May 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanamitindo Millen Magese apewa kibali kuandaa Miss Universe Tanzania 2025

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

BARAZA la Sanaa la Taifa(BASATA) limetoa baraka na kibali kwa Mwanamitindo wa Kimataifa na Mrembo wa Tanzania, Millen Happiness Magese, kupitia kampuni yake ya MILLEN PRIVÉ & Co. LIFESTYLE Bespoke Luxury Lifestyle & Hospitality Management kuandaa mashindano ya Miss Universe Tanzania.

Millen amepata baraka na kibali cha kuandaa Miss Universe Tanzania jijini Dar es Salaam, ambapo wadau wa tasnia ya ulimbwende akiwemo Miss Universe mwaka 2024, Judith Ngussa wameahidi kutoa kila aina ya ushirikiano kwa Millen kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana, amesema baraza hilo kama walezi na wasimamizi wa karibu wa tasnia ya urembo,ulimbwende na utanashati wameamua kumpa baraka zote Millen Happiness Magese kuandaa mashindano hayo nchini.

“Tunajivunia na wale wanaofuatilia Millen Happiness Magese yuko nje ya nchi anakaa Marekani, lakini bado moyo wake unasema kwanini asirudi nyumbani afanye jambo kwa maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania, lakini pia kwa maendeleo na ustawi wa Baraza la Sanaa la Taifa.

“Hivyo tunamtakia kila la heri na tunategemeo mambo yetu yatakuwa mazuri kwamba kazi hii Millen unaiweza lakini na sisi kama Tanzania tutafurahi kuona mashindano ya ulimbwende Miss Universe tuna Mwakilishi kutoka Tanzania,”amesema Dk.Mapana.

Aidha amesema mashindano ya Miss Universe yana mambo mengi na ndio maana mbali ya kumpatia baraka na kibali cha kuandaa mashindano hayo wamemkabidhi muongozo wa maadili katika kazi za sanaa na kusisitiza wanapofanya mashindano ya ulimbwende wasisahau kuna mila na desturi zetu.

Mwanamitindo wa Kimataifa na Mrembo wa Tanzania Millen Happiness Magese (kushoto) akizungumza katika Ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha kukabidhiwa kibali cha kuandaa Miss Universe Tanzania .Katikati ni Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dkt. Kedmon Mapana na kulia ni Miss Universe mwaka 2024 Judith Ngussa.

“Tuhakikishe kwamba kama Tanzania tunapokwenda huko nje tunasema huyu mrembo anatoka Tanzania na anapambanua vipi hasa suala la maadili , hivyo tunatarajia muongozo huu ambao tumekukabidhi Millen utautumia vizuri na sisi BASATA tutahakikisha jambo hili linakwenda kutekelezeka vizuri.

Kwa upande wake Millen Happiness Magese ameishukuru BASATA kumpatia baraka na kibali cha kuandaa mashindano ya Miss Universe Tanzania yeye kupitia kampuni yake kuratibu.

“Nashukuru kwa kupata kibali cha Miss Universe Tanzania kutoka Miss Universe Organization na kwa sasa pia nimepata kibali cha hapa Tanzania kupitia BASATA ,Kwahiyo nina baraka zote mbili.Kwa kushirikiana na BASATA na wadau wote nchini tunategemea safari hii itakuwa ni suala nzima la kunyanyua hii Sanaa nzima ya mambo ya ulimwende Tanzania.

“Nawashukuru kwa kutupa nafasi hii ,kwetu ni nafasi muhimu kwani tutatumia platform hii ya Miss Universe kuitangaza nchi yetu kwani watu zaidi ya bilioni moja kwa wakati mmoja hufuatilia na nchi zaidi ya 174 zimekuwa zikishiriki mashindano haya,”amesema Millen.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA)Dk.Kedmon Mapana(katikati) akimkabidhi muongozo katika sanaa Mwanamitindo wa Kimataifa na Mrembo wa Tanzania Millen Happiness Magese baada ya kumpa kibali cha kuandaa mashindano ya Miss Universe Tanzania.Aliyekaa kulia ni Miss Universe 2025 Judith Ngussa.

Amesisitiza ulimbwende bado una nafasi kubwa sana na ndio jukwaa ambalo linaweza kukutangaza kwa ukubwa nje ya nchi huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza Miss Universe Tanzania mwaka 2024 Judith Ngussa na kuahidi kushirikiana naye katika mashindano hayo kwani tayari yeye anauzoefu maana alishafika Miss Universe World.

“Tunamkaribisha Miss Universe mwaka 2024 Judith Ngussa kuungana nasi na kufanya kazi Kazi na sisi tunafahamu yeye anafahamu zaidi mashindano haya na wasichana wengi wanamungalia na wanapenda kumuona katika safari hii nzima ya kumtafuta mlimbwende wa mwaka huu wa 2025 na hata kama ikiwezekana basi Judith aweze kumsaidia kumuongoza.

Awali Miss Universe 2024,Judith Ngussa amesema amefurahi kwa Millen Magese kupewa leseni ya kuandaa mashindano ya Miss Universe mwaka 2025 na kusisitiza yuko tayari kumuunga mkono katika kufanikisha mashindano hayo.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)Dk.Kedmon Mapana akizungumza wakati wa kutoa kibali kwa Mwanamitindo wa Kimataifa na Mrembo wa Tanzania Millen Happiness Magese (kushoto) kuandaa mashindano ya Miss Universe nchini Tanzania .Kulia ni Miss Universe Tanzania Judith Ngussa.

“Nawashuku BASATA kwa msaada na ushirikiano ambao wanatupatia katika tasnia ya ulimbwende na tunafurahi kufanya kazi na nyie na kwenye shindano la Miss Universe Tanzania nimefurahi kuona dada Millen kuwa mmiliki wa leseni hii na pia kuwa muandaaji wa shindano hili 2025.”

Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba Millen Magese ndiyo National Director na mmiliki wa Leseni ya kuandaa Miss Universe Tanzania 2025.