December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanamke matatani kwa tuhuma za wizi wa mtoto

Na.Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

MWANAMKE mmoja Prisca Clement (25), mkazi wa Buhingo wilayani Misungwi , anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,akituhumiwa kuiba mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi tisa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema kuwa Prisca, alikamatwa Julai 25, mwaka huu, majira ya saa 1:30 jioni huko katika Kijiji cha Ntundu, Kata ya Busangi katika Halamshauri ya Msalala,mkoani Shinyanga.

Amesema Prisca anadaiwa kumwiba mtoto huyo Julai 10,mwaka huu, huko Visiwani Zanzibar baada ya mzazi wa mtoto huyo kumwachia amsaidie kumwangalia wakati akienda katika majukumu mengine ambapo alipata fursa ya kutoweka naye hadi Mwanza na baadaye Shinyanga alipokamatwa na Jeshi la Polisi.

Mutafungwa amesema baada ya mtuhumiwa kufika Mwanza,alimpeleka kumficha mtoto huyo nyumbani kwa mama yake mzazi Maria Furaha, katika Kijiji cha Buhingo,Kata ya Inonelwa wilayani Misungwi,ambako alikutwa na kutambuliwa kuwa ndiye aliyeibwa Visiwani Zanzibar.

Amesema katika mahojiano Prisca alidai kuwa alifanya uhalifu huo wa kumwiba mtoto huyo kwa nia ya kumuza na kujipatia fedha.

Kamanda huyo wa polisi alieleza kuwa walipata taarifa kutoka kwa wazazi wa mtoto huyo kuwa ameibwa na mwizi amekimbilia mikoa ya Kanda ya Ziwa na mara moja walianza kufuatilia na kufanikiwa kumpata.

Aidha jeshi hilo tayari limewasiliana na wazazi wa mtoto huyo ambao watakabidhiwa baada ya kukamilisha taratibu za kisheria huku mtuhumiwa akitarajiwa kusafirishwa hadi Zanzibar alikofanya uhalifu huo ili akakabiliane na mkono wa sheria.