani pia yanatumika kwa mfumo wa maji taka kwa maana ya mtandao mbao umesambaa jijini hapa kwa zaidi asilimia 20 sasa,”anaeleza Mhandisi Lupoja na kuongeza kuwa
“Tunatumia magari ya maji taka kunyonya maji taka kwenye nyumba kwa watu ambao hawana mfumo wa maji taka ambapo tuna jumla ya magari manne ambayo yanafanywa shughuli hizo tumewahusisha magari binafsi katika kuondoa maji taka nyumbani,”.
Pia anaeleza kuwa wamejenga vyoo katika shule mbalimbali jijini Mwanza kwa maana ya Wilaya ya Ilemela na Nyamagana ambapo inawasaidia kujikinga na maradhi kwa sababu wamekuwa na maeneo maalumu za kukidhi haja zao pamoja na maeneo yanayotoa huduma kama zahanati,stendi na sokoni.
Ambapo wamefanikiwa kujenga vyoo 12 katika zahanati zilizopo jijini Mwanza kati ya hivyo vyoo 6 vimejengwa Wilaya ya Ilemela na 6 Wilaya ya Nyamagana huku jumla ya vyoo 5 wamejengewa katika masoko katika ya vyoo hivyo 3 vimejengwa Wilaya ya Nyamagana na 2 Wilaya ya Ilemela.
Aidha anaeleza kuwa wamekuwa wakiwajali watu wa maeneo ya milimani kwa kujenga mtandao wa maji taka na kuwaunganishia huduma hiyo.
“Maeneo hayo yalikuwa changamoto katika kutiririsha maji taka ambayo ni hatari kwa afya ,sisi MWAUWASA tumejaribu kuweka mfumo wa maji taka ambayo inaitwa mifumo rahisishwa kwenye maeneo ya milimani,na Jiji hili lina maeneo hayo ambayo yana milima yenye miamba na mawe na upitishaji wa mabomba ni changamoto ila tumeweza,”anaeleza Mhandisi Lupoja.
Vilevile anaeleza kuwa wanetekeleza mradi huo wa kuweka mfumo wa maji taka katika maeneo mbalimbali ya Jiji hilo ambapo jumla ya Kata 3,697 zimenufaika na mradi ambao unatekelezwa mpaka sasa kwa awamu tatu ikiwemo ya majaribio,awamu ya kwanza na awamu ya pili.
Awamu ya majaribio mradi ulifikia kaya 2,808 kati ya hizo Kilimahewa ni kaya 702,Mabatini 1068 na Igogo 720.
Huku awamu ya kwanza walifikia kaya 1072, kati yao Ibungiro 280,Isamilo 205,Igogo-Sahara 393 na Kabuhoro 194.
Na awamu ya pili umefikia kaya 817 ambapo kati ya hizo Pasiansi Kata 200, Kilimahewa ‘A’296, Kilimahewa ‘B’ 63 na Mabatini 256.
“Miradi hii ya kuondosha maji taka maeneo ya milimani tulipata fedha kupitia wahisani mbalimbali na tulianza majaribio mwaka 2016/2017 na sasa tunaendelea kupanua zaidi katika maeneo hayo na tutaendelea kuboresha huduma ya maji safi, uondoshaji maji taka pamoja na kuyatibu kwani ipo mipango mbalimbali kwani tunafahamu kuwa Jiji la Mwanza lina upungufu wa maji,”anaeleza Mhandisi Lupoja.
Pia anaeleza kuwa wanaendelea na miradi mbalimbali ya kufanya upanuzi wa mitandao ya mabomba katika maeneo ya Buswelu,Nyamadoke,Kahama na baadhi ya maeneo ya Kisesa na Luchelele baada ya mradi kukamilika
“Tumeomba wizarani kiasi cha bilioni 4.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya matokeo ya haraka mara mradi wa chanzo cha maji Butimba kukamilika basi wananchi waanze kupata maji, ambapo tutatandaza mabomba zaidi ya km 42 katika maeneo ya Buswelu, Kahama,Nyamadoke na Ilalila,”.
Pia wataweka kilomita 6.9 mtandao wa bomba Luchelele na kilomita 3.5 Buswelu na bomba kubwa zaidi kwa Oktoba na Novemba watakuwa wamekamilisha mradi huo na watu wataanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama.
Falsafa ya kupiga vita ujinga
Sanjari na hayo anaeleza kuwa MWAUWASA imeenda mbali zaidi kwa kujenga vyoo katika shule mbalimbali jijini Mwanza kwa maana ya Wilaya ya Ilemela na Nyamagana hii yote ni kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi kupata elimu ikiwa ni kuenzi falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kupiga vita adui ujinga.
Anaeleza kuwa vyoo hivyo vinawasaidia wanafunzi kuweza kusoma na kupinga na ujinga kwa kupata elimu bora katika mazingira salama.
Ambapo anaeleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanza kwa mradi wa ujunzi vyoo shuleni na maeneo ya wazi wameisha Jenga vyoo zaidi ya 50 katika shule za Wilaya hizo.
Mhandisi Lupoja anaeleza kuwa katika shule zilizopo Wilaya ya Ilemela wamajenga jumla ya vyoo 43 huku Wilaya ya Nyamagana vyoo 44.
Falsafa ya kupiga vita umasikini
Mhandisi Lupoja anaeleza kuwa wanapo boresha huduma ya maji safi na salama moja kwa moja suala la umasikini wanakuwa wamelipinga kwa sababu mtu asipotumia maji safi atapa maradhi hivyo atatumia fedha kujitibu.
Kwa namna moja au nyingine tunapunguza suala la umasikini kwani unapomsogezea huduma ya maji mwananchi anaunganisha kwa umbali mrefu maji yanafika kwake inasaidia kupunguza muda wa kwenda mbali kutafuta maji na badala yake muda huo atatumia katika shughuli za kujiingizia kipato.
“Kwa namna hiyo naweza kuzungumzia kuwa kupitia huduma ya maji safi tunaepusha magonjwa na kumsaidia mwananchi gharama ambazo angetumia kujitibu akatumia katika masuala ya maendeleo na muda ambao angetumia kutafuta maji atatumia kufanya shughuli za maendeleo,”anaeleza Mhandisi Lupoja.
Mbali na hivyo pia anaeleza kuwa kupitia miradi ya maji inayotekelezwa mbali na wataalamu wa mamlaka hiyo na Wizara ya Maji pia inatoka fursa za ajira kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo hivyo kuondoa umasikini.
Pia inatoka ajira kwa vijana na wananchi wa eneo husika na maeneo mengine ya kufanya vibarua katika miradi hiyo pamoja na kuwezesha jamii inayozunguka kupata kipato kupitia biashara wanaofanya wakati mradi ukitekelezwa ikiwemo mama lishe.
Aidha pia kupitia maji hayo kuna watu wanajiingizia kipato kwa kufanya biashara ya kuwauzia maji wananchi ambao bado maeneo yao hayajafikiwa na huduma.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani