July 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo wa muundo wa vinasaba (DNA)

Mwanamke kukata rufaa kupinga majibu ya DNA

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MWANAMKE mkazi wa Mji Mdogo wa Kagongwa, wilayani Kahama mkoani Shinyanga (Jina limehifadhiwa) anatarajia kukata rufaa kupinga majibu DNA yaliyotolewa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Mwanza ambayo yanaonesha mtoto wake sio wa baba ambaye anadai kuzaa naye.

Mwanamke huyo alitangaza uamuzi huo wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Shinyanga. Alisema hakubaliani na majibu hayo, hivyo tayari amewasiliana na Ofisa Ustawi wa Jamii na kumuelekeza kwamba iwapo anataka kurejea kupimwa upya kwa DNA, itabidi aende Nairobi au Afrika Kusini, lakini hana uwezo wa kufika huko.

Kutokana na ugumu huo, mwanamke huyo alisema anakusudia kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kuomba msaada ili aweze kukata rufaa kupinga matokeo ya vipimo vya DNA, kwani yanaonekana kuchezewa.

Uamuzi huo wa mwanamke huyo unakuja ikiwa ni takribani siku tatu baada ya vipimo vya Maabara Kuu ya Taifa kuonesha sampuli za fenesi, papai na mbuzi zilizopimwa na maabara hiyo zina maambukizi ya Corona.

Mwanamke huyo alidai hakubaliani na matokeo hayo kuonesha mtoto aliyenaye si wa mzazi mwenzie kwani amekuwa naye katika mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi kirefu. Mwanamke huyo alidai mwanamume huyo anataka kukwepa jukumu la malezi ya mtoto.

“Hivi sasa nakusudia kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kuomba msaada niweze kukata rufaa ya kurudiwa kwa vipimo vya DNA,” alisema.

Akifafanua zaidi alisema kwa kipindi kirefu alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume huyo ambaye ni mfanyakazi wa Halmashauri ya Msalala akifundisha Shule ya Msingi Mwalugulu Kata ya Mwakata wilayani Kahama (jina limehifadhiwa).

Alisema katika mahusiano yao walibahatika kupata mtoto mmoja wa kike ambaye kwa sasa ana miaka miwili.

Hata hivyo alidai baada ya kujifungua mtoto huyo mahusiano kati yake na mzazi mwenzake yalianza kufifia kiasi cha kutopewa fedha za matunzo ya mtoto.

Aliendelea kudai kuwa yeye binafsi alipata taarifa kutoka kwa baadhi ya watumishi wenzake na mwalimu huyo kwamba anadai mtoto huyo si wake, hali ambayo huenda ilitokana na hofu ya kuharibu ndoa yake kwa vile mwalimu ana mke wake wa ndoa.

“Nilipopata fununu hizo ilibidi niende kulalamika kwa mwajiri wake na Desemba mwaka jana nilipigiwa simu na Mkuu wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii akisema anatakiwa akapime vipimo vya DNA baada ya mzazi mwenzeka kukataa mtoto wake,”alisema.

“Nilifuata maelekezo kama nilivyoelekezwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kahama, ambaye alinitaka mimi na mzazi mwenzangu twende Bugando tukiongozana na mmoja wa maofisa kutoka katika ofisi yake ili tukapate ukweli wa mtoto huyo kama ni wa huyo mwalimu,” alieleza.

Alisema siku ya safari ya kwenda Bugando ofisa ustawi aliyetakiwa kuongozana nao alimfuata peke yake akidai mzazi mwenzake ameishatangulia Mwanza watamkuta huko huko.

Alisema hatua hiyo ilimpa shaka. “Tulipofika Bugando taratibu zote za uchukuaji vipimo kati yangu, mzazi mwenzangu na mtoto zilifanyika nikaambiwa majibu yatatoka baada ya miezi miwili.

Baada ya miezi miwili nilifuatilia majibu ya DNA kwenye Ofisi za Ustawi wa Jamii nikaelezwa majibu yaliisha toka tangu Januari 9, mwaka huu, hivyo mwenzangu alipigiwa simu akaenda Ofisi za Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kusomewa majibu bila mimi kuwepo,” alidai.

Hata hivyo alisema majibu aliyosomewa yalionesha mtoto aliyezaa si mtoto wa yule mwalimu na kwamba anatakiwa akabadilishe ubini wa mtoto huyo, kwa vile ubini wa awali si wa baba halisi kitu ambacho kilimshangaza.

Aliongeza kwamba alipoomba apatiwe nakala ya majibu, alinyimwa na kutakiwa kwanza kuandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri Kahama Mji ambaye ndiye aliyepatiwa majibu yale na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

“Nilifanya kama nilivyoelekezwa lakini hata hivyo nilitakiwa nikamuone mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala ambaye ndiye mwajiri wa mzazi mwenzangu lengo langu ilikuwa kuelezea jinsi shauri langu lilivyoshughulikiwa, maana niliona kuna mbinu chafu zimetumika,”alisema

“Mzazi mwenzangu aliitwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala bila ya mimi kushirikishwa, hivyo sielewi mambo gani aliyoelezwa, lakini bado ninathibitisha mtoto niliyenaye ni mtoto halali wa huyo mwalimu, isipokuwa pamefanyika mchezo wa kuchezea majibu ya DNA,” alidai mwanamke huyo.

Kutokana na hali hiyo mwanamke huyo anakusudia kuomba msaada wa kurudiwa kupimwa upya chini ya uangalizi wa watu maalumu na lengo lake ni kuhakikisha mtoto wake aliyejifungua kwa njia ya upasuaji asikose baba wa kumlea.

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji Kahama, Abdukarim Nuru alikiri kuwa mwanamke huyo kufikisha malalamiko hayo na tayari yamefanyiwa kazi ingawa hakutaka kuzungumzia kwa kina jambo hilo kwa kuwa yeye si mseamaji wa halamshauri