Na Esther Macha,Timesmajiraonline
WATAALAMU wa Maendeleo wanasema silaha kubwa ya kumkomboa mtoto na jamii kwa ujumla ni elimu, kauli inayoungwa mkono na maandiko yanayosisitiza kuwa watu wengi huangamia kwa kukosa maarifa.
Ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa nguvu kubwa katika sekta ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora bila ubaguzi.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo za Serikali, changamoto bado zinaendelea kujitokeza, hususan kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu hivyo hali hiyo imemfanya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) kupitia Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, kujitokeza na kuchukua hatua za ziada kusaidia watoto wahitaji.
Akizungumza kuhusu jitihada zake, Mwaselela amesema licha ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali, idadi ya watoto na wanafunzi wenye mahitaji maalumu inaendelea kuongezeka, hivyo kuhitaji mchango wa wadau wengine.
“Binafsi nimeanza kuwekeza kwenye elimu ya watoto tangu mwaka 2010, nikianza na kuboresha miundombinu ya elimu. Mpaka sasa nimegusa karibu kila eneo la elimu Mkoa mzima wa Mbeya.
“Lakini ukiwa kwenye majukumu haya, hukosi kukutana na watoto wenye uhitaji mkubwa wanaohitaji kusaidiwa ili wapate elimu,” anasema Mwaselela.
Ameeleza kuwa mwaka 2024 alichukua zaidi ya watoto 25 kutoka vijiji na kata mbalimbali za Mkoa wa Mbeya na kuwasomesha kupitia Shule ya Patrick Mission, ambapo kwa sasa wanaendelea na masomo ya Kidato cha Tatu.
“Tulipowakuta watoto hawa walikuwa wanaishi na bibi zao vijijini. Hadi leo siwezi kujua wangekuwa katika hali gani kama tusingewachukua,” anasema.
Mwaselela anasema kwake kusaidia watoto si jambo la muda mfupi bali ni dhamira ya kweli ya maisha yake ambayo amejiwekea
“Nimechagua hili kama ibada na pia kama eneo la kazi yangu hadi uzeeni. Ninaamini ukimsaidia mtoto kupata elimu, unakuwa umesaidia taifa kwa kiwango kikubwa.
Ndiyo maana nimejikita pia kwenye miundombinu, samani za shule na uwezeshaji wa kuinua matokeo ya wanafunzi,” amesema .
Madarasa ya Mitihani kupewa Kipaumbele
Akizungumzia madarasa ya mitihani, Mwaselela amesema amefanya mazungumzo na halmashauri zote, wakuu wa wilaya na wenyeviti wa halmashauri Mkoa wa Mbeya, akisisitiza umuhimu wa kuyaimarisha madarasa ya mitihani ili wanafunzi wanufaike na ruzuku ya Serikali na kufikia elimu ya juu.
“Hili linahitaji umakini, msimamo na uwazi. Wakati mwingine si rahisi kuzungumza lugha moja na kila mtu, lakini kama kiongozi wa Taifa, nina wajibu wa kuchukua hatua pale ninapoona naweza kusaidia,” amesema.
Amefafanua kuwa nafasi yake kama MNEC inampa mamlaka ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua, bila kusubiri kila jambo lifikishwe ngazi za juu za uongozi wa chama.
Meza na Viti 200 Malama Sekondari
Kuhusu msaada wa meza 200 na viti 200 alivyotoa katika Shule ya Sekondari Malama, Mwaselela amesema msaada huo umeokoa zaidi ya wanafunzi 200 waliokuwa wakikaa chini kutokana na upungufu wa samani.
“Tatizo bado lipo kwa sababu idadi ya wanafunzi inaongezeka kila mwaka, lakini hatua tuliyochukua imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto iliyokuwepo,” amesema.
Kusomesha Watoto Wenye Mazingira Magumu
Mwaselela amesema kupitia Patrick Mission, mwaka huu wamechukua watoto 25 wenye mazingira magumu kutoka maeneo mbalimbali na kuwapa elimu bure, mahitaji yote yakigharamiwa hadi wanapomaliza masomo yao.
“Kila mwaka tumekuwa tukichukua watoto wasiopungua 20,tumefikisha watoto 700,ambao tunasomesha na tumekuwa tukitumia fedha nyingi, lakini hii ni ibada tuliyoichagua. Miradi yetu haijawahi kusimama, bali imeendelea kukua zaidi na zaidi ” amesema.
Ameongeza kuwa lengo la kupanua miradi hiyo si kutafuta utajiri bali kuwafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nsalala, Festo Sanga, amesema Mwaselela ni zao halisi la uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akimtaja kama kiongozi anayeelewa kwa vitendo changamoto za wananchi wa kawaida.
“Ni kiongozi anayetoka katika familia ya kawaida, anayezijua shida za watu wa chini. Ametatua changamoto kubwa sana, ikiwemo kuwapunguzia wazazi mzigo wa michango ya madawati,” amesema Sanga.
Kwa ujumla, MNEC Ndele Mwaselela, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shule za Paradise Mission na Patrick Mission, ameendelea kuwa nguzo muhimu katika kuinua sekta ya elimu Mkoa wa Mbeya kwa kujenga miundombinu, kununua samani na kusomesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi