January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanamitindo akabidhiwa Mil. 3 Samia Fashion Festival

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

MWANAMITINDO wa Kimataifa Millen Happiness Magese amekabidhi kitita cha Sh.milioni tatu kwa Mwanamitindo Elizabeth Masuka aliyeibuka mshindi wa Samia Fashion Festival Zanzibar mwaka 2024.

Millen Happiness Magese aliyekuwa Jaji Mkuu wa Samia Fashion Festival Zanzibar alikabidhi hundi ya fedha yenye thamani ya Sh.milioni tatu katika Hoteli ya Urban by City Blue iliyopo Jijini Dar es Salaam ambapo alimuandalia chakula cha usiku mwanamitindo huyo na fedha hizo zimetoka Kampuni ya Millen PRIVE $ Co kupitia Millen PRIVE Lifestyle ambayo yeye ndio Mkurugenzi Mkuu.

Taarifa ya Mwanamitindo huyo Mtanzania anayeishi nchini Marekani aliyoitoa kwa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam amesema kuwa katika tamasha la Samia Fashion Festival Zanzibar yeye alikuwa Jaji Mkuu hivyo pamoja na kutangaza washindi wa tamasha hilo, aliona umuhimu wa kuitambua kazi kubwa iliyofanywa na wanamitindo walishiriki usiku huo na kumtangaza Elizabeth Masuka kuwa Mwanamitindo bora wa tamasha hilo.

“Tunafahamu kulikuwa na Samia Fashion Festival Zanzibar ambalo liliandaliwa na dada yangu Khadija Mwanamboka na katika tukio hilo nilikuwa Jaji Mkuu ,hivyo baada
ya kutangaza washindi niliona umuhimu wa kuitambua kazi kubwa iliyofanywa na wanamitindo walishiriki usiku huo na kumtangaza Elizabeth Masuka kuwa Mwanamitindo bora wa Samia Fashion Festival Zanzibar mwaka 2024.

“Nimetoa fedha hizo Sh.milion tatu kwanza kwa kutambua mchango wa wanamitindo wote ambao wamefanya kazi kubwa na nzuri wakati wa tamasha hilo lakini fedha hizo ni katika kuwatia moyo wanamitindo wanaochipukia katika medani za Wanamitido na tatu nimetoa fedha hizo Sh.milioni tatu kwa Elizabeth Masuka kwa kutambua yeye ndio Mwanamitindo bora wa Samia Fashion Festival Zanzibar mwaka 2024.,amesisitiza Millen Happiness Magese.

Ameongeza kuwa amefurahishwa kufanyika kwa Samia Fashion Festival Zanzibar kwani limethibitisha nafasi na umuhimu wa wanamitindo nchini Tanzania lakini pia kutoa nafasi ya vijana wa Kitanzania kuonesha uwezo wao katika kutawala Jukwaa la wanamitindo.

Ametumia nafasi hiyo kukumbusha kuwa ni heshima kubwa kwake kuwa Jaji Mkuu wa Samia wa Fashion Festival na anajivunia kushuhudia wanamitindo wote walioshiriki na kuonesha uwezo wao huku akisisitiza kwa zaidi ya miaka ishirini amejitolea maisha yake katika sekta ya mitindo, urembo.

Amefafanua ameona jinsi mitindo inavyothaminiwa katika nchi za Ulaya na mataifa mengine, si tu kama sanaa bali kama alama ya utambulisho, urithi, na fahari.Ametoa rai kwa Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau pamoja na Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuinua na kuendeleza sekta ya utamaduni,mitindo na urembo.

Kwa upande wake mwanamitindo Elizabeth amesema kukutana kwa mara ya kwanza na Millen ilikuwa ni ndoto iliyotimia na amefurahi kumuona ana kwa ana na kwa jinsi alivyo na mafanikio.

“Nimejifuza kitu kipya kutoka kwake, zawadi ambayo alinipa ilikuwa furaha yangu ya pili baada ya kazi nzuri ambayo imefanyika, namshuru sana na kumuombea Mungu aendelee kumuweka kwa ajili yetu, ni mtu mwema sana, kutoka kwake niliona mtu ambaye anataka kuona wanamitindo wengine nchini Tanzania wakifanikiwa.”

Mwisho