January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mshindi wa Gari aina ya Fortuner kwenye Promosheni ya Kampeni ya Bonge la Mpango, Abdallah Mohmed Abdalla iliyokuwa inaendeshwa na Benki ya NMB akikabidhiwa mfano wa Funguo na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa ndani (Acting Chief Internal Audit), Benedicto Baragomwa katika hafla ya kukabidhi zawadi ya mshindi wa jumla wa promosheni ya Binge la Mpango iliyofanyika mkoani Morogoro. wa kwanza kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Mashariki, Dismas Prosper na Meneja Mwandamizi wa Idara ya Wateja Binafsi – Isaac Mgwasa.

Mwanakijiji ashinda gari Benki ya NMB

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Morogoro

PROMOSHENI ya Benki ya NMB ya “Bonge la Mpango” imemalizika rasmi Jumatano wiki hii kwa mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Bw Abdallah Mohammed, kukabidhiwa zawadi nono ya gari la kifahari aliloshinda lenye thamani ya TZS million 169.

Mkazi wa mkoani Morogoro katika Kijiji cha Kinore, Abdallah Mohmed Abdallah akionyesha mfano wa Funguo wa Gari aina ya Fortuner aliyojishindia kwenye Promosheni ya Bonge la Mpango iliyokuwa inaendesha na Benki ya NMB baada ya kukabidhiwa rasmi gari yake na Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa ndani (Acting Chief Internal Audit), Benedicto Baragomwa wakati wa hafla iliyofanyika mkoani Morogoro

Gari hilo aina ya Toyota Fortuner alilolinyakua mshindi huyo kutoka kijiji cha Kinole ni jpya kabisa ambalo lilianza kutembea kilomita zake za kwanza jana baada ya Bw Abdallah kuiendesha familia yake kuelekea nyumbani mara shughuli ya makabidhiano ilipoisha.

“Hatimaye sasa nimeamini kabisa kuwa mimi ndiye kweli mshindi wa zawadi kubwa ya shindano hili ingawa nilipata taarifa ya ushindi wangu katikati ya mwezi jana,” mwanakijiji huyo mwenye umri wa miaka 50 na mzazi wa watoto watano alisema baada ya kuliwasha gari hilo la kisasa kwa mbwebwe za kiushindi.

Akitabasamu kwa furaha mkulima huyo ambaye pia ni mfanyabiashara alisema mpaka anakbidhiwa rasmi zawadi hiyo aliuchukulia ushindi wake kama ndoto kwa sababu kadhaa.

“Kwanza niliona uwezekano wa mimi kuishinda hii zawadi kubwa kama ndoto za alinacha. Pamoja na kuwa mteja mwaminifu wa NMB, kwanza mimi ni mwanakijiji harafu mfanyabiashara mdogo tu wakati benki hii ina zaidi ya wateja zaidi ya milioni nne wakiwemo matajiri wakubwa,” amefafanua.

“Ushindi wangu umenifunza jambo jingine kubwa kuhusu NMB. Kumbe ni benki ya kila Mtanzania bila kujali hadhi yake katika jamii na kiuchumi. Sizingekuwepo huduma za kibenki za kimtandao wala nisingekuwa hata mteja wake acha kuinyakua hii zawadi,” Bw Abdallah aliongeza kwa kicheko cha ushindi.

Aidha ameipongeza taasisi hiyo ya fedha kubwa kuliko zote kwa mikakati yake wezeshi kama kampeni ya Bonge la Mpango ambayo uzinduzi wake mwanzoni mwa mwaka huu kuliweka viwango vipya kwa promosheni kutokana na zawadi zake lukuki zilizokuwa na thamani ya zaidi ya TZS million 500.

Amesema zawadi walizopata washindi zilikuwa pia ni mitaji hasa kwa watu wa kawaida na wajasiriamali wadogo kama yeye. Ili kuimarisha uhusiano na NMB, Bw Abdallah alisema anaenda kuwa miongoni mwa mawakala zaidi ya 9,000 wa benki hiyo.

Akizungumza kabla ya kumkabidhi zawadi yake kwenye Soko Kuu la Kingalu karibu na tawi la NMB la Wami, Kaimu Afisa Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani wa benki hiyo, Bw Benedicto Baragomwa, amesema zawadi zilizonyakuliwa ni pamoja na pesa taslimu walizoshinda wateja 120.

Nyingine ni pikipiki za miguu mitatu 24 aina ya LIFAN na Kirikuu tatu za muundo wa TATA Ace.

Pia NMB ilifanya uwekezaji huo kwa ajili ya kutambua mchango wa wateja katika mafanikio yake ikiwemo kuandika historia katika tasnia ya kibenki kwa kupata faida kubwa kuwahi kutengenezwa na benki nchini ya TZS bilioni 206 mwaka 2020.

“Mwezi Februari tulizindua kampeni maalumu yenye makusudi ya kurejesha faida kwa wateja pamoja na kuhamasisha utamaduni wa kujiwekea akiba kwa Watanzania,” amesema Baragomwa.

“Leo ndo tumefikia kilele cha Bonge la Mpango…Kampeni hii ya miezi mitatu ililenga kuwahamasisha wasio na akaunti ya benki nchini kuja kufungua na kutunza akiba zao kwa njia salama zaidi na Benki ya NMB,” ameongeza.

Meneja wa Tawi la Uluguru,Lilian Abraham, alisema ana sababu kubwa mbili za kufurahia ushindi wa Bw Abdallah ambazo ni mshindi huyo kuwa mwanakijiji na kubwa zaidi kuwa mteja wa tawi lake ambapo ndipo kampeni ya Bonge la Mapngo ilipozinduliwa katika kanda ya Pwani.